Dosari zilivyowatoa jela waliofungwa kwa kumkata mkono mwenye ualbino

Tabora. Mahakama ya Rufani Tanzania, imewaachia huru watu watatu wakazi wa Kijiji cha Mmale, wilayani Uyui mkoani Tabora waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha  jela kwa kosa la kumkata mkono mtoto mwenye ualbino na kuondoka nao.

Wameachiwa huru baada ya majaji watatu walioketi mjini Tabora, Shaban Lila, Patricia Fikirini na Pantrine Kente kutoa hukumu Agosti 22, 2024 wakikubaliana na rufaa iliyokatwa na warufani waliosota mahabusu kwa miaka 10.

Kuachiwa huru kunatokana na dosari zilizobainika kuwa jalada la kesi lilihamishwa kienyeji kutoka kwa hakimu mmoja kwenda kwa mwingine kinyume cha taratibu na vipande vya mifupa walivyodaiwa kukamatwa navyo kutotolewa mahakamani kama kielelezo.

Awali, kesi ya jaribio la kumuua Nkamba Ezekiel na kukutwa na vipande vya mifupa ya binadamu, iliwakabili washitakiwa sita ambao ninMussa Njile, Elizabeth Masanja, Bahati Kilungu, Mhoja Shija, Biria Masanja, na Regina Kashinje.

Ilidaiwa na upande wa mashitaka, usiku wa Julai 19, 2014, katika Kijiji cha Uyui wilayani Tabora washitakiwa walijaribu kusababisha kifo cha Ezekiel kwa kumkata mkono wa kulia na kuondoka nao kusikojulikana.

Katika shitaka la pili, upande wa mashitaka ulidai takribani mwaka mmoja baadaye (Mei 21, 2015) wakiwa katika Hoteli ya Maji iliyopo Kata ya Nyasubi, Kahama walipatikana na vipande tisa vya mifupa ya mwanadamu.

Baada ya kuwasikiliza mashahidi 18 na kupokea vielelezo 14, Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora iliyokuwa na mamlaka ya nyongeza, iliwaachia huru Mhoja Shija, Biria Masanja na Regina Kashinje.

Mahakama iliyotoa hukumu Aprili 1, 2022 iliwatia hatiani mshitakiwa wa kwanza, Mussa Njile na wa pili Elizabeth Masanja waliohukumiwa kifungo cha maisha, huku wa tatu, Bahati Kilungu akihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.

Katika hukumu ya rufaa ya warufani hao iliyotolewa na jopo la majaji watatu, wamebatilisha mwenendo wa kesi hiyo, kufuta adhabu za vifungo walivyopewa na kuamuru waachiliwe mara moja kutoka gerezani.

Kwa mujibu wa majaji, licha ya warufani kudaiwa kukutwa na mifupa tisa ya binadamu iliyoshukiwa ni ya mwathirika, mifupa hiyo haikutolewa mahakamani kama kielelezo, badala yake upande wa mashitaka ukawasilisha hati ya utaifishaji pekee.

Mbali ya dosari hiyo, majaji wamesema upande wa mashitaka ulishindwa kuonyesha kama mnyororo wa utunzaji vielelezo ulifuatwa, na haionyeshi kilihamishwaje kwenda maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali hali iliyosababisha Jamhuri imuite shahidi wa 18.

Dosari nyingine ya wazi wamesema ni shahidi wa 18 kuwa wa Jamhuri wakati hakuwepo kwenye orodha ya mashahidi wala maelezo yake hayakusomwa wakati wa committal (hatua ya kisheria ya kumkabidhi mshitakiwa kwa mamlaka kwa ajili ya kesi) kinyume cha kifungu namba 246(2) na 289(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Majaji wamesema kwa kuwa shahidi huyo hakuwemo kwenye orodha na wala maelezo yake hayakusomwa, milango ilikuwa wazi kwa Jamhuri kupitia njia ya kisheria kwa kifungu 289(1) cha CPA kutoa notisi ya kuongeza mashahidi.

Kutokana na dosari walizoainisha, majaji wamekubaliana na rufaa ya warufani, hivyo kubatilisha mwenendo wa kesi na kufuta adhabu waliyokuwa wamepewa, wakiamuru warufani waachiwe kutoka gerezani.

Mwenendo wa kesi hiyo unaonyesha, upande wa mashitaka ulidai Julai 19, 2014, washitakiwa wote sita walishiriki kumkata mkono Nkamba Ezekiel na kujaribu kumuua.

Ezekiel aliyepata majeraha alipelekwa Hospitali ya Ndanda kwa matibabu na tukio hilo likatolewa taarifa polisi.

Watuhumiwa wa tukio hilo waliodaiwa kutoroka kutoka eneo la tukio, walikamatwa Mei 21, 2015 katika Hoteli ya Maji iliyopo Kahama wakiwa na viungo vya binadamu na walipohojiwa na polisi walikiri kutenda kosa hilo.

Viungo hivyo vya binadamu vilifanyiwa uchunguzi wa kisayansi katika maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (CGCL) na uchunguzi wa vinasaba (DNA) ulithibitisha kuwa mifupa ile tisa waliyokamatwa nayo ilikuwa ya binadamu.

Mahakama iliwatia hatiani washitakiwa watatu na kuwaachia huru watatu kwa kukosekana kwa ushahidi.

