Wafanyabiashara Soko la Chief Kingalu wagoma, wamtaka DC atengue kauli

Morogoro. Baadhi ya wafanyabiashara wa Soko kuu la Chief Kingalu katika Manispaa ya Morogoro leo Agosti 23, 2024 wamegoma kufungua biashara zao na kufunga barabara inayoingia sokoni hapo, wakipinga wafanyabiashara wadogo kuruhusiwa kufanya biashara nje ya soko hilo.

Wafanyabiashara hao wamedai kuwa agizo la wafanyabiashara hao kufanya biashara nje ya soko hilo lilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala na wamemtaka atengue kauli yake.

Akizungumzia madai hayo leo, DC Kilakala amesema maelekezo aliyotoa yeye ni kutowapiga na kuwachukulia vitu vyao wafanyabiashara wadogo na wapewe maelekezo ya wapi wafanyie niashara zao.

“Serikali ilishatenga maeneo ya watu kufanya biashara kwa hiyo haiwezekani watu wakapanga biashara barabarani na wale watu wa sokoni watauza wapi?” amehoji.

Amewataka wafanyabiashara hao kufungua biashara zao kama kawaida, kwani hakuwa na lengo baya.

“Maelekezo niliyotoa mimi ni kwamba watu wasipigwe kwa sababu kuna kasumba ya watu kuwapiga na kuwachukulia vyakula vyao waelekezwe utaratibu wanatakiwa wafanye biashara wapi, sasa inawezekana kuna mtu ameleta taharuki kwa jambo hilo,” amesema Kilakala.

Soko la Chief Kingalu Morogoro lililofungwa na wafanyabiashara kutaka ufumbuzi wa kuruhusiwa kwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo kufanyia biashara zao barabarani. Picha na Lydia mollel

Akizungumza na Mwananchi Digital, Japhet Dickson mfanyabiashara wa soko hilo amesema wamefanya mgomo huo, baada ya Mkuu wa Wilaya Morogoro, Mussa Kilakala kuwataka wanawake wanauza mboga kurudi kufanya biashara katika eneo ambalo wamachinga walitolewa.

“Sisi tuliletwa katika soko hili, lakini tunashangaa mkuu wa wilaya aliyekuja anaruhusu wanawake warudi tena barabarani jana tumeshinda hapa sokoni tumelala kwa sababu hakuna wateja,” amesema Dickson.

Mwenyekiti wa soko hilo, Khalid Mkunyagela amesema kuwa changamoto hiyo imesababisha wateja kushindwa kuingia sokoni kununua bidhaa, hali inayosababisha biashara ndani ya soko kukosa wateja.

“Kwa hali iliyofikia inaonekana tunazidi kuonewa, kwani kila kiongozi anayekuja anakuja na matamko yake, bila kutusaidia. Je, ili jengo kubwa lililojengwa kodi italipwa na nani na wafanyabiashara waliopo kipato watakipata wapi?” alisema Mkunyangela.

Naye, Batuli Ibrahim mfanyabiashara wa soko hilo amesema, wanategemea biashara zao kupata fedha kuedeshea maisha yao, lakini sasa hawapati wateja.

“Leo tumeamua kufunga biashara zetu kutokana na kauli ya mkuu wa wilaya na tumeona kwa vitendo, kwa kuwa tulisikia hatukuamini, lakini jana asubuhi tulipo amka tukaenda kutazama yale maeneo kama kweli wamepanga biashara zao, kwa hiyo sisi tuliazimia kufunga soko maana linaonekana halina maana,” amesema.

Related Posts