NIMEONA maneno mengi mitandaoni kuhusu sakata la mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize. Nimeona mijadala mingi kwenye vyombo vya habari pia.
Kuna maoni mengi kuhusu Yanga kukataa ofa tatu tofauti kuhusu Mzize. Inasemekana Wydad Casablanca, Kaizer Chiefs na timu nyingine moja kutoka Ulaya zimetuma ofa Yanga.
Maoni mengi ni kutaka Yanga imuuze Mzize kwa sasa. Kwanini? Kwa sababu ni fursa kwa Mzize.
Sina shida na maoni ya watu. Kila mmoja ana namna yake ya kuona vitu. Kuna ambao wanaamini Mzize akienda kwingine atapata pesa zaidi. Kipaji chake kitakua zaidi. Wako sahihi.
Ila lazima tukubali kuwa zama zimebadilika pia. Yanga ya miaka mitano nyuma sio hii ya sasa. Malengo ya Yanga miaka mitano nyuma sio sawa na sasa.
Yanga kwa sasa ni miongoni mwa timu zenye malengo makubwa Afrika. Ipo katika malengo ya kushindania taji la Afrika. Katika timu sita ama saba zenye malengo hayo Afrika, Yanga ni mojawapo.
Hii ndio sababu Yanga inasajili wachezaji wakubwa kutoka maeneo mbalimbali Afrika. Inachukua wachezaji bora wa ligi nyingine.
Ndio sababu wanaajiri makocha wakubwa. Ndio sababu inawekeza kwa watendaji wakubwa. Lengo ni kufanya vizuri katika mashindano ya Afrika.
Ndio sababu pia inawalipa wachezaji mishahara mikubwa. Ndio sababu inatoa posho kubwa kwa kila ushindi wanaopata ili kutoa morali kwa timu yao.
Katika malengo kama haya jambo kubwa la kufanya pia ni kubakisha wachezaji wako muhimu. Huwezi kuwekeza pesa nyingi kusajili wachezaji mahiri halafu mwisho wa siku unauza wachezaji muhimu.
Ni wazi kwenye mipango ya kocha Miguel Gamondi, Mzize ni mchezaji muhimu. Ndio sababu msimu uliopita alicheza mechi 29 kati ya 30 za ligi. Anafiti katika mipango ya Gamondi. Anafiti katika mbinu za Gamondi. Halafu ana umri mdogo bado. Kwanini Yanga imuuze kwa sasa?
Lazima tutambue kuwa wachezaji wamepanda bei sana. Huwezi kupata straika mzuri Afrika kwa chini ya Dola 200,000. Na ni wachache pia.
Sasa kwanini umuuze straika wako mzuri kwa fedha hizo? Hata unaowauzia watakucheka.
Yaani Yanga imetumia zaidi ya Sh500 milioni kumsajili Prince Dube halafu siku chache mbele imuuze Mzize? Hapana. Yanga wana hoja pia.
Katika zama hizi wakiwa na malengo Afrika, wanapaswa kuwabakisha wachezaji muhimu kama Mzize.
Hizi sio zile zama za kumuuza Saimon Msuva kwenda Morocco ama Heritier Makambo kwenda Horoya ya Guinea. Hizo zimeshapita.
Leo Yanga inaweza kumlipa vizuri Mzize kama ambavyo angeweza kulipwa na timu nyingine kubwa Afrika. Sasa kwanini tuwalazimishe kumuuza? Mzize anaweza kuonwa na timu nyingine kubwa bado akiwa hapo hapo Yanga. Kwanini? Kwa sababu Yanga inacheza mashindano makubwa Afrika. Ina nafasi ya kufika mbali pia tena kuliko hata timu zinazomtaka Mzize kwa sasa.
Nadhani biashara za wachezaji na timu tusipende kuwa na maoni ya kulazimisha. Tuache pande zote ziangalie maslahi yao kisha ziamue kufanya biashara ama la.
Timu zetu zinataka kuweka heshima Afrika ni wakati ambao wanatakiwa kuwekeza sana kwa wachezaji.
Ndio sababu pamoja na kumsajili Clatous Chama na kuendelea kuwepo kwa Pacome Zouzoua, bado Yanga imetumia nguvu kubwa kumbakisha Stephane Aziz KI.
Alifanya vizuri sana msimu uliopita. Akawa mfungaji bora wa ligi na Mchezaji Bora. Maneno yakaanza kuwa mengi kuwa anatakiwa kwingineko, lakini Yanga imembakisha.