Kesi ya ofisa usalama, shahidi aeleza sifa za mshtakiwa

Dar es Salaam. Shahidi wa 10 wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Ofisa Usalama wa Taifa, Zaburi Kitalamo na wenzake wawili, amedai kuwa mshtakiwa huyo ana sura ya upole na pia huwa anaongea kwa upole kama mchungaji.

Sifa hizo ziliwafanya watu waliokuwapo ndani ya Mahakama ya wazi namba mbili wakisikiliza kesi hiyo kuangua vicheko, wakiwamo mawakili wa pande zote mbili.

Shahidi huyo, Hassan Ndutu (51) ambaye ni Mkaguzi wa Polisi, ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao.

Kitalamo au kwa jina lingine Peter Alex Kitalamo, ambaye ni mkazi wa Uzunguni Wilaya ya Urambo, mkoani Tabora anadaiwa kumuua mke wake Atusege Kitalamo kwa kumchinja na kisha mwili  wake kuutupa mtoni.

Ofisa huyo wa usalama, anadaiwa kutenda kosa hilo, akishirikiana na wenzake wawili kwa imani za kishirikina.

Mbali na Kitalamo, washtakiwa wengine ni mfanyabiashara, Roger Salumu(25) maarufu kama Mayala mkazi wa Utewe, Wilaya ya Urambo.

Mwingine ni Furaha Ngamba (47) mganga wa jadi na mkazi wa Uyogo, Wilaya ya Urambo.

Hata hivyo, washtakiwa hao wanatetewa na mawakili watatu ambao ni Selemani Matauka anayemtetea Kitalamo, Ramadhani Makange anayemtetea Salumu na Hilda Mushi anayemtetea Ngamba.

Ndutu alitoa ushahidi wake jana, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Abdallah Mkama aliyeongezewa mamlaka ya ziada kusikiliza kesi ya mauaji mahakamani hapo.

Msingi wa shahidi huyo kutoa sifa hizo, unatokana na swali alilokuwa ameulizwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Daisy Makakala akishirikiana na Deborah Mushi, kuwa anawezaje kumtambua mshtakiwa mahakamani hapo?

Akijibu swali hilo, Ndutu alidai kuwa atamtambua kwa sababu mshtakiwa( Katalamo) ni mrefu, mwembamba, mweusi ana sura ya upole  na pia anaongea kwa sauti ya upole kama ya mchungaji.

“Mheshimiwa hakimu, Katalamo nikimuona nitamkumbuka kwa sababu ni mwembamba mrefu, mweusi, ana sura ya upole na pia anaongea kwa sauti ya upole kama ya uchungaji au mchungaji,” alidai Ndutu ambaye kwa sasa ni mpelelezi ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni.

Shahidi huyo baada ya kueleza hivyo, watu waliokuwamo ndani ya Mahakama waliangua kicheko na kusababisha hata yeye kucheka.

Hata hivyo, shahidi huyo alimtambua mshtakiwa huyo mahakamani hapo kwa kwenda kumshika begi la kulia akiwa kizimbani.

Awali, akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili Makakala, shahidi huyo alidai Mei 22, 2021 saa tano asubuhi akiwa katika ofisi kituo cha Polisi Oysterbay alipewa maelekezo na bosi wake aitwaye John Makulu ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, kuwa kuna ofisa usalama ameletwa kituoni hapo.

Alidai kuwa, ofisa huyo wa usalama ameletwa na maofisa usalama wa Polisi makao makuu.

“Aliniambia wameleta mtuhumiwa ambaye ni ofisa usalama anayetuhumiwa kwa kosa la mauaji,” alidia Ndutu ambaye kwa kipindi kile alikuwa na cheo cha Koplo.

Alidai mtuhumiwa huyo alijitambulisha kwa jina la Zaburi Alex Kitalamo au Peter Kitalamo.

