WAKATI mashabiki wa Yanga wakiendelea kuchekelea ubora wa kikosi chao, upo moto unaoiunguza timu hiyo ndani kwa ndani.
Yanga kwa misimu mitatu sasa imekuwa ikitingisha katika ligi za ndani na michuano ya kimataifa kutokana na kufanya usajili mzuri wa wachezaji bora wanaoibeba, lakini ikijikuta pia ikipata hasara kutokana na usajili unaofanywa.
Iko wazi kuwa kati ya timu zilizofanya vizuri katika michuano ya Afrika ndani ya misimu mitatu ya karibuni, Yanga haikosi na ni ukweli usiopingika kuwa imeshiriki kuifanya Ligi Kuu Bara kushika nafasi ya sita kwa ubora Afrika.
Licha ya hayo, rekodi hizo, ikiwa imebeba ubingwa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo kama ilivyo kwa Kombe la Shirikisho, ikifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-23 na kubeba Ngao ya Jamii mwaka huu.
Mafanikio hayo yamechagizwa na usajili wa kibabe ilioufanya msimu huu, huku ikimchukua kiungo mshambuliaji kutoka Simba, Clatous Chama na Prince Dube aliyekuwa Azam FC, pamoja na wengine wakiongezewa mikataba akiwamo mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Aziz Ki na Djigui Diarra aliyekuwa kipa bora wa ligi misimu miwili mfululizo 2021-22 na 2022-23.
Mastaa wengine wapya wa kimataifa ni pamoja na Duke Abuya kutoka Kenya, Jean Baleke aliyewahi kuichezea Simba na Chadrack Boka (FC Lupopo), huku wakiwatoa wachezaji wa kimataifa kama Agustine Okrah aliyewahi kuichezea Simba, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ kutoka Sauzi na Mganda Gift Fred.
Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, wamekuwa bora kwa misimu mitatu mfululizo, lakini ndani ya kipindi hicho kuna kitu hakipo sawa katika vipindi tofauti vya usajili.
Hiyo imetokana na baadhi ya wachezaji iliowasajili na kuwaondoa ndani ya kipindi cha muda mfupi kuwasilisha malalamiko yao FIFA kudai malipo ambayo yamekuwa yakiichafua kwa namna moja ama nyingine kama ilivyo kwa sasa wa Augustine Okrah aliyesajiliwa dirisha dogo lililopita kisha kutemwa ghafla.
Klabu hiyo imekuwa ikiingia gharama zisizo za lazima kwani baadhi ya wachezaji waliowaondoa hawakutumika muda mrefu na wanapovunja mikataba inabidi kuwalipa pesa nyingi.
Augustine Okrah aliyesajiliwa dirisha dogo msimu uliopita, alipata majeraha katika michuano ya Kombe la Mapinduzi akitokea benchi, jambo lilipolekea kukaa nje mpaka mashindano hayo yalipomalizika. Hata katika ligi kocha Miguel Gamondi alikuwa hamtumii muda mwingi na hata alipochezeshwa ilikuwa ni dakika chache akitokea benchi, hii inaonyesha kwamba hakuwa na cha ziada kuwazidi aliowakuta katika eneo la winga.
Okrah alisaini mkataba wa miaka miwili na alipovunjiwa baada ya kudumu kwa miezi sita, Yanga ilitakiwa kumlipa Dola 80,000 (zaidi ya Sh216 milioni) kama fidia ya kusitisha makubaliano hayo.
Mamadou Doumbia beki kutoka Mali, alisajiliwa Januari 2023 akaachwa mwisho wa msimu wa 2023-2024 akidumu kwa miezi sita wakati wa kocha Nasreddine Nabi, mkataba ulipositishwa Yanga ilimlipa Dola 50,000 ambazo ni zaidi ya Sh135 milioni.
Tangu atue Yanga alicheza dakika 45 katika mechi ya Kombe la Shirikisho Azam dhidi ya Rhino Rangers na kilichomfelisha na ukamilifu imara wa safu ya ulinza Yanga inayoongozwa na Dickson Job, Ibrahim Bacca na Bakari Mwamnyeto.
Kiungo kutoka Burundi, Gael Bigrimana alisaini mkataba wa miaka miwili Julai 2022 akacheza msimu mmoja tu wa 2022-23, Yanga ilimtema na kuingia gharama za kumlipa Dola 300,000 ambazo ni zaidi ya Sh700 milioni.
Wapo wengine ambao walisajiliwa na kutumika msimu mmoja lakini hawakuingia katika hesabu za kocha licha ya fidia zao kutokuwekwa wazi lakini nao walivunjiwa mikataba, wachezaji hao ni pamoja na Skudu Makudubela, Hafiz Konkoni, Gift Fred na Lazarous Kambole.
Wachezaji watatu pekee Okrah, Doumbia na Bigirimana, Yanga ililazimika kuwalipa Dola 430,000 ambazo ni zaidi ya Sh1.6 bilioni katika kuwalipa baada ya kuvunja mikataba huku nyota hao wakiwa na mchango mdogo katika mafanikio ya timu hiyo.
Katika ripoti ya mapato na matumizi ya Yanga kwa msimu wa 2023/2024, klabu hiyo ilipata hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Yanga uliofanyika Juni 2024, ilionyesha kwamba Yanga ilipata mapato ya jumla ya Sh 21.19 bilioni lakini matumizi yalikuwa ni Sh22.29 bilioni, hivyo kuingiza hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni huku ishu ya usajili na uhamisho wa wachezaji ikionekana kutumia Sh3.5 bilioni.
Mbali na masuala ya usajili yaliyoonekana kutumia kiasi kikubwa cha fedha, lakini katika gharama za mishahara kwa wachezaji na benchi la ufundi zilitumia sehemu kubwa zaidi ya bajeti hiyo ikifikia Sh7.39 bilioni ikiwa ndiyo gharama kubwa zaidi katika bajeti hiyo.
Viongozi wa Yanga walitafutwa jana ili kutoa ufafanuzi kipi kinachochangia hali hiyo kutokea na hasara wanazozipata kila mara wanazichukuliaje, lakini simu zao zilikuwa zikiita bila kupokewa.
Hata hivyo, baadhi ya nyota wa zamani nchini walitoa maoni juu ya hali hiyo akiwamo kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema timu kubwa kama Yanga inachohitaji ni uchunguzi wa muda mrefu ili kuweza kufahamu mchezaji yupi anaifaa.
“Waongeze skauti kubwa ili kupunguza matukio ya kesi kama hayo, kwani sio sifa nzuri kwa klabu kama ile kuwa na sifa za namna hiyo, hata hivyo wana kikosi kipana ndio maana kabla hawajawaza kusajili wajue madhaifu yapo kwa ukubwa gani,” alisema Chambua na kuongeza:
“Kuwa na wachezaji wengi ni vizuri lakini mahitaji ndio jambo la msingi kama kuna eneo wapo wa kutosha basi haina haja ya kusajili zaidi.”
Mshambuliaji wa zamani Simba, Dua Said alisema: “Uongozi wa Yanga ujipange upya na ikiwezekana matukio haya yawe mwisho ili kuunda kikosi chenye sifa bora ndani na nje. Klabu kubwa inatazamwa na wengi hivyo kama itakuwa na makosa basi wapo watakaowaiga, ila jambo la msingi la kushauri ni utulivu wa hali ya juu ufanyike ili kupata kitu kilicho bora na kuchukua mchezaji ambaye alikotoka alikuwa akicheza.”