Awesu atoa msimamo Simba SC, afungukia bao dhidi ya Tabora

KIUNGO mpya wa Simba, Awesu Awesu ametoa msimamo baada ya kukiri alikuwa na ndoto za muda mrefu za kuichezea timu hiyo, lakini sasa ana kazi na kuelekeza nguvu kubwa kutumia kipaji alichonacho  kutoa mchango wa kuifikisha mbali timu hiyo.

Nyota huyo aliyewahi kutamba na Azam FC, Kagera Sugar na KMC, amelizungumzia pia bao la kwanza aliloifungia Simba katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Tabora United, kwamba ni mwanzo mzuri na mashabiki wakae kwa kutulia ili kuendelea kupata burudani zaidi.

Kwa mara ya kwanza, Awesu alifuatwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati wa Usajili wa Simba, marehemu Zacharia  Hans Poppe Machi 19, 2017, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, Simba ilikuwa ugenini dhidi ya Madini FC, mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA).

Hata hivyo, dili hilo lilikufa na kutua katika klabu nyingine kabla ya msimu huu kusajiliwa kama utani akitokea KMC na kufunga bao wakati timu hiyo ikishinda 3-0 akitokea benchini na akizungumza na Mwanaspoti, alisema jinsi alivyokuwa akisubiri fursa hiyo kwa muda mrefu.

Awesu alisema anaona ni muda wa kufanya kile alichokitamani ndani ya klabu hiyo na kwamba hatawaangusha Wanasimba.

“Kusema ukweli ilikuwa ndoto yangu siku moja niicheze Simba, naamini nitakuwa na msimu mzuri, ingawa ushindani wa namba ni mkali, lakini nitapambana kwa kadri niwezavyo,” alisema Awesu na kuongeza;

“Simba ina kikosi kizuri na cha vijana, hivyo kila mmoja yupo kwa ajili ya kuhakikisha malengo ya klabu yanatimia.”

Awesu aliyekaribia kurudishwa KMC kutokana na klabu hiyo kugomea usajili wa awali kiasi cha kufikishana TFF, pia amewahi kukipiga Mwadui na Singida Utd akisifika kwa uwezo wa kutoa pasi za mwisho na kufunga timu mabao.

Related Posts