SERIKALI YA TANZANIA YAWEKEZA BILIONI 840 KUREKEBISHA MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIWA NA MVUA ZA EL-NINO – MWANAHARAKATI MZALENDO

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania imeelekeza kiasi cha Shilingi Bilioni 840 (Dola za Marekani Milioni 325) kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na mvua kubwa za El-Nino na Kimbunga Hidaya. Hatua hii inakuja baada ya mvua hizo kuathiri sana mawasiliano ya barabara, madaraja, na makalvati katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Katika taarifa aliyoitoa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bashungwa alisema kuwa mvua za El-Nino zilizonyesha kati ya Septemba 2023 hadi Aprili 2024 zilileta athari kubwa kwenye miundombinu, hali iliyopelekea Serikali kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 72.1 kwa ajili ya matengenezo ya dharura.

“Wizara yetu inaelewa umuhimu wa kuimarisha madaraja na makalvati, kwani mvua inaponyesha, barabara zinaweza kuwa na mawasiliano kwa shida, lakini ukosefu wa madaraja au makalvati unaweza kuzuia mawasiliano kabisa,” alisema Bashungwa.

Akiwaeleza wajumbe wa Kamati, Bashungwa aliongeza kuwa tathmini ya awali inaonyesha kuwa kiasi cha Shilingi Trilioni 1.07 kinahitajika ili kurekebisha miundombinu yote iliyoharibiwa. Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba miundombinu hiyo inarejea katika hali yake ya awali.

Waziri Bashungwa pia alielekeza Wakala wa Barabara (TANROADS) kufanya mapitio ya kina ya barabara zilizofanyiwa usanifu miaka ya nyuma ili kuhakikisha kuwa ujenzi na matengenezo yanaendana na hali halisi, mabadiliko ya mazingira, ongezeko la watu, na ukuaji wa miji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Selemani Kakoso (Mb), ameshauri Wizara ya Ujenzi kushirikisha Wabunge katika maeneo yaliyolengwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa ujenzi na matengenezo yanatekelezwa kwa tija na kulingana na mahitaji halisi. Kakoso pia ameitaka Wizara kuimarisha usimamizi wa Wakala wa Barabara (TANROADS) na Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) ili kuongeza vyanzo vya mapato na kufanikisha mipango ya baadaye ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts