Dar/Dodoma. Wakati wadau wakilalamikia matukio ya utekaji na watu kupotea, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeshauri iundwe tume ya Rais ya majaji itakayofanya uchunguzi wa kina utakaowezesha kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wanaohusika.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Rais Samia Suluhu Hassan ndiye mwenye mamlaka ya kuunda tume hiyo chini ya Sheria ya Uchunguzi Mahususi.
Chadema ni taasisi ya pili kupendekeza kuundwa kwa tume ya namna hiyo, baada ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kufanya hivyo Agosti 9, 2024.
Mbowe ametoa pendekezo hilo akirejea ripoti ya TLS iliyotaja orodha ya watu 83 wanaodaiwa kutekwa na hadi sasa hawajulikani walipo.
Wakati kukiwa na mashinikizo hayo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa nyakati tofauti, imetangaza kufanya uchunguzi maalumu wa baadhi ya matukio katika mikoa 15, ikiwemo Dar es Salaam na Arusha, yaliyotokea kati ya mwaka 2020 hadi 2024, ili kubaini chanzo na wahusika wake.
Mbowe amesema hayo Agosti 22, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Katika uchunguzi huo, amesema tume hiyo itapaswa kuzisikiliza familia za waathirika wa matukio hayo na kwamba anaamini tume hiyo itafanya kazi kwa haki, ukweli na uhuru.
Ili kuweka msisitizo, Mbowe amemtaka Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuwasilisha waraka mahususi kwa Rais Samia.
“Kama wasaidizi wake hawatampatia waraka wetu kuhusu mambo haya ya utekaji, basi tutamfikishia barua hiyo moja kwa moja,” amesema.
Katika ufafanuzi wake kuhusu matukio hayo, Mbowe ameeleza kushangazwa na kuendelea kwa vitendo hivyo bila vyombo vya dola kuingilia kati au kuvitolea kauli.
Badala yake, amesema mamlaka mbalimbali zinaishia kuwabeza waathirika wa vitendo hivyo, jambo alilosema limesababisha chama hicho kiibuke kulizungumza.
“Inapotokea taarifa ya watu 80 kwenye mazingira yasiyoeleweka alafu vyombo vya dola vikakaa kimya na wengine wakaendelea kubeza, tumelazimika kuungana na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kupaza sauti,” amesema.
Kwa mujibu wa Mbowe, anatambua athari za kukemea vitendo hivyo hadharani, lakini ameamua kuzungumza ili hatua za kuvikomesha zichukuliwe.
Katika kile alichokiita uchunguzi uliofanywa ndani ya chama hicho, Mbowe amesema wamebaini asilimia 60 ya matukio ya kutekwa na kuuawa kwa watu yametokea katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Mbowe ameeleza uchunguzi wao umebaini kuwepo kikosi kazi ndani ya Jeshi la Polisi kilichohusisha askari wa jeshi hilo na vyombo vingine kwa ajili ya kudhibiti uhalifu, akidai baadaye kilibadilisha majukumu na kuwa kikosi cha kuteka wananchi.
Licha ya juhudi zilizofanyika, si Msemaji Mkuu wa Serikali wala viongozi wa Jeshi la Polisi waliopatikana kuzungumzia suala hilo.
Kwa nyakati tofauti, Mwananchi imemtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni lakini simu yake iliita bila majibu. Na hata alipotumiwa ujumbe kwa njia ya WhatsApp hakuusoma.
Hali ilikuwa hivyo pia kwa Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime ambaye awali amesema kupitia ya simu yake kuwa “nitakujibu”, lakini alipotafutwa baadaye simu hakupatikana hadi tunakwenda mitamboni.
Kadhalika, simu ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura hakupatikana hewani, huku Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai akitaka atafutwe Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kwa ufafanuzi zaidi.
Simu ya Muliro alipotafutwa kuzungumzia hilo iliita bila majibu.
Katika maelezo yake, Mbowe amegusia matukio ya watu watatu wakiwamo viongozi wao wawili wa chama hicho wilayani Temeke, Dar es Salaam wanaodaiwa kukamatwa na Polisi mapema wiki hii na hadi sasa hawajulikani walipo.
Kwa mujibu wa Mbowe viongozi hao waliokamatwa Buza Wilaya ya Temeke Agosti 18, 2024, ni Katibu wa Jimbo la Temeke, Jacob Mlay, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), wilayani humo, Deusdedith Soka na dereva wa bodaboda, Frank Mbisa.
Hata hivyo, Agosti 20, 2024, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Foka Dinya alipoulizwa na Mwananchi kuhusu vijana hao, alisema jeshi hilo halina taarifa kuhusu madai hayo, akisisitiza “kama Chadema wanalitaja jeshi la polisi watakuwa wanajua waliko”.
