Azam yatupwa nje kimataifa | Mwanaspoti

Azam imeondolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali baada ya kufungwa mabao 2-0 na APR katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Amahoro, Rwanda.

Mabao ya APR katika mchezo huo yamefungwa na Jean Bosco Ruboneka dakika ya 45 na Gilbert Mugisha dakika ya 62.

Kipigo hicho kinaifanya Azam kuondolewa kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya mchezo wa kwanza nyumbani kushinda 1-0 kupitia bao la mshambuliaji raia wa Colombia, Jhonier Blanco kwa penalti.

Katika mchezo huo wa leo, Azam hawakuwa na mashambulizi mengi huku wenyeji APR wakitawala muda mwingi.

Kitendo cha Azam kuondolewa kwenye hatua ya awali, inakuwa ni mara ya pili kwao kutokea hivyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya mara ya kwanza kushiriki mwaka 2015 kutolewa na Al-Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-2.

Mbali na Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam katika michuano ya kimataifa kwa ujumla ikiwemo ile ya Kombe la Shirikisho, haijawahi kucheza hatua ya makundi na badala yake imewahi kuishia hatua ya pili.

Related Posts