Arusha. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha John Kayombo amewasimamisha kazi watumishi wanne wa Kituo cha Afya Kaloleni ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili za kuchelewesha huduma kwa majeruhi.
Kati ya waliosimamishwa wawili ni madaktari na wengine ni wauguzi ambao taarifa zao zilisambaa katika mitandao ya kijamii ikiwatuhumu kuchelewa kutoa huduma kwa majeruhi wa ajali ya bodaboda Baraka Mudadu (21) Mkazi wa Mianzini.
“Taarifa ya awali inaonyesha majeruhi huyo alipokewa kituoni hapo Agosti 21, 2024 saa nne asubuhi na kupatiwa huduma ya dharura ikiwamo kushonwa na kufungwa majeraha ya kichwani yaliyokuwa yakitoa damu,” amesema Kayombo leo alipozungumza na waandishi wa habari.
“Baada ya hapo inaonekana alipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa Mount Meru kwa ajili ya matibabu zaidi.”
Pamoja na mgonjwa huyo kupewa rufaa hiyo, Kayombo alisema walalamikaji walionyesha kutoridhishwa kutokana na kuchelewa kupatikana gari la wagonjwa, hivyo kuamua kumpeleka hospitali ya rufaa kwa kutumia machela ya kituoni hapo (stretcher) kinyume na utaratibu.
“Kutokana na hilo, nimeunda timu ya ufuatiliaji wa tuhuma hizo ikiwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Halmashauri ya Jiji la Arusha na imeanza kazi tangu Agosti 22, 2024 na taarifa ya uchunguzi huo itatolewa utakapokamilika,” amesema Kayombo.
Pia, ametumia nafasi hiyo kuwaagiza watoa huduma wote na watumishi kwa jumla kutoa huduma kwa wananchi kwa kufuata miongozo, weledi, maadili ya kitaaluma pamoja na sheria taratibu na kanuni.
Steven Mesiaki, amesema rafiki yake amepata ajali asubuhi ya Agosti 21, 2024 na kuwahishwa katika kituo hicho cha afya Kaloleni na kubainika kuwa na majeraha makubwa kichwani, hivyo alipatiwa huduma ya awali na kesho yake kuandikiwa rufaa katika Hospitali ya Mount Meru.
“Tangu asubuhi wanajizungusha hawataki kumpeleka na tulipouliza wanasema gari halina mafuta lakini hawataki kunyoosha kuwa wanataka hela ya mafuta bali wanatuzungusha ili tutoe rushwa.
“Na sisi tumegoma kujiongeza na kutoa hela hiyo tukaamua kuchukua machela yao na kumkokota hadi hapa hospitalini na tunashukuru Mungu tumemfikisha salama na kwa wakati na tumepokewa haraka,” amesema Mesiaki.