Mkutano wa Mbowe ulihudhuriwa pia na ndugu na jamaa wa vijana hao na wamepata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari, huku wengine wakishindwa kutokana na kububujika machozi.
Katika hatua nyingine, Mbowe amemtaka Rais Samia kuondoa utaratibu wa uanzishaji wa vikosi kazi ndani ya vyombo vya dola.
Amefafanua kuwa uwepo wa vikosi kazi hivyo unasababisha utekelezwaji wa majukumu kinyume na matakwa ya sheria, badala yake vinafanya kazi kwa kufuata utashi wa mtu.
Sambamba na hilo, amependekeza kufanyika mabadiliko ya Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 2023, kuondoa kifungu kinachowapa maofisa usalama mamlaka ya kumkamata mtu pale zinapomuona anaweza kuhatarisha amani ya nchi.
Mamlaka hiyo, Mbowe amesema ndiyo yanayovunja utaratibu wa ukamataji watu kwa sababu usalama wa taifa hawana mfumo rasmi wa ukamataji wala mahali pa kumpeleka aliyekamatwa.
Ametumia fursa hiyo kubainisha majina ya viongozi na kikosi kazi hicho jinsi kinavyofanya kazi pamoja na mawasiliano ya mwisho ya baadhi ya vijana hao kabla ya kutoweka.
Mbowe amesema mawasiliano hayo yakifuatiliwa wanaweza kubainika waliomteka kwa kuwa wao (Chadema) wanayo yote huku, akisema “wasitake kujua tumeyapataje, ni wao haohao huko ndani wametupa.”
Katika mazingira hayo, amewataka Watanzania wasiendelee kupiga magoti wakati wanamalizwa na kwamba wamkatalie yeyote anayekwenda kuwakamata bila kujitambulisha.
“Raia tufike mahali tukatae kukamatwa kama kuku. Kama wanataka kukamata mtu wamfuate, wajitambulishe kama PGO (Sheria za Polisi) inavyotaka,” alisema.
Akizungumza huku akitokwa machozi, Laifah Mbisa, mke wa Frank Mbisa mmoja wa vijana wanaodaiwa kutekwa, amesema kilio chake ni mumewe apatikane kwani zimeshapita siku kadhaa hajamwona.
Kinachomuumiza zaidi, ameeleza ni kutoweka kwa mumewe ilhali wana mtoto mdogo wanamlea na sasa amebaki mwenyewe bila msaada.
“Alinitumia ujumbe kwamba anaitwa wakachukue pikipiki polisi, tangu hapo sijaonana na mume wangu hadi leo,” amesema.
Jackline Massawe, Dada wa Jacob Mlay amesema tangu kaka yake ametoweka hakuonana naye hadi sasa, hivyo amewataka Watanzania wasimame kushinikiza kukoma kwa vitendo vya utekaji.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa THBUB, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu amezungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma akisema tume hiyo inaendelea na uchunguzi wake wa matukio hayo ya tangu mwaka 2020 hadi 2024.
Jaji Mwaimu ameitaja mikoa itakayofanyiwa uchunguzi ni Dar es Salaam, Singida, Mara, Shinyanga, Mwanza, Kagera, Geita, Kugoma, Tanga, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Arusha, Ruvuma na Rukwa.
Matukio watakayoyafanyia kazi, amesema ni ya watu waliopotea na kuripotiwa kwenye vyombo vya habari pamoja na taasisi nyingine.
Amesema tayari tume hiyo imekwishachukua hatua kadhaa kwa ajili ya uchunguzi wa matukio hayo, ikiwemo utambuzi wa matukio hayo kulingana na vyanzo mbalimbali vya taarifa, uchambuzi kwa maana ya sehemu yalikotokea na watu wanaodaiwa kuhusika.
“Idadi ya matukio ya watu kupotea inatofautiana kutokana na mikoa, kuna mikoa ina idadi kubwa ya matukio na mingine ina idadi ndogo, kwa hiyo tutakwenda kwenye maeneo 30 kwa ajili ya kuchunguza matukio hayo kwa muda wa wiki mbili hadi tatu, na tutakuja na taarifa ya tulichokibaini huko,” amesema.
Kuhusu matukio ya Shinyanga na Simiyu yaliyosababisha wananchi kuandamana baada ya kupotea kwa watoto, Jaji Mwaimu amesema uchunguzi utafanyika na watapendekeza hatua mahususi kwa taasisi husika.
“Kwa hiyo wananchi waliona ya kwamba hakuna hatua zozote zinazochukuliwa, lakini tume inaamini kwa kushirikiana na vyombo vingine vinavyohusika ni mambo yanayoweza kushughulikiwa na kupata ufumbuzi,” amesema.