WANNE WASIMAMISHWA KAZI WAKIDAIWA KUCHELEWESHA MATIBABU – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, John Kayombo amewasimamisha kazi watumishi wanne ambao ni madaktari wawili na wauguzi wawili wa Kituo cha Afya Kaloleni ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili za kuchelewa kutoa huduma za matibabu kwa majeruhi.

 

 

 

Hatua hiyo imefuatia kusambaa kwa taarifa kupitia mitandao ya kijamii ikiwatuhumu watumishi hao kushindwa kumpatia huduma majeruhi kwa wakati.

 

 

 

Taarifa ya awali inaonyesha majeruhi huyo alipokelewa kituoni hapo Agosti 21, 2024 saa 4 asubuhi na kupatiwa huduma ya dharura ikiwemo kushonwa na kufungwa majereha na kisha kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mt. Meru kwa ajili ya matibabu zaidi.

 

 

 

Pamoja na kupewa rufaa hiyo, walalamikaji walionyesha kutoridhishwa kutokana na kuchelewa kupatikana kwa gari la kubeba wagonjwa na hivyo kuamua kumpeleka mgonjwa wao Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mt.Meru kwa kutumia machela ya kituoni hapo kinyume na utaratibu.

 

 

 

 

Kufuatia tukio hilo Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, John Kayombo ameunda timu ya ufuatiliaji wa tuhuma hizo ikiwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Halmashauri ya Jiji la Arusha ambayo imeanza kazi jana Agosti 22, 2024.

Related Posts