Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka na wazi kuhusu matukio yaliyotokea, Wilaya ya Busega mkoani Simiyu kikidai uwajibikaji kutoka kwa waliohusika.
Kituo hicho pia kimehimiza vyombo vya usalama kuheshimu haki za binadamu na kurejesha imani ndani ya jamii, ambayo imeporomoka kutokana na matukio ya hivi karibuni.
Wito huo umekuja baada ya Jeshi la Polisi kusababisha kifo cha mtu mmoja, majeruhi na kukamatwa kwa wananchi 108 wakati wa maandamano ya kutaka kufahamu hatima ya kupotea kwa watoto wilayani humo.
Kufanyika kwa maandamano kulisababisha shughuli za kijamii na kiuchumi eneo la Lamadi kusimama hivyo Jeshi la Polisi iliwalazimu kutumia mabomu kutawanya waandamanaji.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga leo Agosti 23, 2024 imeeleza wasiwasi mkubwa juu ya kushindwa kwa polisi kushughulikia suala muhimu la kupotea kwa watoto, ambalo lilikuwa chanzo cha awali cha mgogoro.
“Tukio hili linaonesha mfululizo wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika eneo hilo pia majibu ya nguvu kwa wananchi waliokuwa wakitafuta haki yaliongeza hali ya kutokuelewana kati yao na polisi,” amesema Henga.
Henga amesema vyombo vya usalama kutotumia nguvu wanaposhughulika na raia na kipaumbele kiwekwe kwenye kupunguza mivutano.
Amesema mamlaka zinapaswa kuhakikisha kuwa raia wanapata taarifa, hasa katika masuala yenye umuhimu mkubwa kwa umma na wachukue wajibu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.