Rais Samia asema tamasha la Kizimkazi sasa ni la kitaifa, kimataifa

Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amesema ndani ya kipindi kifupi,  Tamasha la Kizimkazi limekua kwa kasi na kuonyesha tija hivyo kwa sasa limeondoka mikononi mwa wananchi wa eneo hilo na kuwa la kitaifa na kimataifa.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Agosti 24, 2024 wakati akizindua mradi wa ufugaji kasa eneo la Kizimkazi Dimbani ikiwa ni sehemu ya tamasha hilo ambalo lilifunguliwa Agosti 18 na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi. Linatarajiwa kufungwa kesho Agosti 25 na Rais Samia mwenyewe.

Akizungumza katika ufunguzi wa mradi huo, Samia amewaeleza wananchi wa eneo hilo walioasisi tamasha hilo kwamba jina litaendelea kuwa hilohilo, lakini halitaendelea kuwa lao bali limekuwa la kitaifa na kadri linavyoendelea kukua litakuwa la kimataifa.

“Kwa hiyo niwaeleze ndugu zangu, sisi ndio wenye tamasha hili ndio waanzilishi lakini sio la kwetu tena yale mambo ya kugombana kuwa wewe unahusika wewe hausiki hayo tuyaache kadri tunavyoendelea tamasha hili limekuwa sana kwa hiyo limekuwa la kitaifa ila jina litaendelea kuwa hilohilo,” amesema.

Rais Samia amesema mambo wanayotakiwa kufanya sasa ni kujitokeza kutangaza shughuli zao zijulikane katika kimataifa, waendelee kulinda utamaduni wao na kujikuza kiuchumi.

“Tamasha tulianza kidogokidogo sasa limekuwa kwa kasi kwa muda mfupi kila mwaka, kikubwa ni kutumia fursa hii kujijenga kiuchumi, kuchangamkia fursa na kulinda tamaduni zetu na kulinda vijiji vyetu,” amesema.

Rais Samia amesema kutokana na eneo hilo kukua kwa kasi na kuwa na shughuli  nyingi za kiuchumi, hawana budi kuhakikisha wanapingilia ardhi na kuondoa migogoro kwa ajili ya uwekezaji.

Hata hivyo, amewasisitiza wasiuze maeneo yote wakasahau kutenga maeneo kwa ajili ya makaburi ili wasije kukosa maeneo ya kusitiri watu muda unapowadia na kutaka watu walipwe fedha zao za fidia inapobidi kupisha maeneo ya miradi.

Akizungumzia kuhusu utunzaji wa kasa, Rais Samia alimpongeza mwekezaji,  Salaam Carve kutunza viumbe hao kwani wanaendelea kupotea lakini kutokana na ufugaji huo utasaidia kuwatunza.

Mbali na kulinda mazingira na kuwatunza viumbe hao, amesema utaongeza ajira na kukuza uchumi.

Amempongeza mwekezaji huyo kwa kuwekeza mradi huo ambao watu walikuwa hawazioni kama ni fursa. “Nikupongeze sana umeona utumie fursa hiyo kutumia mapango haya,”amesema.

Akizungumza kuhusu changamoto zilizowasilishwa kwake ikiwemo ya umeme mdogo, Rais Samia amesema tayari ameshadokezwa kwamba kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa kituo cha umeme katika mkoa huo,  hivyo tatizo hilo litakwisha huku akieleza jinsi ambavyo na yeye amekuwa akiathiriwa na tatizo hilo kwenye ujenzi wa nyumba yake.

Pia alisema tayari amepata mipango kwamba Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi anaendelea na mipango ya kujenga barabara hivyo tatizo hilo pia ndani ya muda mfupi litakuwa limeisha.

Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dk Ashatu Kijaji kwa niaba ya Waziri wa Malisili na Mambo ya Kale, Ramadhani Soraga, amesema katika mradi huo wameajiriwa watu 19 mpaka sasa.

“Vijana hao wamejiriwa kuwahudumia watalii, eneo hili ni muhimu kwani linatengeneza ajira na kukuza uchumi mtu mmojammoja na Taifa kwa ujumla, Na hii inakwenda kuwa motisha na sisi tunaahidi kuendelea kutunza mazingira na kuendelea kuweka vivutio vingi kujenga uchumi,” amesema.

Awali Mkuu wa mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud amesema baada ya kukamilisha tamasha hilo watakuwa wameongeza vivutio viwili likiwemo tamasha lenyewe ambapo tayari kamisheni ya utalii italiingiza kwenye vivutio vyake hivyo kufanya mkoa huo uwe na vivutio jumla ya 19.

Amesema awali wageni walikuwa wanakwenda kutembelea vivutio viwili pekee katika eneo hilo, lakini  kwa sasa vitakuwa vinne ikiwa ni pamoja na kivutio cha Dolphine, msikiti wa historia, tamasha na uhifadhi wa kasa  na hivyo kuongeza kipato cha wananchi.

“Tuna mipango mingine kuongeza vivutio ili mkoa huu uendelee kufunguka kwa kiwango cha juu,” amesema.

Malengo makuu ya salaam Curve ni kutoa elimu, kuendeleza ufugaji na kujenga sehemu ya makumbusho yatakayohifadhi mila, historia na tamaduni na kushirikiana na wadau mbalimbali.

Kasa hao watakuwa wanatunzwa kwenye hifadhi hiyo kisha wanaachiwa ambapo itasaidia kuongezeka kwa viumbe hao ambao wanatajwa kuwa hatarini kutoweka.

Related Posts