Meshack aliyeuawa Simiyu azikwa, LHRC yataka uchunguzi

Dar es Salaam. Wakati kijana Meshack Paka (20) akizikwa kijijini kwao, Lutubika, Busega mkoani Simiyu, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka na wazi kuhusu vurugu hizo. baada ya kuuawa akidaiwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano yaliyofanyika wilayani humo,

Meshaki aliuawa kwa risasi katika maandamano ya wananchi yaliyofanyika Agosti 21, 2024 katika mji wa Lamadi wilayani Busega kulalamikia kitendo cha Jeshi la Polisi kutowapa ushirikiano kwenye madai ya watoto kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Katika maandamano hayo, wananchi walifunga barabara na kushambulia magari wakitaka maelezo kuhusu watoto wanaodaiwa kupotea na kutekwa katika mji huo.

Hata hivyo, maandamano hayo yalidhibitiwa na polisi kwa mabomu ya machozi na risasi, ambapo kijana, Meshack Paka (20) alifariki dunia akidaiwa kupigwa risasi na polisi.

Mbali na kijana huyo kufariki, Jeshi la Polisi liliwakamata wananchi 108 na wengine kadhaa walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo.

Vilio na simanzi leo vimetawala kwa wananchi katika mji Lamadi walipokuwa wakiaga mwili wa Meshack, katika Kanisa la Waadventista Wasabato mjini hapa.

Baada ya kutoka kanisani, waombolezaji waliupeleka mwili wa Meshack nyumbani kwao katika Lijiji cha Lutubiga huku wadau wakitoa wito mauaji kama hayo yadhibitiwe.

Akihubiri katika ibada hiyo ya mazishi, Mchungaji Mussa Itinde wa Kanisa la Wasabato Shimaliwa mjini Mwanza, amesema kuwa maisha ya mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke ni mafupi sana na yenye kujaa taabu, hivyo kwa miaka 20 aliyoishi Mashack naye amepitia mikasa mingi kabla ya mauti yake.

Amesema licha ya kuwa kifo hakiepukiki, lakini ni lazima tuhakikishe vifo kama hivi havitokei katika jamii, kwani kwa tukio hili linaumiza na Mungu wetu ameshinda, hivyo ni vizuri kumshukuru Mungu kwa kila jambo.

Mbunge wa Jimbo la Busega, Simon Songe ameeleza kuhuzunishwa na kifo hicho na kuahaidi kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali ili kuhakikisha ya kuwa matukio kama hayo hayajirudii.

Amesema endapo kutatokea na changamoto kama hizo ni vizuri kukaa na kuzungumza ya kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo.

Mkuu wa wilaya ya Busega, Faidha Salim akitoa salamu za Serikali amesema wakati anatoa taarifa ya tukio la vurugu hizo kwa waandishi wa habari alikuwa hajapata taarifa ya kifo cha kijana huyo na baada ya kupata taarifa hizo akiwa kama mzazi amehuzunishwa.

Amesema Serikali ipo kazini kuhakikisha tukio kama hilo halitokei tena, hivyo anawaomba wananchi wa wilaya hiyo na mji wa Lamadi kila mmoja atunze amani ya nchi yetu.

“Ndugu zangu wana Busega mimi ni mwananchi mwenzenu, naomba tushirikiane zinapotokea changamoto zozote ni vizuri tukaa na viongozi wa eneo husika na tukamaliza hizo changamoto, kuliko hatua zilizochukuliwa za kufanya maandamano na matokeo yake ni kama haya yamesababisha kifo kwa kijana wetu,” amesema.

Akisoma historia ya marehemu, Thomas Ezekiel amesema, Meshack alizaliwa Desemba 18, 2004 katika Kijiji cha Busega ni mtoto wa pili wa familia ya Daud Paka na alipata elimu ya msingi na kuhitimu mwaka 2017 katika Shule ya Msingi Mwabasabina mwaka 2021.

Kijana huyo alihitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Anthony Mtaka iliyoko Busega na baadaye alijiunga na masomo ya kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Loliondo mkoani Arusha na kuhitimu mwaka 2024 ambapo alipata daraja la kwanza kwa alama 7 na alikuwa ameomba kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika fani ya Sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 22, 2024 katika Mji wa Lamadi, RC Kihongosi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi alisema Kamati ya Usalama ya mkoa ilikutana na familia marehemu na imewaeleza kuwa na Serikali itabeba gharama za mazishi pamoja na za wengine waliojeruhiwa.

