Matajiri wa Chamazi, Azam FC wana kibarua kizito jijini Kigali, Rwanda, itakaposhuka uwanja mkubwa nchini humo wa Amahoro kumalizana na APR mabingwa wa nchi hiyo.
Azam imeshuka kwa kitisho ikisafiri na msafara wa watu 60 kwenye timu yao tu lakini pia ikasafirisha mashabiki wao mpaka nchini humo ili kuwaongezea hamasa ya kuhakikisha inafuzu baada ya kutangulia kushinda kwa bao 1-0.
Matajiri hao wanatambua kwamba mechi hiyo itakuwa ngumu itakayoanza muda sawa na ile ya Yanga ambapo inajua kuwa APR itakuja kama mbogo kusaka ushindi ikiwa nyumbani na hapo ndipo wanapotaka kuwanasia wenyeji wao.
Azam inaamini ilishindwa kutengeneza ushindi mkubwa kwenye mechi ya kwanza kutokana na Wanajeshi hao wa Rwanda kupaki sana basi kwa kujilinda na itakapokuwa kwao watashambulia na hapo ndipo watakapopata nafasi ya kuwafunga.
Hakuna mchezaji wa Azam ambaye alikuwa tayari kucheza mechi iliyopita ataukosa mchezo huo, wote wakithibitishwa kuwa wako sawa tayari kwa dakika 90 hizo ngumu.
Azam inaamini wapinzani wakubwa wa APR, Rayon Sports itawapa nguvu kwa kuwashangilia ambao wana urafiki nao lakini wenyeji wao wamekuwa na hesabu tofauti wakiona wanatosha kuing’oa timu hiyo.
Kocha wa Azam, Youssoyuf Dabo ametamba amejiandaa kulinda ushindi, lakini akitegemea zaidi nyota wa timu hiyo kuzitumia nafasi watakazotengeneza , kwani wiki iliyopita walishindwa kupata ushindi mnono nyumbani kwa nafasi walizopoteza na kuambulia bao la penalti ya Jhonier Blanco lililowatoa kimasomaso.
Dabo alisema timu yake ipo tayari kwa mchezo huo na kwamba hatua ya kwanza kwao itakuwa ni kutafuta bao la mapema ili kuwapa mlima mrefu wapinzani wao.
“Hatuwezi kujilinda, ushindi wetu ulikuwa muhimu lakini haukuwa mkubwa, tuna kikosi ambacho kinaweza kutengeneza ushindi mwingine hapa Kigali, tunaweza kutafuta bao la mapema ili kuwapa kazi wenzetu,” alisema Dabo.
“APR sio timu ndogo, wana kikosi kizuri na kocha mzuri, lakini ili wafuzu wanatakiwa kutushambulia na sisi tunataka watushambulie ili mchezo uwe wazi kwetu kwa kufanya kitu tofauti.”
Mchezo wa tatu utakuwa saa 2:00 usiku pale Uwanja wa June 30, jijini Cairo nchini Misri ambapo JKU ambayo imeweka rekodi kuwa timu iliyopokea kipigo kikali itakuwa mbele ya Pyramids.
JKU ilikubalina na Pyramids kuwa mchezo wao wa nyumbani utachezwa nchini humo ambao ndio huo waliokubali kipigo kikali cha mabao 6-0 na sasa wanahesabika wanarudi ugenini mbele ya matajiri hao.
Ili waiishangaze dunia kwa kupindua meza JKU inatakiwa kushinda kwa mabao 7-0, yakisubiriwa maajabu hayo lakini kikosi hicho kimeonekana kuendelea kujiandaa vizuri na mchezo huo wa marudiano, huku mechi ya mwisho itakuwa ni saa 2:30 usiku wakati Uhamiaji na Al Ahli Tripoli zitamalizanana.
Uhamiaji iliyopata nafasi hiyo ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na Chipukizi ambao ni mabingwa wa Kombe la ZFF kuchomoa baada ya kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) kwa madai ya kutokuwa na fedha ilipoteza 2-0 katika mechi ya awali ikiwa kama wenyeji na leo ina kazi ya kulipa kisasi, ili kuona kama itavuka kuifuata Simba inayosubiri mshindi wa mchezo huo kwa raundi ya pili.