Aliyeua wenza aachiwa huru | Mwananchi

Arusha. Mahakama ya Rufani iliyoketi Mwanza, imemuachia huru Elias James, ambaye mwaka 2020 alihukumiwa adhabu ya kifo kwa tuhuma za kuwaua kwa kutumia panga Zawadi Balthazary na Daud Phares ambao ni mke na mume.

Kulingana na kosa lilivyokuwa, ilidaiwa siku ya tukio, baada ya kuwaua wanandoa hao, naye alijijeruhi kwa kujikata kwa kutumia kisu, koo na tumbo lake, hali iliyosababisha utumbo wake kutoka nje.

Septemba 18, 2020 Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, ilimtia hatiani kwa makosa mawili ya mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Katika rufaa hiyo ya jinai namba 640 ya mwaka 2020, iliyotolewa uamuzi wake Agosti 12, 2024, aliachiwa huru baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha makosa hayo bila kuacha shaka.

Hukumu hiyo ambayo nakala yake ipo kwenye mtandao wa mahakama, ilitolewa na jopo la majaji watatu ambao ni Stella Mugasha, Lameck Mlacha na Paul Ngwembe.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Mugasha amesema mbali na hoja hiyo, pia Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo hakufanya majumuisho ya kuwaelekeza wazee wa baraza mambo muhimu ya kisheria yanayohusiana na kesi kabla ya kuwahitaji kutoa maoni yao.

Ilidaiwa Oktoba 5, 2017 saa sita mchana katika Mtaa wa Posta Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Elias aliwaua wanandoa hao.

Ilidaiwa wanandoa hao waliokuwa wakiishi na watu wengine nyumbani kwao akiwemo kaka wa Daud ambaye ni Ibrahim Phares (shahidi wa pili), ambaye alidai awali Septemba 30, 2017 polisi watatu wakiwa na raia mmoja asiyefahamika, walikwenda nyumbani hapo na kuwaulizia.

Alidai kuwa baada ya Zawadi kutoka nje, alikamatwa na polisi akidaiwa kuiba vyombo na pesa na baadaye alikuja kuachiwa huru Oktoba 4, 2017.

Alidai siku iliyofuata Oktoba 5, 2017 akiwa kazini kwake mashine ya kusaga, alipewa taarifa na rafiki yake aliyedai kuona panga likiwa na damu nje ya makazi ya wanandoa hao.

Ibrahim alidai kukimbilia eneo la tukio na baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo, alimkuta Zawadi akiwa amejilaza, huku akivuja damu nyingi na akiwa pale alimtambua mtu mmoja ambaye alikuwa ameshikilia kisu chenye damu.

Alidai mtuhumiwa huyo alipojaribu kumsogelea, alikimbia na kutoroka, huku mtuhumiwa huyo (Elias) akijifungia ndani ya nyumba na Ibrahim alipojaribu kuchungulia dirishani, alimuona mtuhumiwa huyo alitumia kisu kukata koo lake na tumbo na kusababisha utumbo kutoka nje.

Shahidi wa kwanza ambaye ni mtoto wa marehemu, Torokoko Phares, alidai siku ya tukio aliona marehemu wakishambuliwa na kuwa hakumbuki kumuona Daud kwenye eneo la tukio.

Alidai siku hiyo ya tukio alimtembelea baba yao ambaye alikuwa akiishi na (Zawadi) mama yao wa kambo, alishuhudia wazazi wake wakiuawa na kuwa mtu wa kwanza kushambuliwa alikuwa Zawadi, huku akidai kuona baba yake akipambana na washambuliaji hao na kutokana na tukio hilo alilazimika kukimbia.

Ofisa wa Polisi, Bwire aliyechunguza tukio hilo, alidai alipofika eneo la tukio alimkuta mshambuliaji amejifungia ndani ya nyumba na nje kulikuwa na panga lililotapakaa damu. 

Alidai baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo, miili ya marehemu ilikutwa ndani ya nyumba hiyo na mtu aliyekuwa amejifungia ndani nyumba aliyekuwa amejijeruhi akiwa juu ya kitanda ameshika kisu na utumbo wake ukiwa umetoka nje ya tumbo.

Kwa mujibu wa kumbukumbu hizo za mahakama, zinaonyesha upande wa mashtaka uko kimya kuhusu kilichojiri baada ya mtu anayedaiwa kuwa mrufani kufikishwa hospitalini.

Pia, hakuna ushahidi unaoonyesha iwapo mtu huyo anayedaiwa kuwa ni Elias alikamatwa na ofisa yeyote wa polisi au mgambo kabla ya kufikishwa mahakamani huku kukiwa hakuna ripoti ya kimatibabu kuhusu mtu huyo.

Katika utetezi wake, Elias alidai Septemba 10, 2017 alikuwa ufukweni mwa Ziwa Victoria , eneo la Kisorya, ambako alikamatwa na polisi akituhumiwa kwa uvuvi haramu.

