Arusha. Sasa wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) watatakiwa kusubiri kutumia sarafu moja, baada ya Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Veronika Nduva kusema mchakato wake umesogezwa hadi mwaka 2031.
Nchi wanachama wa EAC zilitia saini itifaki ya kuanzisha Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAMU) Novemba 2013.
EAMU iliweka msingi wa kuanzishwa kwa umoja wa fedha ndani ya miaka 10 na kuruhusu nchi wanachama wa EAC kuunganisha sarafu zao taratibu hadi kuwa sarafu moja ndani ya Jumuiya.
Akizungumza Agosti 21 2024, wakati wa mkutano uliowakutanisha viongozi wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) na watumishi wa EAC, Nduva amesema mchakato haujakamilika, hivyo umeahirishwa hadi mwaka 2031.
“Umoja wa Fedha ulitarajiwa kuanzishwa mwaka 2024 kulingana na mpango uliokuwepo. Hata hivyo, haukuweza kufikiwa na muda huo umebadilishwa hadi 2031,” amesema.
Mkutano wa EABC na EAC ulikuwa na mada ya, “Kukuza Biashara na Uwekezaji ndani ya EAC: Kufungua Vikwazo na Kutoa Fursa,” ulioandaliwa na EABC.
Nduva amesema hadi sasa baadhi ya vipengele vya mpango wa huo vimeanzishwa lakini wanachama wameendelea kutofautiana kuhusu vipengele vingine kadhaa.
Vipengele hivyo ni utengenezaji wa nyaraka za kisheria kwa ajili ya kuanzisha taasisi zitakazosaidia Umoja wa Fedha. Nyaraka hizo, alisema, zipo katika hatua mbalimbali za mchakato wa kupitishwa au kuanza kutumika.
Aidha, amebainisha kuwa benki kuu za EAC zimeanzisha Mfumo wa Malipo wa Afrika Mashariki (EAPS); jukwaa la sarafu tofauti linalowezesha malipo katika sarafu za ndani za nchi wanachama, hivyo kurahisisha ubadilishaji wa sarafu katika eneo hilo.
“Nchi wanachama zimetia saini na zinatekeleza Makubaliano ya Ubadilishanaji Sarafu na Urejeshaji Fedha. Nyaraka ya kisheria ya ulinganifu wa kodi ya bidhaa imetengenezwa na inafanyiwa uchunguzi na Baraza la Sekta ya Fedha na Masuala ya Kiuchumi. Mkataba wa Kuepuka Kodi Mara Mbili wa EAC umetengenezwa na unafanyiwa uchunguzi na Baraza,” amesema Nduva.
Hata hivyo, kumekuwa na ucheleweshaji wa kufikia makubaliano kuhusu nchi ipi itakuwa makao makuu ya Taasisi ya Fedha ya Afrika Mashariki (EAMI). EAMI ni hatua ya awali kuelekea Benki Kuu ya Afrika Mashariki.
Changamoto nyingine, amesema nchi wanachama hazijaweza kukubaliana juu ya vigezo vya kuunganisha kwa ufanisi misingi minne ya kiuchumi.
Hii ni pamoja na kiwango cha juu cha mfumuko wa bei cha asilimia nane, akiba ya fedha za kigeni inayofikia miezi 4.5 ya uagizaji bidhaa kutoka nje, ukomo wa nakisi ya jumla ya bajeti wa asilimia tatu ya Pato la Taifa (GDP), na ukomo wa deni la umma uliowekwa kwenye asilimia 50 ya GDP kwa nchi zote wanachama.
Mkurugenzi Mtendaji EABC, Andrian Njau ameitaka EAC kuharakisha mchakato wa safaru hiyo ili kufungua milango ya kiuchumi miongoni mwa wanachama na kufungua mipaka ya kibiashara pasipo na vikwazo.
“Hii itaongeza kasi na nguvu ya mshikamano baina ya nchi wanachama na kufungua zaidi fursa za kiuchumi,” amesema Njau.
Amesema pia itasaidia sekta binafsi kubadilishana uzoefu na kukuza zaidi jumuiya kiuchumi na kufanikisha malengo iliyotarajiwa ya kukua kwa asilimia 5.1 mwaka 2024, kutoka asilimia 4.9 mwaka 2023. Na kukua kutoka asilimia 15 ya sasa hadi asilimia 40 ifikapo 2028.
Kwa sasa mauzo ya nje ya EAC kwenda kwingineko ya dunia yaliongezeka hadi Dola 26.9 bilioni za Marekani mwaka 2023, kutoka Dola 25 bilioni mwaka 2022 na mauzo ya nje ya Afrika yalifikia Dola 9.7 bilioni za Marekani mwaka 2023 wakati bidhaa kutoka Afrika zilifikia Dola 9.7 bilioni kutoka Marekani na Dola 7.9 bilioni mnamo 2022
Hadi sasa nchi wanachama wa EAC, ni Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tanzania.
Aidha katika mkutano huo ulikusudia kuainisha na kuwasilisha vipaumbele vya utetezi wa sera za sekta binafsi wakati wa kupitia maendeleo ya utekelezaji wa ahadi za EAC ili kukuza biashara na uwekezaji ndani na nje ya EAC.
Majadiliano yalijikita katika kubainisha vikwazo vya biashara na uwekezaji vinavyokabili sekta binafsi na kupendekeza suluhisho la uwezekano.
Kwa upande mwingine, Nduva amesema EAC inaendelea kuratibu utekelezaji wa mfumo wa uhuru wa masoko ya usafiri wa anga katika kanda, ambao ungetia moyo ushindani na kupunguza gharama za nauli za ndege kupitia nguvu za soko.
Kuhusiana na hilo, amesema EAC imekamilisha kanuni za uhuru wa anga na kuandaa mikakati ya kupunguza gharama za usafiri wa anga katika eneo la EAC.
Katika maoni yake, Njau amesisitiza kuwa utetezi wa sera za biashara, uwekezaji, na viwanda ni kipaumbele cha juu kwa EABC.
Amebainisha kuwa, jitihada hizo zinalenga kuondoa vikwazo na kuimarisha fursa za biashara na uwekezaji ndani ya EAC na nje.