AZAM imetua salama jijini Kigali, Rwanda tayari kwa mchezo wao wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika lakini kuna kauli ameitoa kocha wao Yusuf Dabo, juu ya Wanajeshi hao wa Kirundi.
Azam iliyoondoka jana alfajiri na kutua Rwanda, itamalizana na APR, kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya mtoano baada ya awali matajiri hao wa Chamazi kushinda bao 1-0 nyumbani pale Azam Complex.
Azam inahitaji sare yoyote ili ifuzu kwenda hatua ya kwanza ya mtoano itakakokutana na mshindi wa mchezo wa Pyramids ya Misri dhidi ya JKU ya Zanzibar.
Akizungumzia mchezo huo wa marudiano Dabo alisema Azam yake wala haina presha kwani kupitia ushindi wa mchezo wa kwanza wameisoma APR inaingiaje.
Dabo alisema endapo APR itakuja na hesabu za kuwashambulia hiyo itakuwa faida kwa Azam kwani watatumia nafasi hiyo kuutanua ushindi wao.
“Mechi tuliyoshinda nyumbani ni dakika 90 za kwanza, nimewaambia wachezaji hizi ni dakika 90 za pili ambazo tunatakiwa kuwa makini kuzitumia ili tufuzu, tutaangalia wapinzani wetu wanaingiaje kwenye mechi hiyo,” alisema Dabo.