Alidai Oktoba 12, 2017 aliwekwa chini ya ulinzi ambapo aliteswa na kupoteza fahamu, alipopata fahamu, alilazimishwa kusaini karatasi ambazo alizikataa na kukanusha kuwafahamu marehemu.

Baada ya Jaji wa Mahakama Kuu kusikiliza kesi pande zote mbili, mmoja wa wazee wa baraza alitoa maoni kuwa Elias ana hatia huku wazee wawili wa baraza wakieleza kuwa Elias hana hatia.

Elias aliwasilisha sababu tano za rufaa ikiwemo Jaji alikosea kisheria kubaini upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi bila shaka yoyote.

Nyingine ni Jaji kukosea kisheria kutokufanya majumuisho kwa kuwaelekeza wazee wa baraza masuala muhimu ya kisheria kabla ya kuwahitaji kutoa maoni yao.

Katika rufaa hiyo Elias aliwakilishwa na Wakili Julius Mushobozi huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali mwandamizi Tawabu Issa na Felix Mshana.

Wakili Julius amesema mahakama haikufanya majumuisho hayo kwa mujibu wa kifungu cha 265 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Kwa upande wake Wakili Issa alikiri majumuisho hayo kutokufanyika ipasavyo na kuomba mahakama aiamuru majumuisho sahihi yakafanyike kwa wazee hao wa baraza kwa mujibu wa sheria na kuomba Mahakama irudishe jalada Mahakama Kuu ili majumuisho yakafanywe upya.

Jaji Mugasha amesema pamoja na ushahidi wa utetezi kutojumlishwa kwa wazee wa baraza, Jaji alishawishi maoni ya wazee hao katika muktasari huo kwa hiyo wazee hao hawakuwa na uwezo wa kutoa maoni yenye mantiki juu ya hatia au vinginevyo vya mrufani.

Jaji Mugasha alieleza kuwa wanakubaliana na mawakili wa pande zote mbili kuwa Jaji aliyesikiliza kesi hiyo hakutoa majumuisho ipasavyo kwa wazee wa baraza juu ya mambo muhimu ya kisheria yanayohusika katika kesi kama inavyotakiwa.

Alieleza katika majumuisho hayo yanayopatikana katika ukurasa wa 43 na 44 wa kumbukumbu za rufaa, Jaji wa Mahakama Kuu alitoa muktasari wa mashahidi wa upande wa mashtaka, hakujumlisha ushahidi uliotolewa na upande wa utetezi.

“Kutokuwepo huko kulifanya wazee wa bazara wasiweze kutoa maoni muhimu kwa Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi, ambayo pia ilipunguza thamani ya maoni yao, kwa sababu hiyo, tunakubaliana na mawakili kwamba, muhtasari haikuendeshwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Jaji.

Kuhusu kuthibitishwa kwa kosa bila kuacha shaka, Jaji Mugasha akimnukuu Wakili Julius, alieleza kutokana na mazingira ya kosa hilo, hakuna uhakika iwapo mtu aliyebainika kujeruhiwa katika eneo la tukio na kupelekwa hospitali ni mrufani anayedaiwa kuua watu wawili.

Jaji Mugasha amesema swali muhimu la kujibiwa ni nani aliua watu hao wawili na kuwa wamegundua katika kumbukumbu hiyo hakuna ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ili kubaini hatima ya mtu ambaye alipatikana akiwa amejeruhiwa eneo la tukio na Elias.

 “Kutokuwa na uhakika kungeondolewa ikiwa daktari angeitwa kutoa ushahidi, juu ya majeruhi aliyepekwa hospitalini,” amesema.

Jaji Mugasha amesema katika mazingira hayo haiwezi kuthibitishwa kuwa majeruhi aliyekuwa eneo la tukio na kupelekwa hospitali na aliyehusika na tukio la mauaji ni Elias, ambaye alifikishwa mahakamani.

“Sintofahamu hiyo inathibitishwa zaidi na upande wa utetezi wa mrufani ambao ulieleza kuwa alikamatwa Oktoba 10, 2017 kando ya Ziwa Victoria, eneo la Kisorya kwa tuhuma za uvivu haramu.

“Pamoja na kwamba tunasikitika kupoteza maisha ya binadamu, mikono yetu imefungwa na sheria na hatuna zaidi ya kushikilia kwamba shitaka dhidi ya mrufani halikuthibitika hadi mwisho kutokana na upungufu wa hati ya mashtaka ambayo haimuunganishi mrufani na kosa aliloshtakiwa,” amesema Jaji Mugasha.

Jaji Mugasha amesema kwa kuzingatia yale ambayo wamejaribu kuonyesha, majumuisho mapya ya wazee wa baraza yasingekuwa kwa maslahi ya haki na kuwa msingi huo wa kutothibitishwa kwa kosa unatosha kuondoa rufaa, hivyo hawataamua sababu zilizosalia za rufaa na kumuachia Elias huru.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts