Dar es Salaam. Nyota wa zamani wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Nicodemus Njohole amefichua kuwa angeweza kuandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England (EPL) ikiwa asingekutana na urasimu hapa nchini.
Njohole anasema alifuzu majaribio katika timu za Arsenal na Bournemouth ambazo zote zilitaka kumsajili lakini alikwama kupata kibali cha kutambulika na kilichokuwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) jambo lililofanya ndoto zake zisitimie.
Hayo ameyafichua katika mahojiano maalum aliyofanya na timu ya waandishi wa Mwananchi Communications Limited, Magomeni, Dar es Salaam juzi.
Anasema baada ya kucheza kwa mafanikio katika kikosi cha Simba mwaka 1982, alisafiri kwenda England kutafuta fursa nzuri zaidi kwa ajili ya maisha yake ya kimpira.
“Mmoja kati ya marafiki zangu wa karibu, Mzee Maulid ambaye alikuwa anafanya kazi katika kampuni ya madini England akiiwakilisha kampuni ya Tanzania, alinialika nikasake malisho ya kijani kule.
“Kama unavyofahamu enzi hizo na hadi sasa, kila mcheza soka ana ndoto za kucheza nje. Kwangu mimi ilikuwa fursa ya dhahabu kwa vile nilikuwa katika daraja la juu la ubora na kundi kubwa la mashabiki,” anasema Njohole.
Njohole anasema kuwa baada ya kukamilisha taratibu zote na kusafiri kwenda England, mwenyeji wake alimpokea vyema na alikuwa tayari ameshamuandalia timu ya kufanya majaribio.
“Baada ya siku chache nilishiriki program ya mazoezi na AFC Bournemouth. Ilikuwa ni nyakati kubwa kwangu kwa vile benchi la ufundi lilikoshwa na ufundi wangu na likapendekeza nijiunge na timu.
“Waliniambia niwape kibali kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) lakini hapo ndio matatizo yalianzia. Mzee Maulid na mimi tuliwasiliana na maofisa wa FAT lakini hawakutoa mrejesho na hakuna aliyekuwa tayari kunisaidia,” anafichua Njohole.
Baada ya mpango huo wa kujiunga na Bournemouth kushindikana, Mzee Maulid alimuandalia majaribio ya kujiunga na Araenal ambayo yalikubaliwa.
Hata hivyo Njohole aliambiwa kuwa atapata fursa ya kuhudhuria mazoezi ya Arsenal ikiwa atakuwa na kibali cha FAT na kibali cha kufanya kazi.
“Arsenal walikuwa tayari kunipokea katika mazoezi yao kutoka na kiwango nilichoonyesha na AFC Bournemouth lakini kwa mara nyingine tena nilitakiwa kuwasilisha nyaraka zilezile. Huo ukawa mwisho wa stori yangu ya kucheza England,” anafafanua Njohole.
Baada ya hapo, Njohole anasema rafiki yake Mzee Maulid aliwasiliana na Kassim Manara aliyekuwa akicheza soka la kulipwa Austria ili kuona kama anaweza kupata fursa ya kucheza huko.
Anasema kuwa Kassim Manara alilipokea kwa mtazamo chanya na Njohole akasafiri kwenda Austria ambako alipata timu ya kuchezea.
Njohole anasema kuwa akiwa Austria aliichezea SV Wernberg kuanzia 1982 hadi 1983 na kujiunga na ASKo Raika Furnitz aliyoichezea hadi 1998 alipoamua kustaafu.