Chama cha soka mkoa wa Arusha (ARFA) imefanya uchaguzi wa nafasi mbali mbali na kupata viongozi watakaoiongoza kwa miaka minne.
Uchaguzi huo umefanyika leo mjini Namanga wilayani Longido ukiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya ARFA, wakili Hilda Mwanga na wasimamizi kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Karume Benjamin ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF na Rahim Shaban katibu wa kamati hiyo.
Katika mkutano wa uchaguzi huo jumla ya wajumbe 14 walipiga kura kuwachagua viongozi wa nafasi tatu za Mwenyekiti, Mjumbe Mkutano Mkuu TFF na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya ARFA na ikishuhudiwa viongozi ambao wameliza muda wakitetea nafasi zao.
Zakayo Mjema ameshinda nafasi ya mwenyekiti kwa kupigiwa kura zote za ndio baada ya kukosa mpinzani, wakati Obedi Joseph akichaguliwa nafasi ya Mjumbe Mkutano Mkuu TFF kwa kura 10 baada ya kuwashinda Omary Wali aliyepata kura nne na Frank Michael aliyetoka kapa.
Nafasi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji zilienda kwa Athanas Sarwatt kwa kura 12 na Siza Masaka kwa kura 14 , wakiwabwaga Aisha Hamis aliyeambulia kura mbili na Tareto Permin ambae hakutokea katika uchaguzi.
Mwenyekiti wa ARFA aliyetetea kiti, Zakayo Mjema amesema malengo makubwa bado ni yale yale kuendeleza soka la Arusha na kuhakikisha nyanja zote zinakuwa katika levo za juu, kuanzia waamuzi, Klabu na heshima katika utawala wa soka.
“Naomba sekretarieti kwa huu muda mchache muendelee na shughuli zenu kwa kushirikiana na kamati ya utendaji ila tutakaa kuunda sekretarieti mpya,” amesema Mjema.
Makamu mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Benjamin Karume amesema sasa ni wajibu wa viongozi hao kwenda kufanya kazi kwa mujibu wa wajumbe waliowachagua kwa maana ya kufanikisha mipango mikakati mbali mbali ya kuendeleza Soka.