MABOSI wa Omonia Nicosia ya Cyprus wameripotiwa kuvalia njuga dili la kumnasa nahodha wa timu ya taifav ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye kwa sasa anaonekana kutokuwa katika mipango ya kocha wa PAOK ya Ugiriki, Razvan Lucescu.
Samatta bado ana mkataba wa kuichezea miamba hiyo ya soka la Ugiriki hadi Juni 30, 2025, awali alikuwa katika rada za Al Kholood iliyopanda Ligi Daraja la Pili Saudi Arabia ambako baadhi ya mastaa wa soka Ulaya wanakimbilia.
Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa, viongozi wa PAOK wameanza mazungumzo na Omonia Nicosia na inaelezwa vigogo hao wapo tayari kulipa mara mbili ya kile ambacho nahodha huyo wa Taifa Stars anavuna huko Ugiriki.
Mmoja wa marafiki wa karibu wa Samatta amethibitisha hilo akisema mshambuliaji huyo anaweza kuondoka muda wowote pamoja na kwamba msimu uliopita alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo akiwa na timu hiyo.
“Samatta anahitaji nafasi zaidi ya kucheza na bahati nzuri zipo timu ambazo zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili. Nadhani mwenyewe atakuwa na uamuzi wa mwisho kuwa wapi ataenda,” alisema rafiki huyo wa Samagoal.
“Kulingana na mazingira ninayoyaona sidhani kama atasalia (PAOK) kwa sababu ni kama hayupo kwenye mipango ya kocha Lucescu, amekuwa akimpa muda mchache na Samatta anajiona kuwa na uwezo wa kuendelea kuonyesha makali yake.”
Katika michezo minne iliyopita, Samatta hakuwa sehemu ya kikosi cha PAOK ambacho kimeshinda mechi mbili, kupoteza na kutoa sare mara moja moja katika mashindano matatu tofauti, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Agosti 6, mwaka huu, PAOK ilikuwa nyumbani kuikaribisha Malmo FF ya Sweden katika mchezo wa mchujo wa kuwania kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, iliotoka sare ya mabao 2-2 na ilipokwenda ugenini ikachapwa mabao 4-3 na kuangukia Europa League.
Kabla ya mchezo wa mchujo wa Europa ambao ilishinda kwa mabao 4-0 dhidi ya Shamrock Rovers, pia Samatta alikosekana katika mchezo wa kwanza wa ligi ambao chama hilo lilishinda kwa mabao 3-2 dhidi ya Panserraikos.
Mara ya mwisho kwa Samatta kuonekana uwanjani akiwa na jezi ya PAOK ilikuwa Julai 31 kwenye mchezo wa mchujo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borac Banja Luka ya Bosnia ambapo alicheza kwa dakika 19 na wa marudiano wa kwanza alipewa dakika 23. Kwa sasa haonekani kuwa na nafasi kwenye kikosi cha kwanza.