Aussems, Nkata  ngoma nzito Kaitaba

KATIKA soka, rekodi zinaweza kuamua matokeo ya mechi, lakini uwezo binafsi nao huwezi kuuweka kando na hili ndilo linalosubiriwa kushuhudiwa leo kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba wakatui Singida Black Stars na Kagera Sugar zitakapowaingiza vitani makocha wa timu hizo.

Wenyeji Kagera Sugara wanacheza mechi hiyo ya kwanza msimu huu ikiwa chini ya kocha mpya, Paul Nkata kutoka Uganda dhidi ya Singida inayonolewa na Patrick Aussems ambaye huu ni mchezo wa pili baada ya awali kushinda mabao 3-1 mbele ya wageni wa ligi hiyo, KenGold ya Mbeya.

Hata hivyo, kuna wakati timu zinatembelea rekodi nzuri kupata ushindi hata kama hazipewi nafasi, huku zingine zinaweza kuwa vizuri lakini zikapata matokeo mabaya kwa sababu rekodi zinawakataa.

Mtihani huo, anao Aussems ambaye hana rekodi nzuri sana anapocheza na Kagera, lakini hata Uwanja wa Kaitaba si rafiki kwa timu anayoifundisha.

Singida ambayo zamani ilifahamika kama Ihefu, leo itacheza dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba uliopo mkoani Kagera katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaoanza saa 1:00 usiku.

Aussems ameanza ligi vizuri kwa ushindi wa 3-1 ugenini dhidi ya wageni KenGold wikiendi iliyopita kwa Emmanuel Keyekeh, Elvis Rupia na Camara Damaro waliyotupia kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Wakiwa bado na mtaji wa pointi tatu walioanza nao, vijana hao kutoka mkoani Singida wanakwenda kuzisaka pointi zingine tatu kwa Kagera Sugar inayonolewa na Kocha Paul Nkata raia wa Uganda.

Aussems si mgeni wa Ligi Kuu Bara kwani Mbelgiji huyo aliwahi kufika Kaitaba mara mbili akiwa na kikosi cha Simba, ya kwanza alipoteza kwa mabao 2-1 msimu wa 2018/19, kisha akashinda 0-3 msimu wa 2019/20.

Katika mchezo huo wa kwanza uliochezwa Kaitaba Aprili 20, 2019, Kagera Sugar ilipata mabao yake kupitia Kassim Khamis na Ramadhan Kapera, huku Emmanuel Okwi akifunga bao pekee la Simba, wakati Septemba 26, 2019 Mohammed Hussein na Meddie Kagere aliyepachika mawili waliipa Simba ushindi wa 0-3.

Aussems dhidi ya Kagera wakati akiwa Simba, alicheza mechi tatu dhidi yao, akashinda moja (0-3) na kupoteza mbili. Ukiachana na ile ya kwanza kufungwa Kaitaba (2-1), msimu huohuo 2018/19 akachapwa tena nyumbani Uwanja wa Uhuru bao 0-1. Ilikuwa Mei 10, 2019.

Kupoteza mechi mbili kati ya tatu dhidi ya Kagera, ni mtihani alionao Aussems kwani vichapo hivyo mfululizo vilitokea katika msimu wake wa kwanza ndani ya Simba, safari hii anakutana tena na Kagera akiwa na Singida BSs katika msimu wa kwanza. Nini kitatokea? Tusubiri tuone.

Ukiachana na rekodi za Aussems dhidi ya Kagera Sugar, Singida Black Stars ilipokuwa ikitumia jina la Ihefu katika misimu mitatu ya ligi nyuma, timu hizo zimekutana mara sita.

Katika mechi hizo sita, tatu zilizochezwa Uwanja wa Kaitaba, wenyeji Kagera Sugar hawajapoteza hata moja, wakishinda mbili na sare moja.

Kagera mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya wapinzani wao hao walipokuwa wakitumia jina la Ihefu walitoka 0-0, ilikuwa Juni 20, 2021. Kisha Desemba 2, 2022 ikashinda 2-0 na Februari 25, 2024 ikapata ushindi wa 2-1.

