Serikali yawaonyesha wafanyabiashara fursa za mikopo

Arusha. Serikali imewataka wafanyabiashara nchini kuchukua mikopo kutoka kwenye taasisi zinazotambuliwa kisheria, kuliko kuingia tamaa ya mikopo ya mitandaoni ambayo imekuwa ikiwaumiza.

Pia, imewataka kuchukua fedha za kiwango cha hitaji lao la kibiashara badala ya kuchukua mikopo mikubwa inayowasumbua kwenye kuirejesha na kuharibu ustawi wa biashara zao.

Rai hiyo imetolewa leo Agosti 23, 2024 na Ofisa Biashara wa Mkoa wa Arusha, Njivaine Mollel kwenye kongamano la wafanyabiashara zaidi ya 300 ambao ni wateja wa benki ya NMB lililofanyika jijini Arusha.

Mollel amesema kuwa hivi karibuni kumekuwa na matangazo mengi ya mikopo ya mitandaoni lakini nyingi zimekuwa sio msaada kwa wananchi kutokana masharti magumu ya kulipika lakini wengine kutumia mwanya huo kutapeli watu.

“Unakuta mtu anakuambia anatoa mkopo wa Sh1 milioni na urejeshe asilimia 30 ya mkopo na wewe unakubali kwa sababu una shida ya hela, kwanini usiende kwenye taasisi za kifedha zinazotambuliwa na Serikali kama benki ya NMB hapa ambazo wamepewa masharti ya kutoa riba chini ya asilimia 15, kama sio unayataka ni nini,” amesema Mollel.

Alitumia nafasi hiyo kuzishukuru wadau wa sekta binafsi hasa taasisi za kifedha ambazo zimekuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa Tanzania.

Mollel amesema hivi karibuni Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kupitia taarifa ya Sera ya Fedha ya Mapitio ya Katikati ya Mwaka 2023/2024, imeonyesha ukuaji wa mapato Tanzania Bara unatarajiwa kufikia takribani asilimia 5.5 mwaka 2024, huku uchumi wa Zanzibar ukitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 7.4.

Pia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inaonyesha kuwa uchumi wa Tanzania utakuwa zaidi ya asilimia 6.1 hadi mwishoni mwa mwaka 2024 na kuwa moja ya nchi yenye uchumi imara Afrika Mashariki.

“Hayo mafanikio yametokana na mchango wa sekta binafsi hasa mabenki ambao wamekuwa wakitoa fedha zao kuwakopesha wafanyabiashara na wawekezaji kufanikisha shughuli zao,” amesema Mollel.

Amesema kuwa mafanikio ya wafanyabiashara kuingiza fedha nyingi kwenye mzunguko inapunguza mahitaji ya kifedha mitaani hivyo kukuza uchumi wa nchi.

“Benki ya NMB imekuwa moja ya msaada mkubwa kwa serikali maana nimesikia hapa wanatoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo hadi Sh 100 milioni ndani ya saa 24 mteja atakapotimiza masharti, hapo amesaidia wananchi na serikali kwa ujumla” amesema Mollel.

Awali, Meneja wa Kanda wa NMB, Baraka Ladislaus amesema benki hiyo imekua kutoka kukopesha Sh200,000 kwa wateja wadogo, hadi sasa wanakopa Sh100 milioni ndani ya saa 24 mteja atakapokidhi vigezo na kutimiza masharti.

Amesema kuwa mbali na hilo pia wana mikopo ya papo kwa hapo ambayo wateja wa benki hiyo wanaweza kukopa kiasi chochote wanachotaka kwa njia ya simu yake hadi shilingi milioni moja kwa simu zao bila masharti wala dhamana yoyote.

“Lengo la kufanya hivi ni kuwaokoa wateja wetu na mikopo umiza ambayo wanakimbilia kutokana na uharaka wake bila kujali riba wala taratibu za kuzilipa, kitendo ambacho imekuwa kilio na mzigo mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo ambao wamefikia hadi hatua ya kufilisiwa mali zao” amesema Meneja huyo.

Mmoja wa washiriki wa Kongamano hilo, Anna Sirikwa amesema benki ya NMB imekuwa msaada mkubwa kwao hasa elimu ya kifedha na mikopo ambayo imekuwa ikisaidia kukuza biashara zao bila masharti magumu wala dhamana yoyote.

Related Posts