“Tunaliachia Jeshi la Polisi kusimamia sheria kama inavyotaka ili waliohusika na uhalifu na uvunjifu wa amani wachukuliwe hatua,” alisema.

Akieleza sababu ya nguvu kubwa kutumika kuzima maandamano hayo, Kihongozi alisema licha ya polisi kudhibiti vurugu hizo, “wananchi waliendelea kuchoma matairi ili waweze kuchoma kituo cha polisi”, jambo ambalo liliwalazimu askari wa jeshi la polisi kutumia mabomu ya machozi.

“Baada ya mambo yale Jeshi la Polisi likawajeruhi wananchi wanne na ilipofika saa mbili usiku, tukapata taarifa kuna mwananchi mmoja amefariki, na tukathibitisha ni kweli,” aliongeza Kihongosi.

Aliwataka wananchi kushirikiana na Serikali iwapo kuna jambo halijakaa sawa, badala ya kujichukulia sheria mkononi na kusababisha madhara.

“Wananchi walikaidi kusikiliza kauli za viongozi wakaanza kurusha mawe na ilipofika kamati ya usalama ya mkoa utulivu ukawa haupo na mpaka sasa tuna wajumbe wawili wa kamati ya waliojeruhiwa kwa mawe, mmoja ameshonwa nyuzi tatu na mwingine nyuzi nne, wanaendelea vizuri na matibabu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Kihongosi ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa huo kuimarisha intelijensia ili kupata taarifa kwa usahihi ili kuepuka viashiria vya uvunjifu wa amani.

“Nimetoa maelekezo kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuwa tayari wakati wote na kuimarisha intelijensia kupata taarifa kwa usahihi na kuhakikisha tunawasiliana na wanachi kujua nini viashiria vya uvunjifu wa amani,” alisema.

Kihongosi alisema jambo lingine alilolisistiza kwenye kikao hicho ni wazazi na walezi kutimiza wajibu wa kila mmoja kulinda familia yake na watoto wa mwenzake.

“Wanapoona kuna uvunjifu wa amani ama kuna watu hawawatambui, waweze kutoa taarifa ndani ya Jeshi la Polisi waweze kuchukua hatua.

“Lakini pamoja na hayo tumeweza kubaini kuwa mji wa Lamadi unakua sana na kuna mwingiliano mwingi wa watu ambao wanatoka maeneo mbalimbali kama Bunda (Mara), wapo wanaotoka Kenya wanaingia humu kufanya shughuli.

“Tumeagiza Udara ya Uhamiaji kuhakikisha kila raia mgeni anayeingia hapa awe na vibali,” amesema Kihongosi.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Anna Henga leo Agosti 23, 2024 imevitaka vyombo vya usalama kuheshimu haki za binadamu na kurejesha imani ndani ya jamii, ambayo imeporomoka kutokana na matukio ya hivi karibuni.

Ameeleza wasiwasi mkubwa juu ya kushindwa kwa polisi kushughulikia suala muhimu la kupotea kwa watoto, ambalo lilikuwa chanzo cha awali cha mgogoro.

“Tukio hili linaonyesha mfululizo wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika eneo hilo pia majibu ya nguvu kwa wananchi waliokuwa wakitafuta haki yaliongeza hali ya kutokuelewana kati yao na polisi,” amesema Henga.

Pia amevitaka vyombo vya usalama kutotumia nguvu kubwa wanaposhughulika na raia na kipaumbele kiwekwe kwenye kupunguza mivutano.

Amesema mamlaka zinapaswa kuhakikisha kuwa raia wanapata taarifa, hasa katika masuala yenye umuhimu mkubwa kwa umma na wachukue wajibu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.

“Jeshi la polisi linapaswa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio ya watoto waliopotea na kuhakikisha kuwa wote waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria haraka.

“Utamaduni wa mazungumzo unapaswa kuzingatiwa sana katika jamii zetu kati ya mamlaka na raia. Hii itarejesha uwazi na uwajibikaji na hatimaye kutatua malalamiko yanayoibuka kwa amani badala ya kutumia maofisa wa utekelezaji wa sheria,” amesema Henga.

Related Posts