MAELFU ya wafugaji kutoka jamii ya Wamaasai kutoka vijiji 25, vilivyosajiliwa kisheria, ndani ya tarafa ya Ngorongoro, mkoani Arusha, wameandamana wiki hii, kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu. Anaandika Navaya ole Ndaskoi…(endelea).
Wazee, vijana, wanawake – baadhi yao wakibeba vichanga migongoni mwao – walidamka mapema tarehe 18 Agosti 2024, wakiwa na mabango yenye jumbe mbali mbali.
Maandamano hayo, yaliyotikisa mitandao ya kijamii nchini, yalichochewa na madai mengi, ikiwamo kutokuwapo vituo vya kupiga kura kwenye vijiji hivyo.
Kwamba, majina ya wapiga kura wa vijiji hivyo yamehamishwa kinyemela kwenda Kijiji cha Msomera, wilayani Handeni, mkoani Tanga. Msomera ndiko Serikali inadai kuwahamishia wakazi hao kwa hiari.
Wafugaji wa vijiji hivyo, wanadai kuwa Serikali inawanyima haki ya kushiriki katika chaguzi. Kitendo wanachokiona ni ukiukwaji wa wazi wazi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inayompa kila raia haki ya kuchagua ama kuchaguliwa.
Mpango wa Serikali kuwahamisha wafugaji kutoka Ngorongoro ulianza miaka ya 1940. Hata hivyo, mpango huo ulipata msukumo mkubwa kuliko wakati wowote ule mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani 19 Machi 2021.
Katika hotuba yake, Ikulu jijini Dar es Salaam, akiwaapisha mawaziri na manaibu mawaziri, tarehe 6 Aprili 2021, Rais alizungumza kuhusu tishio linaloikabili Hifadhi ya Ngorongoro; hasa mifugo na idadi kubwa ya watu.
Alisema, “Ngorongoro inapotea. Ngorongoro tulikubaliana kwamba ni eneo la aina yake. Watu na wanyama wakae pamoja. Lakini sasa, watu wanazidi zaidi kuliko wanyama. Tulipoingia kwenye huu mkataba kulikuwa na populesheni ya watu 9,000 Ngorongoro. Sasa, wapo sijui elfu 60 (anasimama Waziri Damas Ndumbaro] wako elfu 90. Elfu 90 mpaka laki moja kutoka watu 9,000. Mamlaka, wizara mko mnawaangalia tu.”
Aliongeza: “Maeneo ya Ngorongoro yanachukuliwa. Kwa hiyo, Ngorongoro inatoweka. Tulikubaliana watu na wanyama wakae pamoja lakini siyo kiasi hiki. Watu laki moja kwa wanyama wale, wanyama watazidiwa tu. Watazidiwa tu…. Kwa hiyo, kama tunataka Ngorongoro ibakie na inauza Tanzania, tuwe serious kuimeintain na kuhakikisha Ngorongoro inabaki kwenye status yake. Kuhamisha watu, sijui mtafanyaje. Lakini kama wameshaingia laki moja wasiendelee kuingia zaidi.”
Hotuba hii ikafuatiwa na matukio kadha yonayokuika haki za binadamu. Huduma za afya ni miongoni mwa huduma za jamii zilizoathirika mara moja. Hospitali pekee iliyoko tarafa ya Ngorongro, ni inayomilikiwa na Jimbo Kuu Katoliki la Arusha. Serikali inadaiwa kuwa ilikataa, kata kata, kutoa vibali vya kukarabati hospitali hiyo ambayo ni kimbilio pekee la halaiki Ngorongoro.
Mwezi Aprili 2022, Serikali ilipiga marufuku huduma ya afya kwa ndege maarufu kwa jina la Flying Medical Service (FMS). Huduma hii ilianzishwa na Jimbo Katoliki la Arusha miaka zaidi ya 40 iliyopita katika wilaya kadhaa za mikoa ya Arusha na Manyara. Wilaya ya Ngorongoro, Longido, Monduli, Simanjiro na Kiteto ziko kwenye Jimbo Kuu Katoliki la Arusha.
Huduma za afya katika wilaya hizo ni duni mno. Barabara, hadi leo, kwa kiasi kikubwa ni za vumbi. Serikali hukarabati barabara hizi kwa nadra sana. Wakazi wa wilaya hizi ambao wengi ni wafugaji waliteseka mno. Kanisa katoliki lilianzisha huduma hiyo ya afya kwa ndege ili kuokoa maisha ya wagonjwa ikiwa ni pamoja na mama wajawazito, watoto na wagonjwa mahututi.
Ndege hiyo ndogo iliweza kutua hadi kwenye nyasi pasipo na kiwanja cha ndege. Ilitua maeneo ambayo hayafikiki kabisa kwa barabara. Ilibeba madaktari na manesi waliotoa huduma kwa jamii kwa ratiba maalum. Wafugaji walifahamu ratiba ya huduma inayotolewa.
