Dar es Salaam. Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imezindua mwongozo wa usimamizi wa kemikali ya ammonium nitrate lengo kulinda usalama wa nchi unaoweza kutetereka endapo kemikali hiyo itatumika bila kuzingatia sheria.
GCLA imesema kuanzia 2019 hadi Julai 2024 tani 130,000 za kemikali za Ammonium Nitrate zimeingizwa nchini kwa ajili ya matumizi na nyingine kusafirishwa kwenda nchini Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kemikali ya amonium nitrate hutumika kutengeneza milipuko ya kupasua miamba migodini wakati wa utafutaji wa madini na ni chanzo cha naitrojeni kwa ajili ya mbolea mashambani, utengenezaji wa dawa na kutumiwa shuleni kwa ajili ya mafunzo.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa pamoja na matumizi hayo yenye tija endapo kemikali hiyo haitahifadhiwa au kutumiwa kwa usahihi inaweza kuwa chanzo cha mlipuko mkubwa utakaosababisha upotevu wa maisha ya wananchi na mali zao.
Mwongozo huo uliozinduliwa umeelekeza kemikali ya ammonium nitrate ihifadhiwe eneo lisilo na chanzo cha moto, mlipuko au kurundika kemikali husika kwani ni hatari.
Eneo la kuhifadhi kemikali hiyo kwa mujibu wa muongozo huo, ni jengo imara lililojengwa kwa matofali au nondo na lazima liwezeshe mzunguko wa hewa na sakafu iwe isiyoshika moto.
Katika eneo ambalo kemikali hiyo imehifadhiwa uvutaji wa sigara hauruhusiwi wala kutumia vyanzo mbadala wa nishati kupata mwanga lakini pia kemikali hiyo inapaswa kulindwa kuepusha wizi utakaochangia ammonium nitrate kutumika kwa matukio ya uhalifu.
Akizungumza katika hafla ya kuzindua mwongozo huo leo Agosti 24, 2024 Mkemia Mkuu wa Serikali Dk Fidelice Mafumiko amesema kemikali hiyo isiposimamiwa vyema ina madhara makubwa ndani ya jamii hivyo uwepo wa mwongozo huo utasaidia kudhibiti kutokea kwa janga lolote wakati wa matumizi, uhifadhi na usafirishaji wa kemikali hiyo.
“GCLA ndio inayosimamia Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali za Viwandani na Majumbani namba 3 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2020, Tanzania inahitaji kemikali kwa ajili ya matumizi ya kiuchumi na kijamii hasa kwenye elimu, dawa, kilimo na uvuvi,” amesema na kuongeza,
“Kemikali hii inaweza kuleta madhara makubwa kwa afya na mazingira endapo zitatumika, kuhifadhiwa au kusafirishwa bila kuzingatia taratibu za kisheria,” amesema.
Dk Mafumiko amesema katika shughuli za uchimbaji wa madini ammonium nitrate hutumika kulipua miamba hivyo nchi ya Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinapitisha kemikali hiyo nchini hivyo kuifanya Tanzania kuwa lengo la usafirishaji.
“Nchi hizi zina kiasi kikubwa za rasilimali madini hivyo kutumia kiwango kikubwa ya ammonium nitrate, kuanzia 2019 hadi Julai 2024 tani 130,000 za kemikali ziliingizwa nchini kwa ajili ya matumizi ya nchi na kusafirishwa nje ya nchi hivyo ni lazima tuimarishe usalama,” amesema.
Akizungumzia mwongozo huo, Mhandisi wa Migodi Tume ya Madini, Zephania Maduhu amesema kila kampuni iliyepewa leseni ya uchimbaji wa madini kupitia mwomgozo huo ni lazima iwe na ghala maalumu la kuhifadhi kemikali ya ammonium nitrate.
Mtaalamu wa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Adrian Kayombo amesema kupitia mwongozo huo kila mtu ana wajibu wa kutunza na kulinda mazingira dhidi ya kemikali hiyo hatarishi.
“Baadhi hawafuati sheria ya mazingira ya kufanya tathmini ya athari kemikali inapoisha wanazitupa bila kufahamu ni hatari ya kutupa kemikali bila utaratibu,” amesema.
Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania, Waheed Saudin amesema ni muhimu wadau kutekeleza mwongozo huo kwa mustakabali wa usalama wa nchi.
Hoja hiyo inaelezwa pia na Mwakilishi wa Kampuni ya Orica Tanzania Limited, Angela Tenga akisema matukio makubwa ya hatari ya kemikali hiyo imetokana na usimamizi usiosahihi hivyo mwongozo huo utakwenda kuondoa makosa wakati wa usafirishaji, uhifadhi na matumizi ya kemikali ya Amonium nitrate.
Kupitia mwongozo huo, kemikali ya amonium nitrate inatakiwa kuhifadhiwa katika eneo ambalo si rahisi kushika moto na jengo lazima liwezeshe mzunguko wa hewa, pia hairuhusiwi kuweka kemikali hiyo karibu na maji kwani husababisha kuganda na hivyo kuwepo kwa hatari ya kutokea kwa mlipuko.
Pia, katika eneo ambalo kemikali hiyo imehifadhiwa uvutaji wa sigara hauruhusiwi wala kutumia vyanzo mbadala wa nishati kupata mwanga ndani ya eneo lenye kemikali hiyo.
Milipuko iliyotokana na kemikali
mwaka 1921, takribani tani 4,500 za ammonium nitrate zilisababisha mlipuko katika vinu vya Oppau, Ujerumani na kusababisha vifo ya watu 500.
Ajali mbaya ya kiwandani katika historia ya Marekani ilitokea mwaka 1947 mjini Galveston Bay, Jimbo la Texas. Takriban watu 581 walipoteza maisha baada ya tani zaidi ya 2,000 zilipolipuka kwenye meli ambayo ilitia nanga bandarini.
Tukio la karibuni ni la mlipuko wa kemikali hiyo na nyingine ambapo watu 173 walipoteza maisha katika bandari ya Tianjin Kaskazini mwa China mwaka 2015.