Dodoma. ‘Utajiri namba moja ni afya’ ndivyo anavyosema Fulko Mlowe mkazi wa Kijiji cha Mundindi kilichopo wilayani Ludewa, Mkoa wa Njombe ambacho wakazi wake wote wamekatiwa bima ya afya na serikali ya kijiji.
Mundindi ni kijiji chenye jumla ya wakazi 3,196, lakini ambao walikuwa hawana bima ya afya ni wakazi 2,586 na wote hao sasa wana bima ya CHF iliyokatwa kwa zaidi ya Sh12.9 milioni.
Kwa mujibu wa Mlowe ‘fedha na mtindo wa maisha vinafuata baada ya kuwa na uhakika wa afya’.
Serikali ya Kijiji cha Mundindi imekuwa mfano wa kipekee kwa kutumia mapato ya kijiji kuwanufaisha wakazi wote. Mundindi ni kati ya vijiji 12,318 vilivyopo nchini.
Kijiji cha Mundindi kiliweka banda la maonyesho wakati wa uzinduzi wa kanuni za uchaguzi uliofanywa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ambaye pia alitangaza uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika Jumatano ya Novemba 27, 2024.
Umuhimu wa kuchagua viongozi bora
Serikali ya Kijiji cha Mundindi imekuwa kilelezo kizuri kwa wananchi kuchagua viongozi bora wanaojali maendeleo ya wananchi wao.
Viongozi wenye dhamira ya kweli ya kuhudumia wananchi huweka mbele masilahi ya umma badala ya masilahi yao binafsi.
Hii inahakikisha kwamba rasilimali za umma zinatumika kwa njia sahihi na yenye manufaa kwa wote, kama vile kuboresha huduma za afya, elimu, na miundombinu.
Viongozi wanaojali masilahi ya wananchi pia wanahamasisha uwajibikaji na uwazi katika utendaji wao wa kazi, na hivyo kujenga imani kati yao na wananchi.
Wanawahusisha wananchi katika maamuzi muhimu na kuwa sikivu kwa mahitaji yao. Hii inasaidia kutatua changamoto kwa haraka na kwa ufanisi, na kufanya jamii kusonga mbele kwa amani na umoja.
Aidha, kuchagua viongozi wenye kujali masilahi ya wananchi huimarisha demokrasia na utawala bora, kwa kuwa viongozi hawa wanazingatia sheria na kanuni, na wanawaheshimu wananchi kama sehemu muhimu ya maendeleo ya Taifa.
Kwa hiyo, ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha anachagua viongozi bora ambao watawezesha kufikia maendeleo endelevu na ustawi wa jamii nzima.
Mtendaji wa Serikali ya Kijiji cha Mundindi Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, Adrat Msigwa anasema waliingia mkataba wa miaka mitano kwa kununua hatifungani ya kijani ya Benki ya CRDB kwa gharama ya Sh400 milioni.
Anasema kijiji hicho chenye idadi ya watu 3,196 waliokuwa hawana bima ya afya ni 2,586 ambapo waliwakatia kwa Sh12.9 milioni kwa mwaka na kuwezesha wakazi wote kupata tiba bila kulazimika kutoa fedha zao mfukoni.
Msigwa anasema fedha walizotumia kukata bima ya afya kwa kaya zote 431 zilitokana na gawiwo walilopata kutoka kwenye hatifungani ya kijani.
“Hatifungani ya kijani tulinunua mwaka jana na faida ya kwanza tulipata Machi mwaka huu Sh20.5 milioni. Hii ni faida ya miezi sita ni nusu ya gawiwo la Sh41 milioni tunayotakiwa kupata kwa mwaka,” anasema Msigwa.
Anasema mkataba wa hatifungani ya kijani ni miaka mitano, lakini hata ukiisha wana mipango mingine kama misitu na kilimo cha parachichi.
Msigwa anasema mapato ya serikali ya kijiji pia yameweza kufutwa kwa michango ya maendeleo ya kila mwaka toka kwa wananchi.
Felisia Msamba ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mundindi na ni mama wa watoto watatu, anasema bima ya afya inatokana na faida walioipata na wakaamua kila mwananchi anufaike kwa kukatiwa bima ya afya.
“Tulikaa kikao mipango na fedha, tukaenda kwenye kikao cha kijiji na baadaye kwenye mkutano wa kijiji uliojumisha wananchi wote tukaamua ili fedha imguse kila mwananchi ni vema tuwakatie bima ya afya,” anasema.
