KITUO CHA AFYA MWANDOYA CHAPOKEA WAGONJWA WA KIPINDUPINDU ZAIDI YA 200 – MWANAHARAKATI MZALENDO

Kituo cha Afya Mwandoya, kilichopo katika jimbo la Kisesa, wilayani Meatu, mkoani Simiyu, kimepokea zaidi ya wagonjwa 200 wa Kipindupindu tangu ugonjwa huo uliporipotiwa kwa mara ya kwanza katika eneo hilo. Hali hii imezua taharuki miongoni mwa wakazi huku mamlaka za afya zikifanya juhudi za kudhibiti mlipuko huo.

Taarifa hiyo imetolewa wakati wa ziara ya Mbunge wa jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), alipokuwa akitembelea kituo hicho cha afya ili kujionea hali halisi na kuchukua hatua stahiki. Katika ziara hiyo, Mbunge Mpina amekabidhi vifaa tiba mbalimbali kwa kituo hicho, kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na mlipuko huo.

Akizungumza na watumishi wa kituo cha afya pamoja na wananchi, Mbunge Mpina amesisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari kali ili kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo. “Niwahimize wananchi kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huu kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya. Pia, Serikali itaendelea kutoa msaada unaohitajika kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu kwa wakati,” alisema Mpina.

Vifaa tiba vilivyotolewa na Mbunge Mpina vitasaidia katika kuhakikisha kuwa vituo vya afya jimboni humo vinakuwa na uwezo wa kuwahudumia waathirika wa Kipindupindu kwa ufanisi zaidi. Aidha, Mbunge huyo ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kudhibiti kabisa mlipuko huo katika jimbo la Kisesa.

Wakazi wa jimbo hilo wameombwa kushirikiana na mamlaka za afya kwa kufuata ushauri unaotolewa, ili kudhibiti ugonjwa huo ambao umeleta changamoto kubwa kwa huduma za afya katika wilaya ya Meatu.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts