LONDON, ENGLAND: NDO hivyo. Uwezo wa kucheza nafasi nyingi tofauti uwanjani unamfanya Joao Felix kumpa machaguo ya kutosha kocha wa Chelsea katika namna ya kupanga kikosi chake msimu huu.
Chelsea imekamilisha usajili wa staa huyo wa Ureno kwa ada ya Pauni 42.6 milioni kutoka Atletico Madrid. Fowadi huyo alitumikia miezi sita kwa mkopo Stamford Bridge mwaka 2023, akifunga mabao manne katika mechi 20.
Felix, 24, ameshakoga sifa kutoka kwa kocha wake mpya Enzo Maresca kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi ndani ya uwanja.
Maresca alisema: “Felix ni mchezaji mzuri, ana kipaji. Nadhani kitu kizuri kuhusu yeye anaweza kucheza nafasi tofauti nje na ndani. Namba 9 na ndio maana tumemsajili.”
Felix sehemu kubwa ya maisha yake ya soka amecheza kwenye nafasi ya straika na huenda akatumika pia kwenye nafasi hiyo baada ya kutua Stamford Bridge badala ya Nicolas Jackson. Jambo hilo linaweza kumfanya staa huyo wa zamani wa Benfica kucheza kwenye safu ya washambuliaji watatu na atasimama kati, wakati Cole Palmer na Christopher Nkunku watakuwa kwenye wingi za kulia na kushoto.
Kocha Maresca anaweza kutumia safu hiyo mpya ya mastaa watatu mbele ya viungo Enzo Fernandez, Moises Caicedo na Romeo Lavia, ambao walianza kwenye mechi ya kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Manchester City katika mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu England.
Safu ya ulinzi inaweza kubaki vile vile ya wakali wanne, Marc Cucurella, Wesley Fofana, Levi Colwill na Malo Gusto mbele ya kipa Robert Sanchez.
Felix amekuwa na uwezo pia wa kucheza kwenye wingi ya kushoto. Kwa maana hiyo, kocha Maresca anaweza kumweka benchi Nkunku ili amtumie Felix kwenye upande huo wa kushoto. Kama Felix akianzia kwenye wingi, basi Jackson atatumika kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati.
Maresca anaweza kufanya mabadiliko pia kwenye kiungo kwa kumtumia Kiernan Dewsbury-Hall kwenye nafasi ya Lavia, huku kwenye beki atamtumia Tosin Adarabioyo kwenye nafasi ya Fofana na kipa Filip Jorgensen ataanza yeye golini.
Hata hivyo, Maresca anaweza kuchagua mtindo mwingine wa kiuchezaji na kumtumia Felix kwenye Namba 10 nyuma ya mshambuliaji wa kati.
Jambo hilo linaweza kuruhusu mabadiliko mengine kwenye safu ya ushambuliaji kwa maana ya Pedro Neto kupangwa kwenye wingi ya kushoto.
Kwa maana hiyo, kwenye ile safu ya washambuliaji watatu, akiwamo Palmer watakuwa wanapishana kwenye nafasi ya kucheza nyuma ya mshambuliaji wa kati, Jackson na kwenye kiungo ya kati kutakuwa na pacha ya Caicedo na Fernandez.