Dar es Salaam. Serikali imetakiwa kuweka mazingira sawa ya kujifunzia kwa wanafunzi wote nchini, hususan walioko vijijini ili kuwajengea hamasa ya kupenda somo la hisabati na kuwapa fursa ya kushindana na wenzao wa nchi nyingine.
Hatua hiyo kwa mujibu wa wanafunzi, itawaongezea mwamko wa kulipenda somo hilo, ambalo kwa muda mrefu wengi wameonekana kufeli.
Miongoni mwa wanafunzi waliotoa ushauri huo ni Stella Maliti ambaye ni Mwanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Maria, ambaye pia ni mshindi wa mashindano ya Hisabati ya Afrika ya Pan African Mathematics Olympiads (PAMO) 2024, yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Witwatersrand (Wits University), Johannesburg, Afrika Kusini.
“Ninaiomba Serikali itengeneze mazingira mazuri kwa wanafunzi walipende somo la hisabati tofauti na ilivyo sasa ambapo mwamko wake siyo mkubwa sana,” amesema.
Anaongeza kuwa “Hii itasaidia wanafunzi wengi kupata hamasa na hata kushiriki mashindano ya kimataifa ya hisabati pindi yanapotokea. Pia naishauri kuungana na Chama cha Hisabati Tanzania (Chahita) ili kuongeza uzito wakati wanafunzi wanapokuwa wanashiriki mashindano haya kama tulivyoona kwa wenzetu wa Rwanda,” amesema.
Stella ambaye ni wa mwisho kuzaliwa katika familia ya watoto wawili amewasihi wanafunzi wenzake kuongeza bidii na kutokata tamaa, hususan katika somo la hisabati, akisisitiza juhudi na uvumilivu ni muhimu kwa mafanikio.
“Ushauri wangu kwa wanafunzi wenzangu waliko shuleni wasikate tamaa wapambane hadi tone la mwisho bila, pia waondoe dhana kwamba hisabati ni ngumu hapana, kuendelea kuamini hivyo ndiko kunatufanya tushindwe kufaulu. Pia walimu wanapaswa kuwasaidia wanafunzi badala ya kuwa wakali,” amesema Stella.
Angel Augustino anayesoma kidato cha tano shuleni hapo, ameiomba Serikali kuongeza mashindano zaidi ya somo la Hisabati ili kuongeza ushindani zaidi kwa wanafunzi na kuchochea hamasa.
“Mwenzetu hapa leo amefanikiwa kuibuka kinara, hii ni jambo zuri kwani litamsaidia siku za usoni, hivyo Serikali na wadau wengine ni vyema wakaongeza mashindano kama haya ili kuchochea ushindani zaidi ambao utakuwa na faida kwa nchi siku za usoni,” amesema Angel.
Mkuu wa shule hiyo, Constansia Simon amesema kando na medali hizo kuiletea heshima shule na nchi kwa ujumla lakini siri kubwa ya mafanikio ni nidhamu ambayo amekuwa nayo mwanafunzi huyo, huku akitoa wito wa kuendelea kuibuliwa kwa wanafunzi wengi zaidi.
“Ushindi wa Stella umetupa nguvu sana za kuendelea kufanya vizuri kwani ameweza kutuletea medali mbili za shaba mtoto wa kike, hivyo kwetu hili ni jambo la kufurahisha. Siri kubwa ya Stella ni nidhamu katika kazi kwani amekuwa na nidhamu ya hali ya juu sana, hivyo nitoe wito kwa wanafunzi wote nchini kwamba ili ufanikiwe katika kila jambo lazima uwe na nidhamu.
“Wito wangu kwa Chahita waendelee kufika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuibua vipaji kama hivi kwani itatujengea heshima kama nchi na kuondoa dhana iliyozoeleka kwamba hesabu ni ngumu,” amesema Constansia.
Christian Haule ambaye ni Mwalimu wa somo la hisabati shuleni hapo amewasihi walimu wa somo hilo nchini kupunguza ukali ili kuwavutia wanafunzi zaidi.
Hayo ni mafanikio makubwa kwa Tanzania kwani katika mashindano ya mwaka 2023 yaliyofanyika Kigali, Rwanda, Tanzania iliwakilishwa na wanafunzi sita ambao hawakufanikiwa kupata medali yoyote na walipata jumla ya maksi 10 pekee.
Hata hivyo, mwaka huu, wanafunzi watano walioshiriki wamepata alama 37 na kuleta medali nne, ikionyesha ongezeko kubwa la ubora katika mashindano hayo.
Kando na Stella wanafunzi wengine walioshiriki mashindano hayo kwa mwaka huu kutoka nchini Tanzania ni Ambrose George Rutashobya wa Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Iyunga (alipata medali), Ilham Abdulla Awadh, Shule ya Sekondari ya Feza, Zanzibar, Mwanaarab Said Mbwana, Shule ya Sekondari Lumumba, Zanzibar na Zacharia Mataiga Mwita wa shule ya Sekondari Azania (alipata medali).