“Nilikabidhiwa mtuhumiwa huyo nifanye naye mahojiano, nilimuweka nchini ya ulinzi kwa tuhuma za mauaji kisha kuandaa sehemu kwa ajili ya kumfanyia mahojiano,” alidia shahidi huyo ambaye ana uzoefu wa miaka 24 katika jeshi hilo.

“Nilitoka ofisi ya RCO na kumpeleka ofisini kwangu na nilimueleza tuhuma zinazomkabili na kumpa haki zake zote za msingi na pia nilijitambulisha majina yangu na cheo,” alidai.

Aliendelea kudai kuwa wakati anamhoji mtuhumiwa huyo alikuwa na akili timamu na alikuwa amevaa suti ya bluu.

Mtuhumiwa alidai kuwa yupo tayari kutoa maelezo yake hivyo aliandika alichosema na kusaini kisha kujaza fomu ya onyo na hapo ilikuwa imeshafika saa sita mchana.

Alianza kuchukua maelezo ya mshtakiwa saa sita mchana na kumaliza saa nane na baada ya kumaliza kutoa maelezo yake, mshtakiwa alipewa maelezo yake na kuyasoma kisha kuweka saini.

Hata hivyo, shahidi huyo aliomba maelezo hayo yatolewe kama kielelezo mahakamani hapo.

Mshtakiwa baada ya kueleza hayo, Wakili anayemtetea Kitalamo, Seleman Matauka alipinga upokewaji wa nyaraka hiyo kwa kutoa sababu tatu ikiwamo kuwa maelezo hayo yalichukuliwa nje ya muda.

“Kwa mujibu wa sheria, maelezo ya onyo yanapaswa kuchukuliwa ndani ya saa nne tangu mshtakiwa anapokamatwa, hapa tunaelezwa mshtakiwa alikamatwa Mei 15, 2021 saa tatu asubuhi Oysterbay, ofisi za usalama wa Taifa lakini amekuja kuhojiwa Mei 22, 2021, hivyo tangu akamatwe amekaa siku saba ndio akahojiwa, mimi napinga maelezo hayo kutolewa kama kielelezo mahakamani,”alidai Matauka.

Pingamizi la pili, Matauka alidai kuwa nyaraka hiyo iliyotolewa mahakamani hapo ni tofauti na ile waliyopewa wakati wanasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo (Commital Proceedings) kwa kuwa ina kichwa cha habari tofauti na kile walichopewa awali.

Pingamizi la tatu, Matauka alidai kuwa maelezo hayo yalipatikana kinyume na sheria.

“Mheshimiwa hakimu kwa mujibu wa kifungu 166 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai( CPA), inataka ushahidi wowote upatikane kwa njia halali au za kisheria, sasa hapa mteja wangu amechukuliwa nje ya muda, hivyo tunaomba Mahakama ipokee mapingamizi yetu na ikatae kupokea nyaraka hiyo,” alidai Matauka.

Akijibu hoja hizo, Wakili Makakala aliomba Mahakama itupulie mbali pingamizi hizo.

“Pingamizi la pili, litupiliwe mbali mahakamani kwa sababu halina mashiko na kwamba kielelezo hicho kilisomwa katika maelezo ya mashahidi na vielelezo (Commital Proceedings) na kina ushahidi unaoonyesha kuwa nyaraka iliyosomwa ni ile ile” alidai Makakala.

Kuhusu pingamizi la tatu, wakili Makakala aliomba Mahakama kwenda kwenye usikilizwaji wa kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi, uamuzi ambao hakimu Mkama alikubaliana nao kisha kuahirisha kwa muda kesi hiyo.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Desemba 12, 2020 eneo la Kinzudi lililopo Wilaya ya Ubungo na walimuua Atusege Kitalamo.

Inadaiwa kuwa siku hiyo, majira ya usiku washtakiwa Shabani na Ng’amba walivamia nyumba ya Atusege na kumpeleka kwenye mto uliopo karibu nyumba hiyo kisha kumchinja hadi kufa, baada ya kuelekezwa na Zaburi (mume wa marehemu) juu ya imani za kishirikina.

Related Posts