Mbrazili Fountain Gate aanika ukweli

ALIYEKUWA kiungo mshambuliaji wa Fountain Gate, Mbrazili Rodrigo Figueiredo Calvalho amevunja ukimya na kusema ukweli wa kilichotokea, akisema hakuifanyia kusudi katika madai ya fedha wakati akichezea kikosi hicho kama wengi wanavyozungumza.

Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho, Septemba 21, 2022 akitokea Sem Clube, aliishtaki Fountain katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kwa kile alichodai kutolipwa wakati wa kuvunjiwa mkataba uliomfanya kuondoka klabuni hapo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Rodrigo anayeichezea kwa sasa Al Rams SC ya Falme za Kiarabu alisema, wakati viongozi wa Fountain wanalipa fedha alizokuwa anawadai, alichelewa kuthibitisha ili wafunguliwe kwa sababu alikuwa hana taarifa.

“Baada ya kufungua mashtaka yangu FIFA suala langu kuanzia pale nilimuachia msimamizi wangu ashughulike nalo, huku mimi nikiendelea na mambo mengine, baada ya kunilipa sikuweza kuthibitisha kwa haraka kwa sababu nilichelewa kupewa taarifa.”

Rodrigo aliyemaliza msimu na mabao mawili ya Ligi Kuu Bara wakati akiichezea Singida Black Stars kabla ya kubadilishwa jina na kuitwa Fountain Gate alisema, sio kweli kama aliifanyia kusudi timu hiyo kwani alichokifanya ni kudai haki yake.

“Wakati naondoka niliridhia kwa moyo mmoja ila nilitaka nilipwe fedha zangu kwa kitendo cha kuvunjiwa mkataba tofauti na makubaliano yetu, baada ya kuona viongozi wameshindwa kutimiza hilo ikanibidi niende mbele kudai haki yangu,” alisema.

Kitendo cha nyota huyo kuchelewa kuthibitisha kulipwa fedha zake na Fountain, kimeifanya timu hiyo kushindwa kucheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo FC, uliotakiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa Lindi Agosti 17.

Baada ya kuthibitisha malipo hayo, kwa sasa kikosi hicho kimefunguliwa kusajili hivyo nyota wote wapya wameingizwa rasmi katika mfumo wa usajili na leo itatupa karata yake ya kwanza katika Ligi Kuu Bara kwa kucheza na Simba kwenye Uwanja wa KMC.

Related Posts