Huduma hiyo ilikuwa kama ambulensi. Kwa wastani huduma ilitibu au kuchanja zaidi ya watu elfu 37 kwa mwaka. Hasa kwenye mikoa ya Arusha na Manyara. Kwa dharura ilikwenda pote nchini.
Watoto walipewa chanjo mbalimbali na kupimwa uzito. Huduma iliokoa maisha ya mama wajawazito wengi wenye changamoto za kujifungua. Iliwakimbiza wagonjwa wengi wa dhararu katika hospitali mbali mbali zilizoko Arusha, Moshi na Nairobi.
Kuna madai kwamba serikali ilizuia huduma hii ili wafugaji waweze kuhama maeneo hayo kutokana na kukosa huduma. Haikujali maisha ya wafugaji katika wilaya zingine nje ya Ngorongoro.
Kama ilivyoumiza sekta ya afya, vile vile Serikali imezorotesha huduma ya elimu katika tarafa ya Ngorongoro. Shule nyingi za msingi na sekondari zimenyimwa vibali vya ukarabati majengo kama mabweni, madarasa, vyoo na nyumba za walimu.
Fedha zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya shule za msingi na sekondari katika tarafa ya Ngorongoro zinadaiwa kuhamishwa, bila sababu za msingi, kwenda Handeni. Hii ni pamoja na Serikali kusema kwamba wafugaji wanahama Ngorongoro kwa hiari kwenda huko.
Baraza la Wafugaji Ngorongoro lilianzishwa kwa mujibu wa sheria mwaka 2002. Ilitokana na pendekezo ya Tume ya Prof. Kauzeni. Baraza hili lilikuwa na wawakilishi wa kijamii kutoka katika vijiji vyote 25 na kata 11 zinazounda tarafa ya Ngorongoro. Lengo la baraza hilo ilikuwa kutetea haki za wafugaji wa tarafa hiyo ambayo ndiyo Hifadhi ya Ngorongoro.
Pamoja na wafugaji na mifugo yao kuwepo Ngorongoro, Serikali hukusanya zaidi ya Sh. 100 bilioni kwa mwaka. Ni eneo linaloongoza kwa wingi wa watalii nchini. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ililipa Baraza la Wafugaji Ngorongoro kama Sh. 3 bilioni kwa mwaka. Haya ni makombo ya mapato yaliyotokana na utalii katika ardhi ya urithi ya vijiji vyao.
Serikali, mara baada ya kutangaza mpango wa kuwahamisha wafugaji kutoka Ngorongoro, ilisitisha fedha hizo. Fedha zilihamishiwa akaunti za Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro. Hii imesababisha kuzorota elimu hasa kwa wanafunzi kutoka familia masikini.
Wafugaji waishio tarafa ya Ngorongoro wameteseka kwa miongo mingi. Pamoja na kuwa wanaishi kwenye ardhi ya vijiji vyao hata kabla ya uhuru wa Tanganyika 1961, Serikali hudhibiti hata uhuru wao wa kuzalisha chakula. Kilimo kilikatazwa mwaka 2008 na Serikali ya Jakaya Kikwete kupitia alieyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga. Hakuna njia mbadala wa kupata chakula kwa ajili ya wafugaji hawa.
Mifugo wanaopaswa kutegemewa ni duni. Hakuna huduma za mifugo Ngorongoro. Serikali hukataza mifugo kuchungwa kwenye maeneo yenye malisho mazuri na maji ndani ya eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita mraba 8,100. Mifugo hairuhusiwi kuingia kwenye mabonde ya Ngorongoro, Empakaai, Olmoti, Oldupai, Masek na Bonde la Ziwa Ndutu.
Udhibiti huu wa mifugo umesababisha njaa ya kudumu katika vijiji vyote vya tarafa ya Ngorongoro. Maelfu ya akina mama hulazimika kufanya vibarua vya ujira duni (wakiwa na watoto wachanga migogongoni), kwenye mashamba katika wilaya jirani kama vile Karatu, Meatu, Mbulu, Hanang na Monduli. Kabla ya hapo walikuwa na uwezo wa kujikimu.
Prof. Issa Shivji na Dk. Wilbert Kapinga, katika kitabu chao, “The Rights of the Maasai Living in Ngorongoro Conservation Area,” kilichochapishwa mwaka 1998 walibainisha jinsi Serikali inavyokiuka sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro na hivyo kuvunja haki za wafugaji.
Wanazuoni hao walipendekeza serikali ifuate sheria za nchi na kulinda haki za wafugaji. Ni dhahiri kuwa kuheshimu na kulinda haki za wafugaji hakuathiri Hifadhi ya Ngorongoro.