Dk Mpango: Kilimo cha umwagiliaji kumaliza njaa

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya umwagiliaji unaenda kuandika historia ya kumaliza tatizo la njaa nchini na kulijengea Taifa heshima kupitia uwepo wa chakula cha kutosha.

Amesema anaridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji chini ya Wizara ya Kilimo, hivyo wananchi wawe tayari kuipokea miradi mikubwa ya sekta ya umwagiliaji itakayomaliza tatizo la uhaba wa chakula na kuimarisha kilimo cha uhakika.

Dk Mpango amesema hayo leo Agosti 22, 2024 akiwa ziarani mkoani Dodoma alipoweka jiwe la msingi katika ujenzi wa shamba la pamoja la Dk Samia Suluhu Hassan ambao unatekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ukiwa na thamani ya Sh21.7 bilioni.

“Hapa Dodoma kuna salamu ya Mkuliachi ambayo inamaanisha njaa, niwahakikishie kuwa, hiyo salamu inaenda kuisha kupitia uwekezaji unaofanywa na Serikali katika miradi hii mikubwa ya umwagiliaji, inaenda kuandika historia ya kumaliza tatizo la njaa nchini na kulijengea Taifa heshima ya uwepo wa chakula cha kutosha,” amesema.

Amesema Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inafanya kazi kubwa, na hatua hiyo ndiyo maana ya kubadili mifumo ya sekta ya kilimo na kuwa chenye tija na cha uhakika.

“Hili litakuwa eneo la mfano na mashamba haya yawe darasa, elimu ya kilimo itolewe hadi kwa vijana hususani kwa vitendo siyo maneno,” amesema.

Amepongeza hatua ya mradi huo kuhusisha ujenzi wa kituo cha afya na barabara  yenye urefu wa zaidi ya kilomita 18.8 unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Ameagiza eneo la barabara lililobaki ambalo lipo chini ya Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura) litekelezwe na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Mazao yatakayolimwa katika mradi huo ni soya, mtama, alizeti na mahindi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa amesema mradi huo una jumla ya ekari 11,000 na umekusudiwa kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa Halmashauri ya Chamwino na vijiji vyake, kupitia ujenzi wa nyumba za vijana, uwekaji wa miundombinu katika eneo la ekari 1,000 za kijiji na uandaaji wa zaidi ya ekari 400 katika eneo la mradi wa umwagiliaji wa vijana.

Mndolwa amesema kila kijana mnufaika wa mradi atapewa ekari 10 na mpaka sasa nyumba 60 za makazi zimekamilika kwa asilimia 50.

Amesema tume imepewa jukumu la kuandaa maeneo ya michezo, maghala na huduma nyingine za jamii.

Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde, amesema wizara imeelekeza halmashauri zote nchini kutenga maeneo yatakayotumika kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya vijana.

Related Posts