Mailimbili, mtaa wa kupigiwa mfano katika ushirikishaji wananchi

Dodoma. Wakati nchi ikielekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu, Mtaa wa Mailimbili uliopo Kata ya Chamwino mkoani Dodoma umekuwa mfano wa kushirikisha wananchi kwenye shughuli za maendeleo ya mtaa.

Mtaa wa Mailimbili ulipo kwenye Halmashauri ya Jiji la Dodoma mwaka jana ulishika nafasi ya pili kwa usafi kimkoa, ni mtaa uliopo mjini unaonzia eneo la Chinangali Park kuelekea Barabara ya Arusha.

Ni mtaa ambao wakati wa uzinduzi wa kanuni za uchaguzi uliofanywa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ulipata nafasi ya kuweka banda la maonyesho kueleza mafanikio yao katika kushirikisha wananchi kwenye shughuli za kijamii.

Ofisa Mtendaji Kata ya Chamwino, Lucas Nkelege anasema mtaa wao ulishiriki kwenye uzinduzi wa tangazo la uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kipengele cha ushirikishaji wa nchi, wakitokea Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Ni halmashauri nne kati ya 184, ndizo zilishiriki katika hafla ya kutoa Tangazo la Uchaguzi wa serikali za mitaa 2024, zingine ni halmashauri ya Wilaya ya Singida iliwakilishwa na Kijiji cha Mtipa, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika iliwakilishwa na Kijiji cha Kagunga na Halmashauri ya Wilaya Ludewa iliyowakilishwa na Kijiji cha Mundindi.

Wakati Watanzania wakielekea kwenye uchaguzi utakaofanyika Jumatano ya Novemba 27, 2024 utakaowaingiza madarakani wenyeviti wa mitaa, vitongoji na vijiji ni muhimu wakaelewa viongozi wanaokwenda kuwachagua ndiyo nguzo ya maendeleo yao.

Mtaa wa Mailimbili umefanya vizuri kwenye eneo la ushirikishaji, wananchi wanapata nafasi ya kushiriki katika kila hatua ya mchakato kuanzia kupanga, kutekeleza, kufuatilia, na kutathmini miradi na mipango inayoathiri maisha yao.

Lengo kuu la ushirikishaji wananchi ni kuhakikisha kuwa sauti, mahitaji, na mapendekezo ya jamii yanazingatiwa na kupewa kipaumbele katika shughuli za maendeleo. Ushirikishaji huu unasaidia kuimarisha uwazi na uwajibikaji wa viongozi, kuongeza umiliki wa miradi na mipango ya maendeleo, na kujenga ushirikiano mzuri kati ya viongozi na wananchi.

Pia, inachochea demokrasia shirikishi, ambapo wananchi wanakuwa na nafasi ya kutoa maoni na kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayowagusa.

Faida za ushirikishaji wananchi ni pamoja na kuimarisha uwajibikaji na uwazi, kujenga umiliki wa miradi, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii, kukuza amani na umoja, kuchochea uvumbuzi na ubunifu, kuimarisha ustawi wa kiuchumi, kuwezesha utekelezaji bora wa sera za serikali, kuongeza ufanisi na tija, kutoa nafasi ya kujenga uwezo na ujuzi mpya, na kukuza uwazi na uadilifu katika utawala.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mailimbili, Rehema Majii anasema moja ya mbinu anayotumia katika kushirikisha wananchi ni kuwatumia mabalozi wa nyumba kumi kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mtaa wao.

“Huwa tunawapa taarifa wananchi kupitia mabalozi wa nyumba kumi, kutangaza mtaani kwa spika. Pia, wengine wamezidi umri na akili, hivyo huwa natumia hekima. Mwenzangu mtendaji yeye anatumia sheria zaidi, lakini natumia hekima na busara,” anasema.

Anasema kwa kutumia hekima na kujali utu wa mtu kumemsaidia kujenga imani kwa wananchi anaowaongoza.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chamwino, Lucas Nkelege anasema mtaa huo wenye wakazi 1,399 wanaume wakiwa 712 na wanawake 687, umekuwa na mafanikio mengi kutokana na ushirikishaji wananchi.

Nkelege anasema kwa kushirikisha wananchi wameweza kujenga ofisi ya mtaa na zahanati, kutoa elimu ya lishe kwa jamii ikiwamo kuhimiza uchangiaji wa chakula shuleni.

“Kusimamia vizuri walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ambao asilimia 90 wamejikwamua kiuchumi,” amesema Nkelege.

Amesema wamefanikisha kuibua miradi nyenye faida kwa jamii, akiitaja ya mfano kuwa upandaji wa miti zaidi ya 500 katika mradi wa Tasaf, kuweka sakafu nje ‘pavement’ kwenye jengo la wodi ya wazazi la Zahanati ya Chamwino.