Waliotiwa hatiani, walikata rufaa wakiegemea sababu tano. Kila mmoja aliwasilisha rufaa yake lakini mahakama iliziunganisha na kuwa moja. Wakati wa usikilizwaji waliwakilishwa na wakili wa kujitegemea Stella Nyakyi, upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Enosh Kigoryo.

Akiwasilisha hoja kwa niaba ya warufani, Nyakyi alidai kesi ilisikilizwa na hakimu mkazi mwenye mamlaka ya nyongeza na hilo lilitokea baada ya jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kulihamishia jalada kwa hakimu huyo.

Alidai jaji alimpangia Hakimu Mkazi Mwandamizi, Gladys Barthy kusikiliza kesi hiyo.  Hata hivyo, kumbukumbu zinaonyesha wakati wa usikilizwaji wa awali, ni hakimu Seraphine Nsana aliyesikiliza kesi hiyo kitendo ambacho kilikiuka kifungu cha 256A (1) cha CPA na kufanya mwenendo wa kesi kuwa batili na kwamba, hiyo inatosha kuikubali rufaa.

Majaji waliosikiliza rufaa hiyo, wamekubaliana na hoja hiyo wakieleza mwenendo wa kesi uliokuwa mbele ya hakimu Barthy ulikuwa batili kwa kuwa hakuwa na mamlaka ya kuisikiliza.

Majaji waliwataka mawakili watoe hoja wanatokaje katika mazingira hayo; Nyakyi alipendekeza rufaa ikubaliwe akianisha mapungufu matatu, moja ni kuwa hati ya mashitaka inatofautiana na ushahidi.

Alieleza hati ya mashitaka, inazungumzia vipande tisa vya mifupa ya binadamu, lakini shahidi wa nne wa Jamhuri alizingumzia vipande sita vya mifupa ya mwanadamu.

Hoja ya pili ni kuwa mifupa hiyo, iwe ni sita au tisa, haikutolewa mahakamani kama kielelezo wakati wa usikilizwaji wa kesi na tatu, maelezo ya kukiri ya mshitakiwa wa kwanza na wa pili, hayakupatikana kwa njia sahihi zinazokubalika kisheria.

Alitoa mfano wa maelezo ya mrufani wa kwanza, yalirekodiwa nje ya saa nne zinazotakiwa kisheria, huku ya mrufani wa pili hayaelezi kama alisomewa au aliyasoma mwenyewe kama kifungu 57(3) cha CPA kinavyotaka.

Alieleza anadaiwa kukiri kuwa yeye ndiye alikata mkono wa mke wa mtu badala ya mkono wa mtoto (Nkamba Ezekiel), hivyo maelezo hayo ya ungamo yanazungumzia mtu tofauti na anayetajwa katika hati ya mashitaka.

Dosari nyingine ni kuwa mnyororo wa utunzaji na uhamishaji vielelezo tangu mifupa inachukuliwa, haikuzingatiwa na kutoa mfano kuwa inaelezwa ilipelekwa Kituo cha Polisi Kahawa lakini haielezi nani aliipeleka.

Kuhusu majeraha aliyoyapata mtoto huyo, wakili alieleza adhabu ni muhimu kwa ajili ya kurekebisha na kuwa funzo kwa wengine, lakini akakubali kuwa hakuna adhabu itatolewa itabadilisha ukweli kuwa mtoto alikatwa mkono.

Katika hoja hizo, wakili aliiomba mahakama ibatilishe mwenendo wa shauri hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, kubatilisha amri ya kuwatia hatiani washitakiwa, kuiweka kando adhabu na kuwaachilia huru warufani.

Wakili wa Serikali, Kigoryo aliunga mkono hoja ya Nyakyi kwamba mwenendo wa kesi hiyo mbele ya Hakimu Nsana ulikuwa batili kutokana na kukosekana  uhamisho rasmi kutoka kwa hakimu aliyekuwa amepangiwa.

Alitoa sababu za kuunga mkono kuwa warufani waliunganishwa na mifupa iliyodaiwa ni ya binadamu, lakini kunabakia swali ambalo lilihitaji kujibiwa kabla ya kuwatiani hatiani nalo ni mifupa ile ilikuwa ni ya nani.

Sababu ya pili ni kuwa kulingana na shahidi wa 18 kutoka CGCL alisema alipokea sampuli za mate kutoka wa warufani kwa ajili ya kufanya DNA, lakini haielezi kwa nini sampuli hazikuchukuliwa kwa mama wa mtoto au mtoto mwenyewe.

Alisema kama mahakama itaagiza shauri hilo lisikilizwe upya, upande wa Jamhuri unaweza kutumia nafasi hiyo kuijenga upya kesi lakini sababu nyingine ni kuwa mifupa hiyo haikutolewa mahakamani kama kielelezo.

Hoja nyingine ni kuwa si hati ya utaifishaji wala mifupa yenyewe iliorodheshwa kama vielelezo muhimu wakati wa mchakato wa usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo ili kuihamishia Mahakama Kuu.

Aliunga mkono hoja kuwa mnyororo wa utunzaji na uhamishaji vielelezo ulikatika na pia shahidi wa 18 wa Jamhuri alitoa ushahidi  wakati hakuorodheshwa kama shahidi na maelezo yake hayakusomwa kwenye mchakato wa usikilizaji wa awali.

Related Posts