KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujifua kwa ajili ya mechi ya marudiano ya raundi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O ya Burundi, iliyohamishwa kutoka Kwa Mkapa hadi Azam Complex, huku kocha wa zamani wa timu hiyo, Nasreddine Nabi akiitabiria msimu huu kufika nusu fainali ya michuano hiyo.
Nabi anayeinoa Kaizer Chiefs ya Afrika alikuwapo nchini kwa siku mbili kuonana na mabosi wa Yanga na katika kikao chao, aliwaambia kwa kikosi walichonacho, haoni wa kuizuia msimu huu isifike hatua hiyo baada ya msimu uliopita kutinga makundi na kuishia robo fainali ikiwa ni miaka 25 tangu ilipofanya hivyo 1998.
Kocha huyo alifanya kikao na mfadhili wa Yanga, Gharib Mohammed ‘GSM’, Rais Injinia Hersi Said pamoja na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini, Anthony Mavunde, kisha akawaambia kama ni timu basi msimu huu wanayo.
Kocha huyo raia wa Tunisia alisema, kikosi ilichonacho Yanga ni kizito ambacho sio tu kutinga makundi, lakini kama ikivuka hapo basi itakwenda robo fainali hata nusu fainali itategemea na mpinzani gani watakutana naye.
“Nimekutana na viongozi wa Yanga tumekuwa na vikao vizuri vya kifamilia, nilifanya kazi hapa, bado nina maelewano mazuri na viongozi lakini pia wachezaji hata mashabiki na wanachama,” alisema Nabi na kuongeza:
“Nimefurahia kuona kila ninapopita bado watu wanakumbuka kuhusu Nabi, watu wa Yanga, Simba na hata timu nyingine, nimewaambia viongozi kuwa wana timu nzuri sana msimu huu, sitashangaa kama watavuka mbali zaidi ya hatua ya makundi kwa kucheza robo fainali na hata nusu fainali.
“Nadhani ni timu chache zinaweza kuwa na kikosi kizito kama hiki cha Yanga, naamini watafanya vizuri sana hapa ndani na hata Afrika.”
Aidha, Nabi alisema mbali na kuwa na timu bora wakiwamo nyota wapya waliosajiliwa katika dirisha hili kama Clatous Chama, Prince Dube, Jean Baleke, Chadrack Boka, Duke Abuya na kipa Abubakar Khomeiny, pia kocha Miguel Gamondi mbinu zake zimeongeza ubora mkubwa wa timu hiyo aliyoinoa kwa misimu miwili.
“Sio tu kikosi lakini hata benchi la ufundi ni zuri, nimekutana nao, wana kocha bora sana ambaye falsafa zake zimeipa nguvu zaidi timu, hili nalo ni muhimu sana.”
Yanga tayari imeshaweka mguu mmoja ndani kutinga hatua ya mtoano kuwania kufuzu makundi baada ya kushinda ugenini kwa mabao 4-0 dhidi ya Vital’O ya Burundi.
Mashabiki wa Yanga wameiona timu yao katika mechi tatu zilizopita za kimashidano tangu kuanza kwa msimu huu wa 2024-2025 ambazo zote wameshinda wakianza na mbili za Ngao ya Jamii dhidi ya Simba (1-0) na Azam (4-1) ambapo walibeba taji hilo.
Baada ya hapo, safari yao ya kimataifa ikaanza kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Vital’O ya Burundi, mechi ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa kwanza, Wananchi walikuwa wageni kikanuni baada ya Vital’O kuuchagua Uwanja wa Azam Complex kwa mechi za nyumbani za michuano ya kimataifa na kesho zitarudiana hapohapo.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi anautazamia mchezo huo katika safari ya kuandika rekodi mpya kikosini hapo baada ya msimu uliopita kuifikisha hadi robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Gamondi aliiongoza timu hiyo kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupita miaka 25, kisha akaweka rekodi ya Yanga kucheza robo fainali kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo tangu michuano ilipobadilishwa mwaka 1997 kutoka Klabu Bingwa Afrika.
Kuna dakika 270 kwa Gamondi za kuhakikisha anaandika rekodi nyingine ya kuwa kocha wa kwanza wa Yanga kuipeleka timu hiyo makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa misimu miwili mfululizo.
