Ukuta Simba na deni la msimu uliopita

Dar es Salaam. Wakati wakianza mechi ya kwanza ya ligi kuu msimu huu bila kuruhusu bao dhidi ya Tabora United, mabeki na makipa wa Simba wana kibarua cha kufuta takwimu mbaya za msimu uliopita za safu yao ya ulinzi.

Takwimu hizo ni za kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara nyingi zaidi kwa msimu mmoja ukiwa ndio pekee ambao ilifungwa mabao mengi kati ya misimu mitano iliyopita.

Kabla ya msimu uliopita, Simba haikuonekana kuwa na udhaifu mkubwa kwenye safu ya ulinzi na hilo linathibitishwa na takwimu za ligi hiyo.

Katika msimu wa 2022/2023, Simba iliongoza kwa kufungwa mabao machache zaidi kwenye Ligi Kuu ambapo iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara 17.

Msimu wa 2021/2022, Simba ilishika nafasi ya pili katika chati ya timu zilizofungwa mabao machache kwenye ligi ambapo iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14 na kınara ilikuwa ni Yanga iliyofungwa mabao nane.

Msimu wa 2020/2021, Simba ilimaliza ikiwa imefungwa mabao 14 na ndio iliongoza kwa kufungwa mabao machache kama ilivyofanya msimu wa 2019/2020 ambapo iliongoza tena kwa kuwa na safu imara ya ulinzi iliyofungwa mabao 21 tu.

Beki wa zamani wa timu hiyo, George Masatu alisema kilichoigharimu Simba kufungwa mabao mengi msimu uliopita ni majeraha.

“Wachezaji wengi walikuwa wanasumbuliwa na majeraha, hivyo ilikuwa ni ngumu kucheza kwa kiwango kinachotakiwa, kwani wanakuwa wanalinda ajira zao.

“Ila  kuhusiana na wapya ngoja tuwape angalau mechi tatu, ndipo tutakapoona mwelekeo wao,” alisema Masatu.

Kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Mohammed Banka, alisema “msimu uliopita baadhi ya walinzi wa Simba hawakuwa na ujitoleaji mzuri uwanjani jambo ambalo lilichangia kufungwa mabao mengi.

“Na kuhusu wachezaji wapya natumaini watafanya vizuri kwani mpaka sasa wameshacheza michezo ya kiushindani mitatu na wameruhusu bao moja tu kwenye mchezo wa Ngao ya jamii dhidi ya Yanga,” alisema Banka.

Related Posts