KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani matukio ya ukatili na mauaji yaliyotekelezwa na Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Busega, mkoani Simiyu na kusisitiza kuwa huo ni ukiukwaji haki ya kuishi iliyowekwa katika Ibara ya 14 ya Katiba na haki ya uhuru iliyowekwa katika Ibara ya 15 ya Katiba hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hatua hiyo imekuja baada ya tarehe 21 Agosti mwaka huu, Jeshi la Polisi kudaiwa kumuua kwa kumpiga risasi mtu mmoja, kujeruhi watatu kwa risasi na kukamata watu 108 kutokana na vurugu zilizosababishwa na hasira za wananchi waliolituhumu jeshi hilo kushindwa kuchukua hatua dhidi ya matukio ya watoto kupotea.
Inaelezwa kuwa wanawake nane walioenda katika kituo cha polisi cha Lamadi kutafuta taarifa kuhusu watoto wao waliopotea, walidhalilishwa, kubezwa jambo lililoibua hasira miongoni mwa wananchi wa karibu walioamua kufunga barabara kuu na kurusha mawe kwenye kituo hicho.
Katika taarifa aliyoitoa kwa waandishi wa habari leo Ijumaa, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga amesema matukio hayo yanatishia utulivu wa kitaifa na kudhoofisha imani ya umma kwa vyombo vya utekelezaji sheria.
Amesema LHRC inatoa wito kwa mamlaka husika kupunguza matumizi ya nguvu kupita kiasi kwani vyombo vya sheria vinapaswa kuchukua hatua za kuzuia mivutano kwa amani, badala ya kutumia nguvu kupita kiasi.
“Pili tunatoa wito kuhimiza uwajibikaji na uwazi, kurejesha imani ya umma kupitia utamaduni wa mazungumzo lakini pia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina.
“Uchunguzi wa kina unahitajika kuhusu matukio ya kupotea kwa watoto, na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika,” amesema.
Amesema LHRC itaendelea kufuatilia kwa karibu tukio hili, kutetea haki, na kuhakikisha uwajibikaji na ulinzi wa haki za binadamu kwa raia wote.