Kamati kuundwa kusaka fedha ufadhili wa masomo ya sayansi

Unguja. Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema wapo kwenye mchakato wa kuunda kamati maalumu ya kutafuta fedha kuongeza ufadhili wa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi, uhandisi na elimu tiba nje ya nchi.

Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Agosti 24, 2024 alipozindua bweni la wasichana, madarasa na maabara ya Sekondari ya Kizimkazi Dimbani ambayo yamejengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Amesema Serikali inaendelea kuhamasisha wanafunzi wengi wajitokeze kusoma masomo hayo kwa kuwa hakuna Taifa linaweza kuendelea kama halina wataalamu katika sekta hizo.

Profesa Mkenda amesema tayari Serikali imeanzisha mfuko maalumu wa ufadhili wa Samia ambao mwanafunzi katika maeneo hayo anapatiwa ufadhili na Serikali kwa asilimia 100 na kugharimiwa kila kitu anapokwenda nje kusoma.

“Kuna fursa nyingi za kusoma nje ya nchi hatuwezi kujifungia ndani kisha tukategemea kuendelea hata mataifa yaliyoendelea yanasomesha watu wake nje, kwa hiyo tuchangamkie fursa hii,” amesema.

“Tunataka kuunda kamati maalumu ya kutafuta fedha kwa kushirikiana na mabenki ili kuongeza mfuko huo kuwasaidia wanafunzi kusoma,” amesema.

Amewataka walimu na wazazi kuwahimiza wanafunzi kusoma masomo hayo kuanzia kidato cha kwanza ili wanufaike na fursa hiyo.

Profesa Mkenda amesema wakati wanaanzisha ofisi ya Atomu Zanzibar walitafuta watu wenye sifa lakini wamebaini kuna changamoto kubwa ya watu wenye elimu hiyo, hivyo wameanza mpango kuwekeza katika eneo hilo kuwasomesha watu kwenye sekta hiyo.

Amesema wameagiza itengwe bajeti katika taasisi hiyo kwa ajili ya kusomesha wataalamu.

“Kwa hiyo mtaona kuwa kuna fursa nyingi, yapo maeneo ambayo tunahitaji wataalamu lakini hatuna wa kutosha, tutumie fursa hii,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Tasaf, Shadrack Mzirai amesema katika kipindi cha pili cha uhaulishaji wa fedha kwa kaya masikini jumla ya Sh48.84 bilioni zimetolewa kwa kaya 53,441.

Amesema miradi 761 yenye thamani ya Sh15 bilioni imeibuliwa na kati ya kiasi hicho, Sh1.98 bilioni zimetumika kununua vifaa, huku Sh13 bilioni zikitumika kulipa ujira kwa wananchi wanaoshiriki kujenga miradi hiyo ambao wanatokana na kaya hizo zinazonufaika na mfuko.

“Miradi iliyoibuliwa ni pamoja na barabara, ujenzi wa shule, mazingira, uvuvi na miundombinu hivyo wananchi hao kujiongezea kipato kinachotokana na mfuko wenyewe,” amesema.

Amesema kupitia mpango huo wameanzisha vikundi vya ujasiriamali, ambavyo zaidi ya wananchi 23,000 wamenufaika.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdalla Said amesema madarasa manne yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 180 sawa na wastani wa wanafunzi 45 kila darasa yamejengwa.

Khamis  amesema maabara na madarasa hayo vimegharimu zaidi ya Sh400 milioni.

Amesema Serikali inaendelea kuhakikisha inaondoa changamoto za elimu ili wanafunzi wasisome mikondo miwili.

Related Posts