Singida BS yaichapa Kagera | Mwanaspoti

SINGIDA Black Stars, wameendeleza ubabe wao katika Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wao, Kagera Sugar.

Mchezo huo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, Singida Black Stars ilipata bao hilo pekee kupitia beki wake wa kati, Anthony Tra Bi Tra dakika ya 90+2.

Mashambulizi ya hapa na pale yaliyokuwa yakifanywa na timu zote mbili, kila upande ulionekana kuwa makini kulinda lango lake kabla ya dakika za jioni wenyeji kulegeza kamba na kujikuta wakifungwa nyumbani.

Huo ni ushindi wa pili kwa Singida Black Stars ambayo sasa inakaa kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha pointi sita kutokana na mchezo wa kwanza kushinda 3-1 dhidi ya KenGold.

Ushindi huo unaifanya Singida Black Stars ambayo zamani ilikuwa ikifahamika kama Ihefu kupata ushindi wa kwanza Uwanja wa Kaitaba baada ya kucheza mara nne, ikipoteza mbili na sare moja.

Kagera Sugar inayonolewa na Kocha Paul Nkata huo ulikuwa mchezo wao wa kwanza wa ligi huku Agosti 29 wakitarajiwa kuikaribisha Yanga uwanjani hapo.

Related Posts