Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Takukuru mkoa wa Ruvuma wametoa mafunzo kwa waandishi wa habari katika manispaa ya songea namna ambavyo wao kama vyombo vya habari wana nafasi kubwa ya kuzuia rushwa kipindi cha uchaguzi
Ameyasema hayo hii leo Kaimu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Ruvuma Janeth Haule, wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuwataka kua makini katika kuelekea kipindi hichi cha uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kutumia ushawishi walionao kwenye jamii kwa kubadili fikra za wananchi kuhusu athari za rushwa.
Amesema kua vyombo vya habari vimekua vikiaminiwa sana katika jamii hivyo waandishi wanapaswa kutumia taaluma zao katika kutoa elimu kwenye jamii juu ya mapambano dhidi ya rushwa kwani kutoa na kupokea rushwa ni kosa la jinai na ni utovu wa maadili katika jamii.
Nae Ndg Yahaya Mwinyi kutoka TAKUKURU mkoa amesema wamejikita katika utoaji elimu ili watanzania waweze kuelimika na kuichukia rushwa na kubadili mitizamo hasi hivyo waandishi wa habari wanapaswa kuhamasisha wananchi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na TAKUKURU kwa kufichua maovu kwenye jamii .
Pia Yahaya Mwinyi amesema vyombo vya habari vinapaswa kuwashawishi wananchi kushiriki kikamilifu uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuchagua viongozi bora watakaoenda kubadilisha matokeo chanya ya changamoto zao kwenye jamii ili viongozi hao wawafikishe kwenye ustawi bora wa nchi
Aidha amesema kuna madhara mengi ya rushwa kwenye uchaguzi yakiwemo kumnyima mpiga kura haki ya kuchagua kiongozi bora anayemuhitaji, kukwamisha maendeleo kwa jamii kwa kupata viongozi wasio waadilifu hivyo kupelekea kuongezeka kwa umasikini nchini Hivyo waandishi wa habari wanapaswa kuhabarisha umma kwa kubadili fikra za wananchi na kueleza juu ya umuhimu wa wananchi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kwani ni muhimu kwa mustakabali wa taifa.