Walz akubali rasmi kuwa mgombea mwenza wa Kamala Harris – DW – 22.08.2024

“Shukrani. Kwanza kwa Makamu wa Rais Harris. Ahsante kwa kuniamini na kunialika kuwa sehemu ya kampeni hii kubwa kabisa. Na shukrani kwa Rais Joe Biden kwa miaka minne ya uongozi uliotukuka. Ni heshima kubwa maishani mwangu kukubali uteuzi wenu kuwa makamu wa rais wa Marekani. Tupo hapa sote usiku huu kwa sababu moja nzuri na nyepesi: tunaipenda nchi hii. Kwa hivyo, ahsanteni.” Alisema Gavana Walz mbele ya maelfu ya wafuasi wa chama chake cha Democrat waliokuwa wakionesha mabango yaliyoandikwa “Kocha Walz”, kuonesha kumuunga mkono mgombea mwenza huyo, ambaye aliwahi kuwa mwalimu na kocha wa mpira.

Soma zaidi: Walz ahutubia mkutano mkuu wa chama cha Democratic Marekani

Walz hakuwa akifahamika sana kwenye ngazi ya taifa na Wamarekani wengi walilisikia kwa mara ya kwanza jina lake alipotajwa na Kamala Harris kuwa mgombea mwenza wake, lakini tangu wiki ya kwanza ya kampeni zake amekuwa akijizolea umaarufu kwa jinsi anavyoweza kutumia historia yake binafsi kujenga hamasa za wapigakura.

Bill na Show

Hotuba ya Walz kwenye mkutano huo ilifuatiliwa na ya rais wa zamani, Bill Clinton, ambaye alimponda mgombea urais wa Republican, Donald Trump, kama mtu mbinafsi na kumsifia Kamala Harris kama mtu aliyejikita kwenye mahitaji ya Wamarekani.

USA, Chicago | mkutano wa Democrat | Tim Walz
Mkutano Mkuu wa chama cha Democrat mjini Chicago, Marekani.Picha: J. Scott Applewhite/AP/picture alliance

“Kwa hivyo mwaka 2024, tuna chaguo zuri na la wazi. Kamala Harris ni kwa ajili ya watu na kwa huyu jamaa mwengine ambaye amethibitisha zaidi ya mara moja kwamba yeye ni kuhusu mimi, mwenyewe na peke yangu.” Alisema Clinton.

Soma zaidi:Barack Obama atarajiwa kuhutubia kwenye siku ya pili ya mkutano wa DNC 

Mbali ya wanasiasa wakubwa wa Democrat waliohudhuria mkutano wa usiku wa jana, alikuwapo pia mtangazaji mashuhuri, Oprah Winfrey, ambaye alitumia jukwaa hilo kuwataka Wamerakani wajitokeze kwa wingi kupiga kura hapo Novemba 4.

“Kuna mambo ya kuchaguwa wakati tunapopiga kura zetu. Sasa, kuna mgombea mmoja anayesema kwa uwazi kwamba tukenda kwenye vituo mara hii, huenda tusiweze tena kufanya hivyo. Mnamjua ni nani. Lakini leo mbele yenu ni mtu huru ambaye anaona fahari kupiga kura tena na tena kwa sababu mimi ni Mmarekani na hicho ndicho Wamarekani wanachofanya.” Alisema Oprah.

Wajumbe wa chama hicho wamekusanyika kwenye ukumbi wa United Center mjini Chicago wakitazamia kuendeleza hamasa iliyorejea kwenye kampeni zao tangu Kamala Harris achukuwe nafasi ya Joe Biden kuwania urais mwezi uliopita.

Vyanzo: Reuters, AP, AFP

Related Posts