Rukwa. Wakulima mkoani Rukwa wameitaka Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kuharakisha kuwalipa malipo yao pindi wanapokwenda kuuza mazao yao ili wajikwamue kiuchumi.
Wakulima wametoa wito huo kufuatia malalamiko yao ya kutumia muda mrefu katika vituo vya ununuzi wakisubiri malipo yao bila mafanikio, jambo linalowakwamisha kufanya shughuli nyingine za kiuchumi.
Mkulima wa kata ya Mazwi, manispaa ya Sumbawanga, Anselimo Mahenge ameliambia Mwananchi leo Alhamisi Agosti 22, 2024 kuwa wamekuwa wakipoteza muda kwenye vituo vya mauzo kusubiri malipo baada ya kupeleka mazao.
“Awali, nilipoleta mazao niliambiwa malipo yatafanyika siku mbili baada ya kuuza mahindi, lakini hadi sasa ni wiki mbili sijapata pesa yangu. Pia kumekuwa na changamoto ya foleni, naomba NFRA kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha wakulima hatutumii muda mwingi kukaa kwenye kituo cha ununuzi,” amesema Mahenge.
Naye mkulima kutoka Matai, Wilaya ya Kalambo, Samson Gadau ameomba NFRA kuongeza kasi ya upimaji kwani wakulima wengi wanaendelea kupeleka nafaka kwenye vituo hivyo vya ununuzi wa mazao.
“Hatutarajii kukopwa, wakinunua tu watulipe maana ndiyo tunazitegemea hela hizo kwa mambo mbalimbali ya kifamilia,” amesema Gadau.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu suala hilo, Meneja wa NFRA Mkoa wa Rukwa, Marwa Range amesema lengo la Serikali kununua nafaka ni kuwarahisishia wakulima kwenye mauzo ya mazao yao kwa urahisi.
Amesema katika vituo vyao mkoani humo wanatumia mizani ya kidigitali kupima uzito wakati wa kununua nafaka kwa wakulima, huku akiwaotoa hofu kuwa hakuna mkulima atakayedhulumiwa malipo yake.
“Wakulima wote na hasa wadogo, wasisite kuleta nafaka, tumepanga kununua mahindi meupe katika msimu huu, wahakikishe wanaleta nafaka hizo katika ubora wa hali ya juu unaotakiwa,” amesema Marwan a kuongeza:
“Hatutarajii kumkopa mkulima yeyote, wote watalipwa kwa wakati, tena kwenye vituo vyao vya ununuzi,” amesema meneja huyo.
Ameongeza kuwa vituo ambavyo vinaendelea na ununuzi kwa Sumbawanga ni Mazwi, Kanondo na Laela huku kwa Wilaya ya Kalambo ni Matai na Mkombo na wilayani Nkasi ni Namanyere, Mtenga Kasu na Ntalamila.