Mpole hatihati kuivaa Dodoma Jiji

KESHO Pamba Jiji itarusha karata yake ya pili Ligi Kuu itakapoikabili Dodoma Jiji katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, huku shauku ya mashabiki wa timu hiyo kumuona mshambuliaji wao, George Mpole ikiwa njiapanda kutokana na leseni yake kutokamilika.

Mchezo huo wa raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara utachezwa kuanzia saa 10:00 jioni, timu hizo hazikuanza vyema mechi zao za kwanza, Pamba Jiji ikilazimishwa suluhu na Tanzania Prisons huku Dodoma Jiji ikichapwa bao 1-0 na Mashujaa FC.

Akizungumzia sakata la wachezaji wake wa kimataifa kukosa leseni za kucheza Ligi Kuu, Afisa Habari wa Pamba Jiji, Martin Sawema alisema uongozi umeshakamilisha taratibu za wachezaji hao kupata leseni huku leseni ya uhamisho wa kimataifa (ITC) ya George Mpole kutoka klabu ya St. Eloi Lupopo ya DR Kongo ukiwa haujakamilisha.

“Leseni za wachezaji wetu wote zimeshakamilika imebaki leseni ya Mpole ambayo iko mwishoni kwahiyo kufikia Jumamosi wote watakuwa tayari isipokuwa Mpole, hata kipindi kile tulikuwa tumeshalipia ilikuwa tu imebaki kusomeka kwenye mfumo jambo ambalo tumelikamilisha,” alisema Sawema na kuongeza;

“Kimsingi tunazihitaji pointi tatu katika mchezo wa Jumamosi tukiwa na faida ya kutumia uwanja wa nyumbani na mashabiki wetu ni watu wa muhimu kuchangiza ushindi tunawahitaji wajitokeze kwa wingi, mpaka sasa hatuna majeruhi wala changamoto inayoweza kutuzuia kupata ushindi.”

Kocha wa timu hiyo, Goran Kopunovic alisema: “Nina matumaini mechi ijayo nitawatumia wachezaji wangu wote na tutakuwa tayari kuonyesha ubora wetu, mchezo uliopita tulicheza vizuri hii ni Ligi Kuu kila timu ni bora lazima tuwe ngangari tupambane.”

Beki wa Dodoma Jiji, Dickson Mhilu alisema mchezo uliopita walipoteza kwa kukosa maelewano kutokana na ugeni wa wachezaji jambo ambalo limefanyiwa kazi mazoezini, hivyo mechi ya kesho lazima wapambane kupata pointi tatu.

Ofisa Habari wa Dodoma Jiji, Patrick Semindu alisema; “Tunahitaji ushindi kwa hali na mali kurudisha imani kwa mashabiki wetu usajili tuliofanya tunastahili matokeo mazuri. Kikosi kiko vizuri hakuna majeruhi tumefika Mwanza Jumatatu na tunajifua uwanja wa Butimba na ligi tutaanza Jumamosi kwa kishindo.”

Related Posts