Rais TEC: Serikali irejee meza ya mazungumzo na wananchi Ngorongoro

Mbulu. Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Wolfgang Pisa ameiomba Serikali kurejea katika meza moja ya mazungumzo na wananchi wa Ngorongoro, akisema: “Iwasikilize, isiwalazimishe kuhama wala kuwakosesha huduma muhimu.”

Askofu Pisa amesema uhalali wa uongozi uliopo madarakani katika utawala bora,  unatoka kwa wananchi na viongozi hao wanawajibika kwa wananchi.

Ameyasema hayo leo Alhamisi Agosti 22, 2024 katika maadhimisho ya Misa ya Jubilei ya miaka 25 ya Upadri wa Askofu Antony Langwen wa Jimbo Katoliki Mbulu, Mkoa wa Manyara.

Katika maelezo yake, Pisa ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi, amesema uhalali wa uongozi uliopo madarakani katika dhamana ya utawala bora, unatokana na madaraka na rasilimali zinazomilikiwa na wananchi,  na kwamba viongozi ni wasimamizi wa rasilimali hizo.

“Yanayotokea Ngorongoro, tunaomba Serikali irudi katika meza ya mazungmzo, isiwalazimishe wala kuwakosesha huduma muhimu za jamii, au kuzuia chakula kuwafikia, pia wapewe haki yao ya kupiga kura mahali walipo.”

“Leo hii huwezi kueleza umma kuwa Wamasai wanahama kwa hiari yao, kesho yake tunaona Wamasai wamejaa barabarani, wakilia na kupaza sauti kuwa haki zao zimepokonywa,” amedai Askofu Pisa.

Hata hivyo, Jumapili Agosti 18, 2024, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kupitia taarifa kwa umma, ilisema hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu na shughuli za utalii katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro zinaendelea kama kawaida.

“Maandamano yaliyoripotiwa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii yanaidhihirishia dunia na jumuiya za kimataifa, vyombo vya habari na asasi za kimataifa, kwamba ndani ya hifadhi hiyo hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa wananchi,”ilisema taarifa hiyo.

Askofu Pisa ameongeza kusema:“Serikali ina wajibu wa kulinda haki, kuwajibika, uwazi na kuzuia hila zote za uvunjifu wa amani hasa tunapoelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.”

Related Posts