Kwa upande wake, Fulko Mlowe ambaye naye ni mkazi wa Kijiji cha Mundindi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulipa fidia wanakijiji kutokana na Serikali kuchukua eneo lililokuwa limepandwa miti ya mbao ambapo mradi wa chuma wa Liganga umechukua eneo hilo.
“Fidia ya mradi wa Liganga na Mchuchuma iliyolipwa na Serikali ni Sh15.6 bilioni. Sisi kijiji kilikuwa na eneo tulipanda miti ya mbao tukalipwa Sh464 milioni kama kijiji.
“Serikali ya kijiji ikakaa na wananchi tukaona Sh64 milioni tuzitumie kuboresha taasisi kama shule na maji. Shule tumejenga vyoo na maji tumeweka matenki na kununua mabomba nab ado fedha zipo. Sh400 milioni tukaona tukanunue hatifungani na tulinunua Agosti mwaka jana,” anasema Mlowe.
Mlowe anasema gawio la kwanza walipata Machi 23, 2024 la Sh20.5 milioni. “Ilikuwa ni suala la uwazi na Serikali ya Kijiji ikatoa wazo la kulipa bima kwa wakazi wote.”
Anasema mbali na bima ya afya, kijiji kina mipango mingine ya kilimo cha parachichi ambapo kila mkazi atapewa miche 20 aanzishe kilimo kwa ajili ya kuongeza kipato na lish bora.
Pia, anasema mipango mingine ya kijiji ni kusaidia vijana waliomaliza kidato cha nne na kushindwa kuendelea na masomo ya juu ambapo Serikali ya Kijiji itawapeleka VETA wakijifunze ujuzi utakaonufaisha kijiji na vijana wenzao kwa kupata ajira.
“Tutawapeleka VETA wakape ujuzi kwa mfano ufugaji bora wa kuku ili wakirudi waanzishe vikundi vya ufugaji vitakavyonufaisha vijana wenzao na wanakijiji wengine,” anasema.
Mwanakijiji mwingine Steven Mwageni amemshukuru Rais Samia kwa kulipa fidia ambao kwa miaka mingi ilikuwa ikizungumzwa tu, na ndio imesaidia wao kupata fedha za kulipia bima ya afya na maendeleo mengine.
Anasema kwa sasa kila mwananchi akijihisi kuumwa anakwenda hospitali haraka, tofauti na zamani ambapo mtu akiumwa anakaa tu ndani hadi ndugu waje kumchangia fedha za gharama za matibabu.
“Sasa hivi mtu akiumwa anakwenda haraka hospitali kutibiwa na baada ya hapo anaendelea na shughuli zingine za kiuchumi bila kupoteza muda,” anasema Mwageni.
Moja ya faida kubwa ya bima ya afya ni uwezo wake wa kuzuia umasikini unaotokana na gharama za matibabu. Gharama hizi zinaweza kusababisha familia kuingia katika umasikini wa ghafla kutokana na kulazimika kuuza mali zao au kutumia akiba yao yote kugharamia matibabu.
Kwa kuwa na bima ya afya, wananchi wanakuwa na uhakika wa kupata matibabu bila ya kujitwika mzigo mkubwa wa kifedha, hivyo kuzuia kuanguka katika umaskini.
Pia, bima ya afya inaongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za msingi na za rufaa bila kikwazo cha kifedha.
Upatikanaji mzuri wa huduma za afya unachangia pia kuboresha afya ya jumla ya jamii, na kufanya wananchi kuwa na uwezo zaidi wa kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Bima ya afya hutoa usalama wa kiafya kwa wananchi kwa kuhakikisha kuwa wanapata huduma za afya wanazohitaji bila kujali uwezo wao wa kifedha.
Kwa kuwa na uhakika wa kupata matibabu, wananchi wanakuwa na amani ya akili na wanaweza kujikita katika shughuli nyingine za kiuchumi bila hofu ya gharama za matibabu.
Usalama huu wa kiafya pia unachangia kuimarisha mshikamano wa kijamii na kupunguza pengo kati ya matajiri na maskini katika upatikanaji wa huduma za afya. Afya bora ni msingi wa uzalishaji na ufanisi katika kazi.
Wananchi wenye afya njema wanaweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali kama kilimo, viwanda, na huduma.