Jalada waliokuwa vigogo wa TPA lipo Takukuru kwa uchunguzi

Dar es Salaam. Serikali imesema bado wanaendelea na upelelezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),  Madeni Kipande (66) na wenzake watano.

Pia, jalada la kesi hiyo lipo Takukuru kwa ajili ya kupitiwa kwa sababu ilibainika kuwa kuna vitu bado havijakamilika.

Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Ijumaa Agosti 23, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Kipande na wenzake wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya dola za Marekani 1.85 milioni sawa na Sh4.2 bilioni.

Kasala alitoa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, anayesikiliza shauri hilo, ambapo alidai kuwa bado wanaendelea kuchunguzwa na baada ya uchunguzi kukamilika watatoa taarifa mahakamani hapo.

Katika hatua nyingine wakili wa utetezi, Kilian Mutasa amewasilisha maombi akiomba mteja wake anataka kubadilisha hati ya dhamana kwa kuweka kiwanja kingine kwa kuwa kiwanja hicho cha awali walichotumia kujidhamini, kinatakiwa kuendelezwa.

Alidai kutokana na ombi hilo anawasilisha hati nyingine yenye thamani kama ile ya awali ili  iweze kutumika katika dhamana.

Hata hivyo upande wa mashtaka walipinga ombi hilo kwa madai kuwa hawajapewa hati hiyo ya kiwanja waone na kufanya tathmini iwapo kina thamani sawa na masharti ya dhamana yaliyowekwa wakati washtakiwa hao wanapata dhamana.

Hakimu Magutu baada ya kusikiliza hoja za pande zote, alisema anaenda kwanza kupitia jalada kwa ajili ya kuthibitisha iwapo masharti ya dhamana yanaendana na thamani ya hati hiyo ya kiwanja, kisha atatoa maamuzi.

Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 24, 2024 itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Mbali na Kipande, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 38/2022 ni Peter Gawile (58) aliyekuwa Ofisa Rasilimali Watu wa TPA na mkazi wa Mianzini; Casmily Lujegi (65) mkazi wa Mbezi Juu na Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa TPA; Mashaka Kisanta (59) Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi, Kilian Chale (51) Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na Andrew John.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kati ya Oktoba Mosi, 2014 na Oktoba Mosi 2020 Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa la kuisababishia TPA hasara ya Sh4.2 bilioni.

Pia, kati ya Januari Mosi, 2015 hadi Februari 17,2015 washitakiwa kwa pamoja wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia dola za Marekani 1,857,908.04.

Shtaka la tatu, inadaiwa kati ya Oktoba Mosi, 2014 na Oktoba Mosi, 2020 eneo la TPA na maeneo mengine ya Dar es Salaam, washtakiwa kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP) bila kupata kibali cha bodi ya zabuni ya Mamlaka hiyo na kushindwa kufuata kanuni za zabuni hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya bodi hiyo, jambo lililosababisha TPA hasara ya dola za Marekani 1.8 milioni ambazo ni sawa na Sh4.2 bilioni.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Juni 30, 2022 na kusomewa mashtaka yao.

Related Posts