Anasema kwa kushirikisha jamii wameunda kikundi imara cha ulinzi shirikishi kwenye mtaa wao.

Nkelege anasema katika suala la miundombinu walishirikisha wananchi kuchanga fedha kwa ajili ya kutengeneza kalavati kupitisha maji kuelekea korongoni kuepuka changamoto za mafuriko.

Anasema katika suala la usafi wa mazingira wanashirikisha wananchi ambao wamehamasika na kujitokeza kufanya usafi katika maeneo ya wazi, taasisi, korongoni na kuunda kikundi imara cha uondoshaji wa taka ngumu kwenye maeneo ya makazi na biashara.

Nkelege anasema ushirikishaji huo umewezesha kusimamia utoaji na urejeshwaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, akisema zaidi ya asilimia 85 ya mikopo iliyotolewa imerejeshwa.

Kuhusu elimu anasema ushirikishaji umewezesha kuwaibua watoto zaidi ya 50 wenye ulemavu na kuwapeleka kusoma katika shule zenye mahitaji maalumu.

Umhimu wa kushirikisha wananchi

Viongozi wa serikali ya mtaa wana jukumu katika kuhakikisha maendeleo endelevu katika jamii wanazoongoza.

Hii ni kwa sababu wao ni kiungo muhimu kati ya Serikali Kuu na wananchi wa kawaida.

Katika mtaa wa Mailimbili mkoani Dodoma, kama ilivyo katika maeneo mengine, ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za maendeleo umekuwa nguzo muhimu ya kuleta mabadiliko chanya.

Ushirikishwaji huu una faida nyingi, ambazo ni muhimu kwa ustawi wa jamii.

Moja ya faida kubwa ya kushirikisha wananchi ni kuimarisha uwajibikaji na uwazi wa viongozi wa serikali ya mtaa.

Wananchi wanaposhirikishwa kikamilifu katika shughuli za maendeleo, wanakuwa na uelewa wa jinsi fedha za umma zinavyotumika na miradi inavyotekelezwa.

Hii inazuia mianya ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali, kwani viongozi wanakuwa na hofu ya kuwajibishwa na wananchi walio na ufahamu wa kutosha juu ya masuala yanayoendelea katika jamii yao.

Wananchi wanaposhirikishwa katika shughuli za maendeleo, wanajenga hisia ya umiliki juu ya miradi inayotekelezwa.

Hii ni kwa sababu wanakuwa sehemu ya mchakato wa kufanya maamuzi na utekelezaji.

Umiliki huu ni muhimu kwani unawahamasisha wananchi kulinda na kudumisha miradi ya maendeleo.

Pia, ushirikishwaji wa wananchi husaidia katika kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kama vile elimu, afya, na usafi wa mazingira.

Wananchi wanaposhirikishwa, wanatoa maoni na mapendekezo juu ya namna bora ya kuboresha huduma hizo.

Ushirikishwaji wa wananchi pia ni njia muhimu ya kukuza amani na umoja katika jamii.

Wananchi wanaposhirikishwa kikamilifu, wanahisi kuwa sehemu ya mchakato wa maamuzi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hii hupunguza migogoro na malalamiko ambayo yanaweza kutokea pale wananchi wanapohisi kutengwa au kutozingatiwa.

Ushirikiano huu hujenga uhusiano mzuri kati ya wananchi na viongozi wao, na hivyo kuimarisha mshikamano na utulivu katika jamii.

Wananchi wanaposhirikishwa wanakuwa na fursa ya kuleta mawazo mapya na ya ubunifu ambayo yanaweza kusaidia kuboresha miradi ya maendeleo.

Kwa mfano, viongozi wa mtaa wanapowapa vijana nafasi ya kushiriki katika maamuzi na utekelezaji wa miradi, wanachochea uvumbuzi na ubunifu ambao ni muhimu kwa maendeleo endelevu.

Pia, kushirikisha wananchi katika shughuli za maendeleo kunaweza kuimarisha ustawi wa kiuchumi wa jamii.

Wananchi wanaposhiriki katika miradi ya maendeleo, wanapata fursa za ajira na kuongeza kipato chao.

Kwa mfano, miradi ya ujenzi wa miundombinu kama vile barabara, shule, na hospitali inaweza kutoa ajira kwa wakazi wa mtaa.

Viongozi wa serikali ya mtaa wanaposhirikisha wananchi katika shughuli za maendeleo, wanawawezesha kuelewa na kutekeleza sera na mipango ya Serikali kwa urahisi.

Related Posts