Harris, mwenye umri wa miaka 59, alimteuwa Walz, mwenye umri wa miaka 60, kuwa mgombea mwenza wake siku 15 tu zilizopita. Harris mwenyewe aliingia kinyang’anyiro cha White House mwezi mmoja uliopita wakati Rais Joe Biden alijiondoa katika kampeni za uchaguzi wa rais wa Novemba 5.
Walz, ana ulimi mwepesi ambao maramoja ulianza kuwashambulia Trump na mgombea mwenza wake JD Vance. Wademocrat wenye hamu ya kuungana na kusimama nyuma ya mgombea wanayeamini ana nafasi nzuri zaidi kuliko Biden, mwenye umri wa miaka 81, wamevunja rekodi kwa kuchangisha dola milioni 500 ili kusimamia kampeni ya Harris, ambaye ni makamu wa Biden.
Walz, ambaye amesifiwa na Wademocrat kwa kumuunga mkono Harris na wanawake wengine, alizungumzia kukua kwake mashambani Nebraska, familia yake na uhuru ambao Wademocrat wanasema unashambuliwa na Trump, ambaye anatafuta kuingia katika Ikulu ya Marekani.
Hotuba kuu ya Walz katika siku ya tatu ya mkutano mkuu wa chama unaofanyika Chicago inafuatia hotuba zenye kusisimua kutoka kwa vigogo wa Democratic akiwemo Rais Barack Obama na mkewe Michelle na Hillary Clinton, mgombea wa zamani wa rais, seneta wa Marekani na waziri wa mambo ya nje. Harris, mwenye umri wa miaka 59, atauhutubia mkutano huo kwenye siku yake ya mwisho Alhamisi.
Chanzo kimoja kimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa mgombea huru Robert F. Kennedy anatumai kufikia makubaliano na Trump ambapo atajiondoa kinyang’anyironi ili naye apewe kazi katika serikali mpya ya Trump. Uungwaji mkono wa Kennedy unaweza kumsaidia Trump katika uchaguzi ambao uchunguzi wa maoni unaonesha huenda ukawa mchuano mkali. Trump alikutana na Kennedy mwezi uliopita kujadili uwezekano wa kupata uungwaji mkono wake.
Uchunguzi wa maoni ulimuonesha Biden akiwa nyuma ya Trump kabla ya rais huyo Mdemocrat kumwachia Harris nafasi hiyo, na sasa utafiti huo unaonesha Harris akiwa mbele ya mpinzani wake huyo Mrepublican katika majimbo kadhaa ambayo yataamuwa matokeo ya uchaguzi.
Walz ameleta haiba ya kitamaduni kwenye kampeni za Harris, akijielezea yeye na Harris kuwa wapambanaji machachari wanaolenga katika mustakabali bora wa Marekani na kuwatuhumu Warepublican kwa kuzusha hofu na mgawanyiko nchini.
Kuna video itakayongazia huduma ya Walz katika Jeshi la Ulinzi wa Taifa, licha ya tuhuma za chama cha Republican kuwa alidanganya cheo chake katika jeshi hilo ambako alihudumu kwa miaka 24. Maafisa wa timu ya Kampeni za Harris wanaitegemea mizizi ya Walz na mtindo wake wa uzungumzaji kuwavutia baadi ya Wamarekani weupe katika maeneo ya vijijini ambao walimpigia Trump kwa idadi kubwa katika uchaguzi uliopita — na kusaidia kuzoa kura katika majimbo kama vile Michigan, Pennsylvania na Wisconsin.