Mahakama yazuia tangazo la Serikali kufuta vijiji Ngorongoro

Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imezuia tamko la Serikali namba  673 la Agosti 2, 2024 la kufuta kata, vijiji na vitongoji, vikiwamo vya wilayani Ngorongoro hadi amri ya Mahakama itakavyoelekeza vinginevyo.

Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Agosti 22, 2024 na Jaji Ayoub Mwenda, aliyesikiliza maombi madogo ya zuio hilo yaliyowasilishwa na mmoja wa wananchi wa Ngorongoro, Isaya Ole Pose kupitia wakili Peter Njau.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Mwenda aliridhia maombi hayo madogo na kukubali zuio la kusimamisha tamko hilo kupisha usikilizaji wa maombi ya msingi.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha, wakili Peter amesema katika maombi hayo madogo namba 6953 ya mwaka 2024, wameyawasilisha mahakamani leo, kusikilizwa na kutolewa uamuzi huo.

Amesema maombi hayo madogo yalikuwa na hoja mbili, ya kwanza ni kuomba zuio hilo na ya pili ambayo ni kuu katika shauri hilo ni kuiomba Mahakama itoe kibali cha mleta maombi  kufungua maombi ya marejeo ya amri hiyo kama ilikuwa halali au si halali.

“Jaji ameridhia maombi yetu na ametuamuru tuwape nakala za maombi yetu upande wa Jamhuri (mjibu maombi) kwa hiyo amri ile ya tangazo la Serikali itasimama, ili kupisha maombi mama kama amri ile ilikuwa halali au la.

“Mteja wangu na wengine ambao ni wakazi wa Ngorongoro wanahisi aliyetoa amri ile hakuwa na mamlaka stahiki kuweza kutoa amri na haikutolewa kihalali, hivyo kwenye maombi ya msingi Mahakama itatazama hilo,” amesema.

Jaji Mwenda ameahirisha shauri hilo hadi Septemba 26, 2024 Mahakama itakaposikiliza maombi ya msingi ya Ole Pose.

Agosti 2, 2024 lilitolewa tangazo la Serikali chini ya kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya, ilitoa tamko la kufuta vijiji, kata na vitongoji kutoka wilaya za Ngorongoro, Bahi, Chemba, Kasulu, Kakonko, Hai na Rombo.

Related Posts