Dakika hizo 270 ni sawa na mechi tatu zilizosalia, moja ya marudiano dhidi ya Vital’O, mbili ni za hatua ya kwanza nyumbani na ugenini dhidi ya mshindi kati ya CBE ya Ethiopia na SC Villa kutoka Uganda.
Rekodi zinaonyesha katika miaka 10 iliyopita kuanzia 2014 hadi sasa, Yanga imefundishwa na makocha tisa tofauti wa kigeni, lakini ni wawili tu walioipa heshima kubwa katika michuano ya CAF ikiwamo kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2022-2023 chini ya Nasreddine Nabi na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa 2023-2024 ikinolewa na Gamondi. Hata hivyo, awali ilitinga makundi ya Kombe la Shirikisho mara mbili 2016 na 2018 ikiwa na makocha wawili tofauti.
Makocha hao tisa ni Marcio Maximo (2014), Hans Pluijm (2015-16), George Lwandamina (2016-2018), Mwinyi Zahera (2018-2020), Luc Eymael (2020), Zlatko Krmpotic (2020), Cedric Kaze (2020-2021), Nasreddine Nabi (2021-2023) na sasa Gamondi aliyejiunga na timu hiyo Julai 2023.
Nabi baada ya kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho, hakuendelea kuifundisha timu hiyo, akaondoka ndiyo akaja Gamondi akaweka rekodi iliyosubiriwa kwa miaka 25.
Ukiangalia kikosi cha Yanga msimu huu kinaonekana kuwa bora zaidi ya kile kilichopita.
Ubora wa kikosi hicho umeonekana mapema tangu kipindi cha pre-season ilipoenda Afrika Kusini kucheza mechi dhidi ya FC Augsburg ya Ujerumani na kufungwa 2-1, kisha ikazifunga TS Galaxy (1-0) na Kaizer Chiefs (4-0) zote za huko. Baada ya hapo, ikawafunga mabingwa wa Kagame Cup, Red Arrows 2-1 katika kilele cha Wiki ya Wananchi na kisha ikachukua Ngao ya Jamii kwa kuzifunga Simba (1-0) na Azam (4-1), timu ambazo zimekuwa washindani wakubwa kwao kila msimu.
Kikosi hicho kimefanyiwa maboresho ya kusajiliwa wachezaji wapya saba Khomeini, Boka, Andabwile, Chama, Abuya, Jean Baleke na Prince Dube ambapo kati ya hao, cheche zao zimeanza kuonekana akiwamo Boka, Chama, Duke na Dube.
Hivi sasa Yanga katika kila nafasi, ina wachezaji wenye ubora mkubwa unaofanana au kuzidiana kidogo jambo linalomfanya Gamondi kuwa na wakati mzuri wa kupanga timu ya ushindi.
Msimu uliopita Yanga ilikuwa na matokeo mazuri zaidi nyumbani katika michuano ya kimataifa kuanzia hatua ya awali hadi robo fainali ambako ilishuka dimbani mara sita, ilishinda nne na sare mbili, haikupoteza.
Hatua ya awali na ile ya kwanza, Yanga kwenye uwanja wa nyumbani ilizifunga Djibouti Telecom (5-1) na Al Merrikh (1-0). Katika makundi mechi tatu ilizocheza ilishinda dhidi ya Medeama (3-0) na CR Belouizdad (4-0) huku ikitoka sare 1-1 dhidi ya Al Ahly. Robo fainali nyumbani ikatoka 0-0 dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Gamondi msimu uliopita katika mechi sita za ugenini, alishuhudia timu hiyo ikipata ushindi mara mbili pekee ndani ya dakika 90 dhidi ya Djibouti Telecom (0-2) na Al Merrikh (0-2) zote hatua za mwanzoni, huku ikipoteza kwa mabao 3-0 mbele ya CR Belouizdad na 1-0 dhidi ya Al Ahly, kisha sare ya 1-1 na Medeama na 0-0 robo fainali dhidi ya Mamelodi ambayo mwisho Yanga ikapoteza kwa penalti 3-2.