WAZAZI WATAKIWA KUWAHAMASISHA VIJANA KWENDA SHULE – MWANAHARAKATI MZALENDO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha vijana wao wanapata elimu kwa kuwapeleka shule, hasa katika shule za sekondari. Waziri Mkuu alisisitiza kuwa bila elimu, vijana hawawezi kufikia malengo yao na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza jana na wakazi wa kijiji cha Mtondo, Kata ya Nambiranje, wilayani Ruangwa, Waziri Mkuu alisema, “Wazazi wenzangu hakikisheni vijana wenu wanaenda shule. Hatuwezi kufika mbali kama vijana wetu hawaendi shule. Tunajenga shule kila mahali, tunataka maeneo yote yawe na shule.”

Waziri Mkuu Majaliwa, ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, aliipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa mafanikio katika sekta ya elimu wilayani Ruangwa, akibainisha kuwa wilaya hiyo sasa ina shule tatu za wasichana pekee, ambazo ni Liuguru, Ruangwa Girls, na Lucas Malia. Pia, alieleza kuwa wilaya hiyo ina shule tano za sekondari zenye kidato cha tano na sita, ambazo ni Ruangwa, Mbekenyera, Nkowe, Lucas Malia, na Hawa Mchopa, huku shule ya sita ya Mandawa ikiwa inakaribia kukamilika.

Akizungumzia maendeleo katika sekta ya maji, Waziri Mkuu alieleza kuwa ingawa vijiji vyote 90 wilayani Ruangwa vilichimbiwa maji kupitia taasisi ya GAIN, mahitaji bado ni makubwa. Aliwahakikishia wakazi kwamba Serikali imetoa Shilingi bilioni 49 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji kutoka Nyangao, ambao unatarajiwa kunufaisha vijiji 34 vya wilaya ya Ruangwa na vijiji 29 vya wilaya ya Nachingwea.

Kuhusu umeme, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa vijiji vyote wilayani Ruangwa sasa vina umeme, na juhudi zinaendelea kusambaza umeme kwenye ngazi ya vitongoji. “Leo hii hakuna kijiji kisichokuwa na umeme,” alisema, akisisitiza kuwa Serikali imefanya juhudi kubwa kuhakikisha huduma za umeme zinawafikia wananchi wengi zaidi.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu aligusia changamoto za miundombinu ya barabara, akitaja barabara kadhaa zinazohitaji ukarabati ili kufikisha huduma za msingi kama afya na elimu kwa wananchi. Alisema kuwa barabara ya kutoka Mandawa Chini hadi Mtondo, Nanjalu hadi Mtondo, Nambiranje hadi Mtondo, na kutoka Namiyenje hadi Mtondo, ziko kwenye mpango wa ujenzi.

Aidha, Diwani wa Kata ya Nambiranje, Mossa Mohammed Mtejela, alimuomba Waziri Mkuu kuongeza fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara na daraja kwenye kijiji cha Mkaranga, ambapo alisema kuwa kiasi cha Shilingi milioni 300 kilichotengwa hakitoshi kukamilisha ujenzi huo. Pia, Diwani Mtejela aliomba bweni la wavulana kujengwa katika sekondari ya Nambiranje ili kuwasaidia wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kutoka vijiji vya Mtondo na Nanjalu.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts