BIRMINGHAM, ENGLAND: UNAI Emery amepoteza mara moja tu kati ya tano alizokutana na Mikel Arteta. Na mechi tatu kati ya hizo – ikiwamo mbili za mwisho – kikosi chake kilizima kabisa tishio la fowadi ya Arsenal na kutoruhusu bao lolote.
Jambo hilo linaonyesha wazi kabisa staili ya soka la Emery ni matatizo makubwa kwa Arsenal, akiipa shida timu hizo mara zote walizokutana tangu alipoachana na timu hiyo mwaka 2019.
Baada ya kushinda mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England ilipoibabua West Ham United 2-1, Aston Villa inaamini ipo kwenye kiwango bora kabisa cha kutibua mipango ya Arsenal ya kufukuzia ubingwa mapema kabisa itakapomenyana nao leo, Jumamosi.
Ni kitu gani Emery amekuwa akifanya kumzidi ujanja Arteta na kumpa shida kwenye mechi zao?
Kuishambulia Arsenal upande wa kushoto
Emery anafahamu wazi eneo lenye udhaifu mkubwa kwa Arsenal ni upande wa kushoto na ndiyo maana katika mechi zote mbili za ushindi za msimu uliopita, winga wa kulia, Leon Bailey alihusika kuwaangamiza Arsenal kwa kufunga na kuasisti. Katika mechi hizo, Bailey alicheza kwa dakika 74 tu, lakini aliweka alama na kutoa mchango mkubwa katika mechi zote mbili. Emery anafahamu wazi Oleksandr Zinchenko amekuwa na shida nyingi na ndiyo maana ametumia winga wake wa kulia kuiangamiza Arsenal, kwa sababu hilo ndiyo eneo dhaifu kwenye timu ya Arteta.
Zinchenko ni fundi mpira unapokuwa kwenye miguu yake, lakini shida amekuwa hana nidhamu ya kubaki kwenye eneo lake na hilo ndilo ambalo Emery amekuwa akilitumia kumwaadhibu Arteta kupitia kwa winga Bailey.
Msimu huu mambo yanaweza kuwa tofauti kutokana na Jurrien Timber kupona, huku Arteta akisajili beki mwingine pia wa kuchenye eneo hilo la kushoto, Riccardo Calafiori – ambapo mmoja wao anaweza kuchaguliwa kuanza kwenye mechi hiyo ya Villa Park. Nini kitatokea? Ngoja tuone.
Upenyo kwenye safu ya kiungo
Kujaribu kupita katikati kwenye kiungo ni eneo ambalo Emery amekuwa akilitafutia namna ya kukabiliana nayo anapocheza na Arsenal. Kwa kukabia juu, kuna fanya kupunguza ukubwa wa eneo la kiungo ya juu, mahali ambako Arsenal imekuwa na nguvu zaidi. Bila shaka kocha wa Aston Villa atakuwa amepata somo kwenye mechi zote za msimu uliopita, alipojaribu kukabia juu na hivyo kupata shida kutokana na mikimbio ya viungo wa Arsenal kutoka kwenye eneo la juu yao.Kai Havertz, aliyecheza kiungo kwenye mechi hiyo, alikuwa na mikimbio ambayo iliwafanya Aston Villa kuwa kwenye wakati mgumu sana kukabiliana naye. Hata hivyo, Emery anafahamu eneo hilo ndilo linalopaswa zaidi kuwatibua Arsenal kama kweli unahitaji kupata matokeo mazuri dhidi yao.
Moja ya siri kubwa ya Aston Villa kucheza kwa kiwango bora sana kwenye kipindi cha pili cha mechi yao dhidi ya Arsenal iliyofanyika Aprili ni vila timu iliporudi nyuma na kulitawala eneo alilokuwa akicheza Odegaard, ambaye ni hatari zaidi unapomwaacha akizurura na mipira kwenye eneo hilo. Kocha Emery anafahamu wazi unapocheza na Arsenal unapaswa kumnyima uhuru Odegaard kwa maana ya kulibana eneo hilo. Kwenye kuhakikisha hilo, Emery anategemea zaidi huduma ya viungo wake Tielemans na McGinn ambao watasimama mbele ya mabeki wa kati kuwazima Arsenal kwa maana ya kumnyima Odegaard uhuru wa kuwa na mpira na kufanya anachoka. Hivyo, kwenye mchezo wa leo bila shaka, Emery atakuwa na mpango kama huo wa kuhakikisha Odegaard hachezi kwa uhuru.
Mikoba kwa Onana na Tielemans
Arsenal ya Arteta ilihusishwa na mpango wa kuwasajili Tielemans na Amadou Onana kabla ya viungo hao kutua Villa Park, ambako wamekuwa wakicheza pamoja na kuunda safu matata kabisa kwenye sehemu hiyo ya katikati ya uwanja. Onana na Tielemans walicheza vizuri kabisa kwenye mechi ya West Ham, walipocheza pamoja kwenye kiungo ya kukaba na kurudisha mipira kwenye himaya ya timu yao mara nyingi.
Kwenye eneo hilo Onana na Tielemans walisaidiana na Namba 10, Morgan Rogers, na bila shaka, Arsenal itakuwa na wakati mgumu itakapokwenda kuwakabili Aston Villa huko Villa Park. Upande wa kushoto kutakuwa na McGinn, ambaye kuna nyakati atakuwa anaingia kati kuongeza wingi. Lakini, katika kipute hicho cha kuwakabili Arsenal, silaha za Aston Villa zimekuwa kwenye mikono ya Onana na Tielemans. Kitatokea nini?
Mchakamchaka wa Ligi Kuu England utaendelea kwa mechi kadhaa wikiendi hii, ambapo kipute cha mapema kabisa kitakuwa huko uwanjani American Express, wakati wenyeji Brighton watakapokipiga na Manchester United katika mechi ya kibabe kabisa. Rekodi zinaonyesha kwamba katika mechi 14 ambazo timu hizo zilikutana, hakuna sare, ambapo Brighron imeshinda sita, nne nyumbani na mbili ugenini, huku Man City ikishinda nane, tano nyumbani na tatu ugenini. Kazi ipo.
Baada ya mechi hiyo ya mchana, zitafuatia mechi tano zitakazopigwa muda mmoja, jioni – ambapo Crystal Palace itakuwa Selhurst Park kucheza na West Ham United, wakati Fulham itajimwaga Craven Cottage kucheza na Leicester City, wakati mabingwa watetezi Manchester City watakuwa Etihad kucheza na wageni kwenye ligi, Ipswich Town, Southampton itacheza na Nottingham Forest huko St Mary’s wakati Tottenham Hotspur itakuwa London kucheza na wakali wa Merseyside, Everton. Mchezo wa usiku ni ule wa Aston Villa na Arsenal. Shughuli ni pevu kwelikweli.
Kesho, Jumapili kutakuwa na mechi tatu tu, ambapo Bournemouth itakuwa mwenyeji wa Newcastle United uwanjani Vitality, wakati huko Molineux, Wolves itakuwa na kibarua kizito cha kuwakabili Chelsea huku mchezo wa mwisho utakuwa Anfield, ambapo wenyeji Liverpool chini ya kocha wao mpya, Arne Slot watacheza mechi yao ya pili kwenye Ligi Kuu England kwa kumenyana na Brentford.