Simba yapewa Waarabu CAF | Mwanaspoti

Dar es Salaam. Simba itakutana na Al Ahli Tripoli ya Libya katika raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ambapo itaanzia ugenini na kumalizia nyumbani.

Hiyo ni baada ya Al Ahli Tripoli kuitupa nje Uhamiaji ya Zanzibar kwa ushindi wa mabao 5-1 katika mechi mbili za raundi ya kwanza ambazo zote zilichezwa Libya.

Tofauti na Al Ahli Tripoli, Simba ilifuzu moja kwa moja katika raundi ya pili pasipo kucheza raundi ya kwanza kutokana na kuwa miongoni mwa klabu zilizokusanya idadi kubwa ya pointi kutokana na ushiriki kwenye mashindano ya kimataifa.

Al Ahli Tripoli imejihakikishia rasmi kutinga raundi ya pili jana baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Uhamiaji katika mechi ya marudiano iliyochezwa jijini Tripoli, Libya jana.

Katika raundi ya pili, Simba itaanzia ugenini huko Libya, kwa mechi itakayochezwa kati ya Septemba 13 hadi 15 na timu hizo zitarudiana Dar es Salaam, kati ya Septemba 20 hadi 22.

Timu itakayoibuka na ushindi kwenye mchezo baina ya Al Ahli Tripoli itafanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiungana na nyingine 15 kutoka mataifa tofauti Afrika.

Al Ahli Tripoli ilianzishwa Septemba 19, 1950 na inatumia Uwanja wa Tripoli unaoingiza mashabiki 45,000 kwa mechi zake za nyumbani.

Kwa miaka 73 ya uwepo wake, Al Ahli Tripoli mafanikio makubwa ambayo inajivunia katika mashindano ya klabu Afrika ni kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Washindi Afrika mwaka 1984.

Related Posts