Dk Biteko: Serikali kutafuta ruzuku kupunguza gharama za nishati safi

Unguja. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema Serikali itahakikisha inatafuta ruzuku kupunguza gharama za nishati safi kwani kimekuwa kilio cha wananchi wengi.

Amesema hayo alipofungua mdahalo wa nishati safi leo Agosti 23, 2024, Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja.

Dk Biteko amesema gharama za nishati safi limekuwa tatizo kubwa kwa wananchi kushindwa kumudu, hivyo Serikali inafanya kila linalowezekana ipatikane kwa bei nafuu.

“Kila tunapokwenda watu wengi wanalalamika gharama kubwa ya kupatikana kwa nishati hiyo, Serikali tuna mkakati wa kutafuta kila aina ya ruzuku ili nishati safi ipatikane kwa bei nafuu,” amesema.

Ametoa wito kwa wadau, kampuni za gesi kutumia teknolojia itakayowasaidia wananchi kununua gesi kulingana na kiwango cha fedha zao na isiwe lazima kununua mtungi mzima.

Amesema Serikali itahakikisha inaungana na wadau wote kuandaa programu ya utoaji elimu na kufanya tathmini kutambua idadi ya wananchi walioacha kutumia nishati isiyosafi na kutumia iliyosafi.

Amesema takwimu zinaonyesha watu 2.4 bilioni duniani hawatumii nishati safi kati yao watu 933 milioni wanatoka Afrika.

Amesema watu milioni 3.7 wanakufa duniani kwa kutuma nishati isiyo safi na kati ya hao asilimia 60 ni wanawake na watoto.

Dk Biteko amesema hayo ni sababu ya nishati safi kuwa ajenda muhimu inayotekelezwa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kwa miaka 20 tumekuwa na hatua ya kuimarisha ajenda ya matumizi ya nishati safi ili kumaliza hili, kwani watu wengi wanatumia muda mwingi kupika kuliko kuzalisha,” amesema.

Amesema kila wanapokwenda kutoa elimu wanakutana na kauli ya kuwa wao ni masikini gharama zilizopo hawawezi kuzimudu lakini gharama ya kutumia nishati isiyokuwa safi ni kubwa zaidi.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Christina Mndeme amesema takwimu zinaonyesha hekta 469,420 za misitu zinapotea kila mwaka kutokana na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali, ikiwemo uvunaji wa miti kwa ajili ya kuni.

Amesema hali hiyo imekuwa ikisababisha madhara makubwa, ikiwemo kupunguza vyanzo vya maji, kuwepo kwa vipindi virefu vya ukame na kupotea bioanuai.

“Matumizi ya kuni na mkaa huchangia katika uchafuzi wa hali ya hewa kwa sababu ya uzalishaji mkubwa wa gesijoto na kuongeza vyanzo vya joto, kupungua kwa viwango vya hewa safi na oksejeni inayozalishwa na miti,” amesema.

Amesema Serikali inafanya jitihada katika kuhimiza matumizi ya nishati safi ikiwemo kuandaa Sera ya Mazingira ya mwaka 2021 inayoelekeza uhamasishaji mbadala wa gharama nafuu katika maeneo yote nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mahmoud amesema kiasi kikubwa cha wananchi mkoani humo hawatumii nishati safi, hivyo kuharibu mazingira ya hifadhi ya Jozani.

Amesema msitu wa Hifadhi ya Jozani ndiyo tegemeo la wananchi wa mkoa huo hivyo lazima elimu itolewe ili kupunguza changamoto hiyo.

Mwenyekiti wa Mwanamke Initiative Foundation (MIF), Wanu Hafidh Ameir amesema tamasha la Kizimkazi limekuwa chachu ya kuleta hamasa nchini hasa katika mageuzi ya nishati safi na salama ya kupikia.

Related Posts