Arusha. Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema kuwa hatakimbia tena nchi kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Lema aliyewahi kuwa mbunge wa Arusha Mjini alikimbilia nchini Canada mwaka 2020 baada ya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais kwa kile alichodai kuhofia maisha yake kabla ya kurejea Februari 2023.
Akizungumza leo Jumamosi Agosti 24, 2024 jijini Arusha kwenye mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa Operesheni Kucha inayolenga kuhamasisha wananchi kukataa dhuluma za uchaguzi ujao wa wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji, Lema amesema msimu huu hatakimbia nchi tena kama alivyofanya awali.
Amesema uonevu wowote utakaofanyika msimu huu kwenye uchaguzi atakuwa tayari kukabiliana nao, bila kuogopa kudhurika.
Mbali na hilo, Lema amewataka wananchi kutoa ushirikiano wanapokuwa wanapambania haki zao kwa kuwa wanaporudi nyuma na kuwaacha viongozi wao wenyewe wanawakatisha tamaa.
“Hakuna watu wanakatisha tamaa nchi hii kama ninyi Wananchi, hapa tunaongea mikakati ya uchaguzi lakini baada ya muda mnarudi nyuma wote na kutuacha wenyewe tunapopata shida.
“Mnasababisha hadi baadhi ya viongozi wenye mioyo midogo wanahama chama kwa sababu yenu, ndiyo maana siwalaumu, hata akina David Silinde na Mchungaji Peter Msigwa waliokimbia kwa sababu ya hatma ya maisha yao,” amesema Lema.
Amesema katika watu waliokamatwa mara nyingi na kuwekwa polisi au kufungwa magereza na yeye yumo lakini ni kwa sababu ya kupigania haki za wananchi ambao wamerudi nyuma kisiasa.
Ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kukataa michezo michafu inayofanyika kwa ajili ya kuufanya uchaguzi usiwe na huru na haki.
“Kuanzia sasa chukueni fomu na kama kuna mtu unamjua ana sifa, nenda kamshawishi achukue fomu na nawahakikishia mkifanya hivyo tutapata viongozi wenyeviti waliotokana na wananchi na nawaambia tutashinda sana endapo mtakuja kushiriki uchaguzi bila hofu wala kurubuniwa,” amesema.
Awali, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amewataka wananchi kuhakikisha wanashiriki hatua zote za uchaguzi na wasilaghaiwe na mtu yeyote kwa kuwa, mwaka huu hawatasusia uchaguzi.
“Miaka mitano tuliyowaachia imewatosha waliopita na wananchi wamenyimwa haki yao vya kutosha, hakikisheni mwaka huu hamkai nyuma kushiriki mchakato mzima wa uchaguzi na mkagombee ili tupate watu wenye uzalendo,” amesema Golugwa.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Elisa Mungure amesema lengo la Operesheni Kucha ni kukataa michezo yote michafu inayofanywa kipindi cha uchaguzi kwa ajili ya kuufanya isiwe wa huru na haki.
“Safari hii msikubali watu wanaokuja kwenye nyumba zenu na kuwataka vitambulisho vyenu au kuwahonga chochote kununua haki zenu, huo sio wakati wa kanga na pombe, bali ni kazi tu kuhakikisha tunarudisha jimbo letu kwa kuanza na wenyeviti wa mitaa,” amesema Mungure.