Kwa rekodi za jumla nyumbani na ugenini, Kagera ni wanyonge wa Singida (Ihefu) kwani wameshinda mechi mbili pekee, huku wakipoteza tatu na sare moja.

Mechi hii sio nyepesi kwa timu zote, kwani kila moja itataka kuvuna pointi, Singida ikitaka kurejea kileleni mwa msimamo kwa kuing’oa Simba iliyotofautiana nao mabao ya kufungwa na kufungwa, lakini Kagera ikitaka kuzipata pointi tatu za kwanza katika mbio za kusaka ubingwa kwa msimu huu.

Kocha Aussems ameuzungumzia mchezo huo na kusema; “Tumeanza ligi vizuri, safari ndio imeanza, tunatakiwa kuendelea na mwendo huu bila ya kuangalia yaliyotokea nyuma.”

Nkata akiwa naye anaanza majukumu mapya Kagera, amesema ameiandaa timu yake kushinda na itakuwa na maana kubwa wakianza na ushindi nyumbani.

Singida itaendelea kuwategemea nyota wake kama Rupia, Habib Kyombo, Marouf Tchakei, Ayoub Lyanga, Hamad Majimengi, Tra Bi Tra, Joseph Guede na Mohammed Camara wakataokuwa na kazi mbele ya wakali wa Kagera wanaoongozwa na Nassor Kapama, Samuel Onditi, Athuman Rajab, Erick Mwijage, Emmanuel Charles, Cleophas Mkandara na wengine ambao wanalifungua pazi la Ligi Kuu msimu huu.

Kagera 2-1 Singida BS (Ihefu)

Singida BS (Ihefu) 1-0 Kagera

Singida BS (Ihefu) 2-0 Kagera

Kagera 2-0 Singida BS (Ihefu)

Kagera 0-0 Singida BS (Ihefu)

Singida BS (Ihefu) 2-1 Kagera

Kabla ya mchezo wa Kagera Sugar dhidi ya Singida Black Stars, saa 10 jioni tutashuhudia Pamba Jiji wakiikaribisha Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Pamba wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kuanza na matokeo ya 0-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Wakiwa wamepanda daraja kucheza ligi kuu baada ya kupita takribani miaka 23, Pamba Jiji walianza na suluhu hiyo nyumbani na sasa wapo tena nyumbani kujiuliza kwa Dodoma Jiji katika vita ya timu za majiji.

Mecky Maxime akiwa na kikosi cha Dodoma Jiji, wanakwenda tena ugenini kucheza dhidi ya Pamba Jiji baada ya kutoka Kigoma walipofungwa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana, hivyo tutarajie mchezo unaozikutanisha timu ambazo kila moja inasaka rekodi kwa mwenzake ya kuanza vizuri.

Kocha Mserbia, Goran Kopunovic anayeinoa Pamba, amesema: “Kwa sasa hakuna kupoteza pointi, tunahitaji ushindi ambao utaiweka timu katika nafasi nzuri Kipindi hiki cha mwanzo wa ligi.”

Maxime akiwa na majukumu mapya ndani ya Dodoma Jiji, naye anaamini mchezo huo unaweza kuwarudisha katika hali nzuri baada ya kuanza ligi kwa kichapo na itaendelea kuwategemea nyota wake wapya kama Reliants Lusajo, Ibrahim Ajibu, Wazir Junior watakaoshirikiana na wakali wengine kama Emmanuel Martins, Ausgutino Nsata, Gustapha Saimon na Paul Peter.

Kwa Pamba Jiji inayosaka ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu tangu ipande itaendelea kuwategemea zaidi mastaa kama Erick Okutu, Ben Nakibinge waliotoka Tabora Utd, Kenneth Kunambi, Salum Kipemba, Ibrahim Abraham na kipa Yona Amos aliyefanya kazi kubwa dhidi ya Prisons katika mechi iliyopita.

Related Posts